OTHER WEBSITE LISTS


Monday, September 3, 2012

NDIMI ZITEMAZO KWELI!


Mimi si mwanasiasa, japo siwezi kujitenga na siasa kwani ndio mustakabali wa maisha ya mwanadamu kwenye ulimwengu wa mwili.
Ukiachilia ulimwengu wa kiroho, hivi nilivyo leo naakisi siasa za Tanzania, kwa kuwa ndizo zilizozaa sera ya elimu niliyosoma, hospitali niliyotibiwa nilipougua na sasa kazi ninayofanya. Hii ndiyo maana napata ujasiri wa kusema wazi kwamba japo si mwanasiasa lakini siwezi kujitenga na siasa.
Hoja yangu leo imejikita katika siasa, nikimulika kurunzi yangu katika ndimi za aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania), Bw. Edward Ngoyai Lowassa, pamoja na wenzake wanaotajwa sasa katika kasi ya kuwania kiti cha heshima ndani ya jumba jeupe “Ikulu”.
Kimsingi Lowassa anasura nyingi, wengine wamethubutu kumwita shujaa, na baadhi kumwita majina ambayo sina ujasiri wa kuyataja. Wanaomuita shujaa wanadai eti ni mwenye maamuzi, si mnafiki akisema ndio anamaanisha ndio, na hapana anamaanisha hapana.
Wiki jana alivuta hisia zangu nikaamua kumualika kwenye safu hii nikitafakari jambo moja kwa kina miongoni mwa mambo ya kustaajabisha aliyothubutu kufanya.
Akiwa katika kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Luninga ya ITV, ya jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema kamwe hakubaliani na sera ya Kilimo kwanza inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Lowassa, kilichodhamini ubunge wake.
Kwa madai yake, Lowassa, anasema hakubaliani na sera ya Kilimo kwanza kupewa kipaumbele, badala yake angependelea ‘Elimu Kwanza’. Nikiweka kando ubora wa hoja wanazozungumzia wawili hawa ambao mwaka 1995, walipanda ndege moja wakasafiri nchini kusaka uungwaji mkono ili wawanie urais, wakabatizwa jina la ‘Boys II Men’ ingawa  kura hazikutosha na  ‘mr. Clean’  Benjamin William, Mkapa akashinda kwa msaada wa Mwl. Nyerere.
Msimu wa uchaguzi ulipowadia tena (2005) nyota ya wawili hawa ikawaka tena, mmoja akawa Rais na mwingine Waziri Mkuu, ingawa mmoja alipata ajali ya kisiasa kwa kujikwaa kwenye furushi la kashfa ya Richmond na kulazimika kujiuzulu.
Lakini ninalotazama hapa ni moja kubwa! Ujasiri wa kusimama mbele ya hadhira na kumpinga ‘mshirika’ wako wa zamani, tena ukijua ni mwenyekiti wa Chama chako, Rais na Amiri Jeshi.  Ni lazima mtu anayefanya hivyo awe jasiri na shujaa wa kweli anayeweza kusema kweli hata mbele ya upanga.
Katika moja ya tafiti bora zilizowahi kufanywa kuhusu uongozi na viongozi wa bara la Afrika ilitoa majibu haya:
“Bara la Afrika linaangamizwa na dhambi ya unafiki, idadi kubwa ya viongozi na hata waongozwa wanacheka usoni wakati mioyo yao imenuna. Wanasema karibu machoni, wakati moyoni wanatamani uage haraka na kuondoka. Ni wanafiki waliopindukia mipaka.” (utafiti huu ulifanywa na Dk. Moses Herman, wa Oxford University ya Uingereza.
Katika utafiti huo uliohusisha mataifa kadhaa ya Afrika, Dk. Herman anasema wanasiasa wengi wanakataa matokeo ya baada ya kura na hata kuingia msituni kwa kuwa wapiga kura wanafiki waliwapa matumaini ya ushindi mkuu kwa kuwashangilia  kwenye mikutano ya kampeni, wakati kwenye masanduku ya kura walichangua wengine na hilo huwafanya wagombea kudhani wameibiwa kura zao.
Naamini watafiti hao wangemkuta Lowassa, wangeweza kuwa na mtazamo tofauti kwa kuwa yeye amethubutu kuonesha msimamo wa kile anachoamini, hata kama ni kinyume na matakwa ya wengi ikiwa ni pamoja na Amiri Jeshi Mkuu.
Nasema hivyo kwa kuwa msingi wa siasa safi ni ukweli, hata kama ukweli huo unapingwa na wengi, utasalia kuwa ukweli unaodhihirisha imani ya kweli.
Lowassa katika hoja yake anasema anapingana na hoja ya Kilimo Kwanza kwa kuwa haitekelezeki bila wakulima kuwa na elimu ya kutosha.
Akipingana naye, Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka, alisema: “Watu kijijini hawawezi kupokea elimu wakati wana njaa.”
Lo! Hili ni jibu jepesi katika hoja nzito. Nasema hivyo kwa kuwa kilimo cha leo sio kile cha mwaka 47 cha jembe la mkono, kilimo cha leo katika ardhi iliyochoka, kinahitaji zana za kisasa, mbolea kutoka viwandani inayohitaji maelezo ya kitaalam, maofisa ugani walio na ujuzi wa kitaalamu.
Mfano; leo hii tunakula matunda Apple kutoka Afrika Kusini na Israel, tunda moja linauzwa kati ya shilingi 600-1000, Tanzania tuna ardhi kubwa na bora kuliko Israeli, tuna maji ya kutosha na watu wengi kuliko wao, lakini tunapungukiwa jambo moja tu ‘elimu bora ‘ ni  tofauti hiyo, kwamba wao wanajua mbinu za kutumia ardhi kidogo kuzalisha  sana, wakapaki vyema na kusafirisha hadi kwetu watuuzie.
Sisi tunalima mananasi tukivuna tunauza bei chee, na asilimia kubwa yanaoza, kidogo yananunuliwa na waarabu wanakwenda nayo jangwani wanakamua juice na kutuletea kwenye supermarket  tununue kwa bei ya shilingi 3000.
Tuungane na Lowassa kusema kweli kuwa elimu ni ufunguo wa mafanikio katika kila nyanja, kikiwepo kilimo na vinginevyo. Ndio maana hata Biblia takatifu inatutaka kuzingatia elimu.
Tena mahali pengine inasema: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” Sehemu ya maarifa tunayokosa hadi tuangamie kwa njaa na ukosefu wa virutubisho muhimu miilini mwetu ni elimu bora, inayotuwezesha kulima kwa kuzingatia tafiti za kisayansi, zinazoamua udongo gani ulimwe mazao gani, kwa wakati gani, yakishalimwa yalindwe dhidi ya wadudu kwa mbinu gani, na yakishavunwa yahifadhiwe kwa mbinu gani. Bila elimu Kilimo Kwanza ni sawa na kuhifadhi maji kwenye pakacha, hakika yataishia chini hata kama utayakumbatia kama mwana mchanga.
Nimalizie kwa kuwaasa watanzania kuacha unafiki, nyeusi waiite nyeusi na nyeupe waiite nyeupe, hata kama aliyeileta ni bora na mwenye mvuto kiasi gani. Lazima tukue tufikie mahali pa kujadili hoja badala ya mtoa hoja. Tukatae hoja kwa ubaya wake, bila kujali sura ya mtoa hoja.
Nawashauri watanzania wenzangu tutubu dhambi ya kuwa wanafiki, kushangilia huku mioyo imenuna na kununa huku mioyo inacheka. Tabia ya unafiki au kuwa vugu vugu, kujipendekeza kila upande ni ya ushetani na Biblia inaonya watu vuguvugu ikisema:
“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. ……..Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii ukatubu.” (Ufunuo 3: 15-19).
Ingawa andiko lililenga kwa watu wanaoishi maisha ya mseto baina ya shetani na Mungu, lafaa kujifunza leo na kuukimbia unafiki wa aina yoyote ile, kama vile Msafiri alivyopiga mbio kuukimbia mji wa dhambi. (rejea kitabu na filamu ya ‘Safari ya Msafiri’).

Friday, February 24, 2012

PICHA YA MUGABE


KIKONGWE RAIS WA ZIMBABWE ANADAI ETI KAMZIDI YESU KRISTO KWA KUWA YEYE ALIKUFA MARA TATU NA KUFUFUKA LAKINI BWANA YESU YEYE ALIKUFA MARA MOJA, HII NI KUFURU.

Thursday, December 29, 2011

Mauti si ya Kafulila ni mabaki ya ‘zidumu fikra za Mwl

WIKI iliyopita Mbunge wa Kigoma Kusini, (NCCR Mageuzi) Bw. David Kafulila, aligeuzwa ndama wa kafara ili kuhitimisha mgogoro uliokikumba chama chake, alipovuliwa uanachama na kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, hiyo inamaanisha kuwa kijana huyu mwenye umri wa miaka 29 tu, amepoteza ubunge wake, labda utokee muujiza.

Ni bahati mbaya kuwa mwisho wa Kafulila umekuwa hivyo, na haukuwa kama rafiki yake wa siku nyingi Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), ambaye aliweza kuruka vihunzi akafanikiwa kubaki chamani, japo mpango ulisukwa kumtoa. Naam si hao tu, Mbuge wa Jimbo la Wawi kupitia (CUF) Hamad Rashid, naye amekalia kamba ya katani mlimani wakati wowote inaweza kukatika, tayari hoja ya kumfukuza uanachama imewasilishwa chamani na vikao vinaandaliwa. Kisa katofautiana na viongozi wenzake.

Matukio haya matatu, pamoja na yale yanayoendelea ndani ya CCM, yanaashiria jambo moja kubwa! Tatizo la kimfumo na mabaki ya dhana ya iliyotamalaki katika awamu ya kwanza ya utawala wa Tanzania iliyosema; ‘zidumu fikra za Mwalimu,’ ambayo haikutoa nafasi kwa watu ndani ya chama kutofautiana kwa hoja na bado kuendelea kubaki pamoja.

Tukio hilo ambalo kabla ya kufikia uamuzi wake, kulikuwa na misuguano mingi ndani ya chama cha NCCR Mageuzi, huku kukiwa na pande mbili za wanaomuunga mkono Kafulila na wale wa upande wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Bw. James Mbatia, ambapo kwa ujumla wake ilionekana kwamba, Kafulila alikuwa akikinzana na iongozi wa chama hicho kimtazamo.

Itakumbukwa kuwa, mfumo wa siasa za vyama vingi ulianza mwaka 1985, ukirithi ule wa chama kimoja, ni mchanga na wala haujawa na mizizi mizito ndani ya viongozi, vyama na wananchi kwa ujumla. Dhana ya ujamaa ambayo hasa ilijenga msingi wa ‘zidumu fikra za Mwalimu’ umesalia hata kwenye katiba, japo kinachofanyika ni uchumi wa soko.

Pia katika siasa za nchi, mfumo unabaki ule ule wa ‘Zidumu fikra za Mwalimu, yaani mtu mmoja afikiri na wengine watekeleze, hakuna kuhoji wala kujadili mawazo mengine, badala yake utaitwa muasi na kikao kitaitwa kukushushia rungu kichwani.

Ninachotaka kujadili hapa ni ukweli uliofichwa nyuma ya pazia kuwa wabunge, wanachama na hata viongozi wa ngazi za chini katika vyama vyetu vya kisiasa hawako huru kifikra wanapaswa kudumisha fikra za wenyeviti wao na wapambe wao.

Simaanishi kuwa, hawa wahusika mmoja mmoja ambao wamefikishwa kwenye mabaraza ya juu wakitishiwa kuvuliwa uanachama hawana hatia, laa hasha! lakini ninalotaka kuonesha hapa ni kuwa kuna jambo la zaidi ya makosa au uasi wao.

Ninalotaka lionekane hapa ni ukweli mwingine kuwa, ndani ya vichwa vya akina Mbatia, Mbowe, Profesa Lipumba na hata Jakaya Mrisho Kikwete, kuna mabaki ya dhana ya ‘zidumu fikra za Mwalimu’ ambayo yanawanyima nafasi ya kutambua kuwa, wanaweza kutofautiana katika falsafa, lakini wakandelea kufanyakazi pamoja.

Kilichotokea kwa Kafulila, kiliwahi kutokea Zambia, ambapo rais aliyekuwa madarakani alitofautiana na wenzake chamani, lakini kwa kuwa mfumo wao wa sheria ulikuwa umeshaondolewa kwenye dhana ya zidumu fikra ukamuokoa, akaanzisha chama chake haraka na akaendelea kutawala akiwa na chama kipya.

Mchungaji Christopher Mtikila, aliliona hili mapema, akaamua kufungua kesi mahakamani akipinga dhana ya kikatiba ya kuzuia mgombea binafsi, akashinda kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini jopo la majaji, lililoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Augustine Ramadhani, aliamua kuwa Mahakama haina mamlaka ya kikatiba ya kuiamuru serikali kuondoa kifungu cha katiba kinachozuia mgombea binafsi na wakati huo, kulikuwa na siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu kuitishwa.

Ni hukumu hii tata ambayo ilidai eti suala hilo ni la kisiasa, hivyo linastahili kujadiliwa katika majukwaa ya kisiasa iliyoendeleza dhana hii chafu hadi leo, ambayo kwa hakika ni mauti mazito katika siasa za Tanzania.

Ninaamini moyoni mwangu kuwa, ni mauti hii ya demokrasia inayokuza ufisadi kuanzia ndani ya vyama hadi serikalini kwa kuwa watu wamewekwa kufuli mzito midomoni wakithubutu kupinga jambo lolote, wanaitwa waasisi wanafukuzwa na wale wenye mamalaka wanalindwa na mfumo uliopo .

Lakini kama Jaji Ramadhani, katika hukumu yake angezingatia ukweli mwingine kuwa Mahakama ndicho chombo chenye mamalaka ya kisheria, kutafsiri sheria na kutoa haki iliyominywa, angeruhusu mgombea binafsi kwa kuwa hiyo ndiyo hukumu ya haki.

Kwamba kuna mgogoro wa kikatiba na kifungu cha kisheria kimewekwa kwa madhumuni ya kuminya haki za wengine, na kinakiuka haki za kibinadamu na shauri lipo mbele ya Mahakama, ni chombo hicho chenye haki ya kutafsiri na kutoa hukumu na wala si kingine.

Kwa maoni yangu, Jaji Augustine Ramadhani, hawezi kusahaulika kutokana na hukumu hii na nadhani iko siku ataungana nami kujutia maamuzi yake, ambayo leo yanamsindikiza Kafulila mitaani na kuliacha jengo la bunge Dodoma, kubaki katika historia tu huku ikikiacha chama cha NCCR Mageuzi, kubakia na wabunge watatu tu.

Sio Kafulila ambaye amekutana na maswahiba ya namna hiyo, madiwani watano wa CHADEMA, wakitokea Arusha nao walishindwa kufurukuta baada ya maamuzi ya chama hicho, kuwavua uanachama na kuwafanya wapoteze ridhaa ya wananchi ya kuwachagua kuwa, madiwani wao kwenye maeneo yao mkoani humo.

Watu wengine ndani ya NCCR- Mageuzi, ambao waliambatana na Kafulila ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa chama hicho, kwa nafasi ya urais 2010, Hashimu Rungwe, ukiachilia mbali wengine 16 waliopewa onyo kali.

Tanzania kwa ujumla tunapaswa kutambua kwamba, kiongozi si mtu anayejua yote, kuna wakati anaweza kukosea na tujifunze kukubali makosa, pale tunapokuwa tumekosea na si kung’ang’ania eti kwa kuwa ni kiongozi.

Ufisadi mkubwa ambao leo tunaweza kuuona kwenye maeneo mbalimbali ni kutokana na watu kuogopa kusema ukweli, mtu anaogopa kwa kile anachohisi kwamba watu wengine watamuona muasi, tena mwenye kimbelembele. Ni wakati ambao tunatakiwa kubadilika kutoka kwenye fikra za; nitaonekanaje na tujijenge kwenye ukweli na uwazi pale penye ukweli.

Vyama vingi vya siasa Tanzania tumejaribu demokrasi, tunaona tutaweza na hata kusonga mbele, ikiwa tu tutaachana na siasa za woga na kusimamia haki hatakama itatugharimu kwa muda. Ni wazi kuwa huu ni wakati wa kujenga upya siasa zetu tukiwa tayari kulipa gharama ya demokrasia kama ile watangulizi wetu waliyolipa. Ninapowaaga nawashauri watanzania wote kujitambua kuwa wao ndio wajenzi wa siasa safi na utamaduni wa ukweli na uwazi, wanapaswa kusema ndio wakamaanisha ndio na hapana wakamaanisha hapana, wasimpigie makofi fisadi wakimtazama usoni, lakini akiwapa kisogo wanamsonda vidole.

Niweke kalamu yangu chini nikisisitiza kuwa maadui wa Tanzania ya leo ni Watanzania wenzao, ambao wamebobea kwenye unafiki na uzandiki wa kutisha ambao wakiibiwa wanacheka, wakidhulumiwa wanacheka na wakidanganywa wanashangilia usoni japo mioyoni wanalia!

Tuesday, December 27, 2011

IS CHRISTMAS A DAY OR JUST A MESSAGE?



KRISMAS NI SIKU AU NI UJUMBE?

Napenda nianze kwa kuomba radhi msomaji wangu kwa kukatisha makala ya “Masuala yaliyopo leo katika tafsiri za unabii” ambapo sasa tunatazama swali: “Je, kanisa litapita kwenye dhiki kuu? “Makala hiyo tutaendelea nayo wiki ijayo, ila nimewiwa moyoni mwangu leo kukushirikisha ujumbe maalum wa Krismas leo ikiwa ndiyo siku yenyewe. Katika ujumbe huu tutajadili mada niliyoipa jina KRISMAS NI SIKU AU NI UJUMBE?

Katika sikukuu zinazosherehekewa kwa msisimko mkubwa duniani, hakuna inayofikia Krismas. Utafiti unadhihirisha kuwa sikukuu hii inasherehekewa kwenye mataifa mengi duniani kama sikukuu ya kidini na pia ya kitaifa (public holiday). Hii hufanywa hata na baadhi ya mataifa yasiyofuata mwelekeo wowote wa dini. Mambo yafanyikayo katika sikukuu hii mfano, kupambwa kwa mti wa Krismas, kubadilishana zawadi, kutembeleana n.k, yana mizizi yake tokea mbali sana kihistoria. Dunia imekuwa ikisherehekea siku hii kama kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo.

Lakini ni wachache sana duniani wanaofahamu kuwa kwa kweli Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Desemba, wala kwamba tarehe hiyo haina uhusiano wowote na ujio wake duniani. Labda la kushtua zaidi ni ule ukweli kuwa siku hii ilianza kusherehekewa kwa mara ya kwanza mwaka 350 BK (wengine husema ni 354 BK) kama siku ya kuzaliwa kwa Yesu ikiwa na lengo la kubadilisha sikukuu ya kipagani ya Saturnalia iliyokuwa ikiheshimiwa sana siku za dola ya Rumi, kuwa ya Kikristo. Pengine utaniuliza, “kama ni hivyo, je, mchungaji huoni kuwa ni makosa kabisa kusherehekea Krismas kwa kuwa ni kama kuabudu miungu ya uongo, tena ni kudanganya kuwa ni ‘birth day’ ya Yesu wakati sivyo?” Hili ndilo swali na hoja ya wengi wasioamini kuwa ni sahihi kuadhimisha Krismas, na ndiyo maana natamani tujadili leo, ili tuone maana ya kweli ya Krismas na umuhimu wake kwa waamini wa kweli leo. Neno kuu tutakalojifunza hapa ni ule ukweli kuwa Krismas sio siku, ila ni ujumbe tuupatao kutokana na lile tukio la kuja kwa Mwokozi duniani.

Kama mtu akiitazama Krismas kama siku na akaadhimisha siku hiyo kama “birth day” ya Yesu, kama ni mtafiti wa mambo atagundua haraka sana kuwa amekuwa akiadhimisha siku ambayo siyo yenyewe. Lakini baya zaidi, atakuwa amekosa ile maana yenyewe ya tukio la ujio wa Yesu duniani, na hivyo kuadhimisha kwake kutakosa maana. Kwa sababu hii vyema tujifunze undani wa Krismas ili tunaposherehekea tusiwe kama wachezao ngoma wasioijua. Kwa kuanza hebu tuangalie kwa ufupi maana ya neno “Krismas” na historia yake.

Neno “Krismas” wala tarehe ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu havipo kwenye Biblia. Hatuna budi kurejea historia ya Ukristo tuone asili ya neno na historia yake. Huku kutokuwapo mambo haya kwenye Biblia kwenyewe kunaonesha dhahiri kuwa Roho wa Bwana hakuona umuhimu wa kutilia uzito kwenye siku au tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu, ila alitilia uzito kwenye tukio na ujumbe wa tukio lenyewe, kama walivyoandika Mathayo na Luka. Kama tutakavyoona, hata kanisa la kwanza halikutilia mkazo kwenye tarehe au siku ya kuzaliwa kwake, ila maana na uzito wa ujio wake. Hebu tuone ituambiavyo historia kuhusu Krismas:

Maana ya Neno Krismas na Historia yake

Neno "Krismas" kama linatokana na neno la kiingereza "Christmas" ambalo likitafsiriwa moja kwa moja (transliteration) linakuwa "Christ's Mass" ikimaanisha "Kusanyiko la Kristo." Kwa mujibu wa encyclopedia ya Wikipedia, tarehe au mwaka wa kuzaliwa kwa Yesu hasa haujulikani, ila inakisiwa ni kati ya mwaka 7-2 BK. Kabla ya mwaka 350 BK siku ya kuzaliwa kwa Yesu iliadhimishwa tarehe 6 January. Mwaka huo (350) kwa uamuzi wa kanisa la Rumi tarehe 25 Desemba ilianza kutumiwa kama sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu. Hii ni kwa mujibu wa kitabu cha Earle E. Cairns kiitwacho Christianity Through the Centuries (1954, 120).

Kabla ya hapo tarehe hiyo ilitumiwa na wapagani wa Rumi kuabudu mungu wao aliyeitwa Saturn. Katika ibada ya Saturnalia watu walipamba miti, na kupelekeana zawadi. Wengine walitembea uchi mitaani, vitendo vya uasherati na kuua, vilikuwa sehemu ya ibada hiyo. Wapagani hao walipotakiwa kuacha upagani na kuukubali ukristo waliona kuwa kikwazo ni kuacha kuadhimisha siku ya Saturnalia. Kanisa la Rumi likawaruhusu waabudu siku hiyo lakini sio kama kwa mungu Saturn, bali kama kuadhimisha kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo. Hii inashuhudiwa na wanahistoria wengi sio Cairns pekee. Leo ukifanya utafiti kidogo tu kwenye google utakutana na hilo kwa wingi sana.

Kilichofanywa na kanisa la Rumi, yaani kuwaingiza wapagani kanisani kwa kutengenezea sikukuu inayoendana na siku yao ya kipagani kuliifanya hatimaye ibada yao ya kipagani ife kabisa. Lakini kwa kweli hakukuwabadilisha mioyo yao wala hawakugeuka kuwa Wakristo wa kweli. Walipokea dini kama dini lakini sio uzao mpya mioyoni mwao. Historia inatuambia kuwa wapagani hao walikuwa wanasherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kanisani, lakini wakitoka kanisani vile vitendo vya kipagani waliendelea navyo kama kawaida. Hii ni kusema kuwa siku pekee haitoshi kumbadilisha mtu, wala kuadhimisha siku hakumuokoi mtu yeyote.

Tuseme nini basi kwa habari ya siku ya terehe 25 Desemba kuwa Krismas, yaani kusanyiko la Kristo linaloadhimisha kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu? Je, kwa kuwa mwanzo wake kihistoria ni dhaifu kiasi hicho ni dhambi kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu. Je, tunapoadhimisha Krismas tarehe hii ya leo huku tukijua kuwa kweli Yesu hakuzaliwa tarehe kama hii ya leo tunamkosea Mungu wetu? Je, tufanyapo haya tunajiunga na wale wapagani kuabudu mungu Saturn kama wengine wasemavyo? Je, tuache kabisa kutambua kuzaliwa kwa Yesu.

Jibu la hayo yote lipo kwenye kutofautisha kati ya kuiadhimisha siku kama siku, na kuadhimisha tukio la kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu. Kama tukitukuza siku ya tarehe 25 Desemba, kana kwamba ni siku takatifu ya kuzaliwa kwa Yesu, na kuadhimisha kwetu tukakujenga kwenye siku kama vile ni "birthday ya Yesu" tutakuwa tunakosea. Kwanza kwa sababu uzito wa kuja kwa Yesu haupo kwenye siku au tarehe ya kuja kwake bali kwenye maana na ule ujumbe utokanao na kuja kwake. Pili kwa sababu siku au tarehe haituongezei wala kutupunguzia kitu chochote kiroho hata tuitukuze na kuiadhimisha. Kama ingekuwa muhimu kiasi hicho basi Biblia ingetuwekea mazingira ya kujua tarehe ya kuzaliwa kwake na kutuagiza tuiadhimishe, lakini iko kimya kwa habari hiyo. Tatu sio sahihi kusema kuwa Yesu alizaliwa tarehe ambayo hakuzaliwa.

Lakini kama tukiiona tarehe 25 Desemba kama siku tuliyoitenga kutafakari tukio la kuja kwa Yesu Kristo duniani, siyo kwa sababu ndiyo tarehe aliyozaliwa, wala siyo kwa lengo la kuwafanya wapagani waukubali Ukristo kama lilivyofanya kanisa la Rumi, bali kwa sababu kuzaliwa kwa Yesu kuna umuhimu na uzito unaostahili na unaokubalika kibiblia kusherehekewa na kuzingatiwa na wafuasi wa kweli wa Kristo tunatenda vyema, naam, vyema sana.

Neno kubwa hapa ni ule mtazamo tunaokuwa nao kuhusu ile siku, kunakotokana na mahali , yaani hatua tulipo kiroho. Mara nyingi watu walio wachanga kiroho wanapofahamu kuwa kumbe tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu siyo hii, na ya kwamba mazingira yaliyopelekea hata tarehe hiyo itumike kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu ndiyo hayo, dhamiri zao changa hutishiwa usalama, wakidhani kuwa wakiadhimishisha Krismas watakuwa wanaabudu miungu au watakuwa wanasema uongo. Lakini tukumbuke kuwa hakuna siku ya shetani, bali siku zote ni za Bwana. Kwamba kuna watu waliowahi kuabudu miungu siku au tarehe fulani kihistoria, hakutuzuii leo kumwabudu Mungu wetu siku au tarehe hiyo. Tusifanye makosa ya kumkabidhi shetani siku.

Kama kanisa la Rumi lingewapa Injili ya kweli wale wapagani, wakaokoka, kisha wakawaambia kuwa badala ya kufuata ibada mfu za Saturnalia, afadhali siku hiyo mtafakari wema wa Mungu wetu aliyetupenda hata akatuletea zawadi ya Mwanawe wa pekee atuokoe, wangefanya vyema. tatizo halikuwa kwenye kubadilisha siku kutoka kuwa siku ya kumwabudu shetani kuwa siku ya kumwabudu Bwana. Tatizo lilikuwa kuwapa wapagani siku kidini badala ya Yesu mwenyewe aokoaye.

Ujumbe wa Krismas ni Neema ya Mungu sio Siku

Ni sahihi kusherehekea Krismas, tena inapasa, kwa nini? Kwa sababu kwanza, mbingu zinatupa mwongozo huo. Alipozaliwa Yesu Mungu alifanya "Krismas" ya kwanza kwa kupeleka Malaika kondeni walikokuwa wakichunga kondoo wachungaji. Unakumbuka ujumbe wa Malaika hao? Hebu tukumbushane walivyosema:

Malaika akawaambia, "Msiogope, kwa kuwa mimi nawaletea HABARI NJEMA YA FURAHA KUU ITAKAYOKUWA KWA WATU WOTE, maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa KWA AJILI YENU Mwokozi ndiye Kristo Bwana"....Mara walikuwapo pamoja huyo Malaika, wingi wa jeshi la Mbinguni wakimsifu Mungu na kusema; Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia (Luka 2:10-14).

Hii ndiyo krismas ya kwanza, na kama unavyoona ilifanywa na Malaika. Mkazo wao ulikuwa nini? Je ni siku? la sivyo. mkazo wao ulikuwa: "habari njema ya furaha kuu wa watu wote." Hii habari njema ni kwamba amezaliwa kwa ajili ya kila mtu Mwokozi, Kristo Bwana, hii ina maana kuwa dunia imempata mmoja mwenye uweza wa kumwokoa kila mtu na dhambi zake, taabu zake, na kumpa kila aliyekata tamaa tumaini jipya la uzima wa milele. Hii ina maana kuwa kila mwenye dhambi sasa aweza kupokea uzima bure na kuifanya mbingu kuwa nyumbani kwake. Siku ile aliyozaliwa Bwana ilikuwa ni mapambazuko mapya, ilikuwa ni asubuhi mpya kwa dunia iliyokuwa imewekwa kwenye giza la uvuli wa mauti tangu alipoanguka Adamu baba yetu dhambini. Jua la haki lilizuka likiwa na uponyaji katika mbawa zake, Jua hilo ndiye Yesu, aliyefanyika kuwa jibu kwa kila nafsi iliyochoka, na isiyo na matumaini. Krismas inatuonesha neema kuu ya Mungu aliyetujilia tukiwa wafu kiroho, na waliohukumiwa kwenda jehanamu ya moto, na kutuletea wokovu huu mkuu kwa mkono wa Mwanawe Yesu Kristo.

Huu ndio ujumbe wa Krismas, na ndio tupaswao kuusisitiza, sio siku. Aha, hivyo basi kumbe kwa Mkristo wa kweli, Krismas ni kila siku, ila tu siku tuliyokubaliana kuitenga inatupa nafasi ya kuweka mkazo wa pamoja, na mazingira ya kuuambia ulimwengu uache kutukuza siku na badala yake uinue macho na kumtazama Yesu Kristo awaokoe, na kuwapa ushindi maishani kwani yeye ndiye amani yetu. Waliompokea Yesu wanapokusanyika pamoja mioyo yao huimba "atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia." Hao kama "kusanyiko la Kristo" ndiyo Krismas yenyewe, siyo siku. Ikumbukwe kuwa Krismas ni "Christ's Mass" yaani "kusanyiko la Kristo."

Hii ina maana kuwa kwa mkristo wa kweli Krismas ina mikazo miwili; wa kwanza ni mkazo wa kuelekea juu (vertical emphasis) na mkazo wa kuelekea kwa watu (horizontal emphasis). Mkazo wa juu ni wa ibada. Huu unadai kudumisha moyo wa ibada kwa Mungu na shukrani kwa neema yake aliyotupatia kwa kumleta Kristo kwetu. Malaika walitazama juu wakisema "atukuzwe Mungu juu mbinguni." Mkazo kwa watu unadai tuwapelekee wengine hizi "habari njema kwa watu wote" ili nao wapate wokovu wapokee "amani" ya mioyo yao na kufanyika sehemu ya "kusanyiko la Kristo" ambalo ndilo Krismas ya kweli.

Wengi siku hii ya leo, wanasherehekea Krismas kwa ulevi, uasherati, ugomvi, na wivi. Katika hao, wengi wametoka makanisani mwao, wamepokea mahubiri kwa makasisi, wachungaji, na mpadre ambao nao yumkini mkazo wa mahubiri yao ni siku ya kuzaliwa kwa Mwokozi kuwa ni leo badala ya ile maana ya kuja kwake. Ni wangapi walioenda kanisani leo wamezaliwa mara ya pili na kuokoka? Wengine hata hawaamini kuwa kuna kuokoka duniani, lakini wanadhani bado wanasherehekea Krismas. Hivi haya makusanyiko mengi ya wasemao hakuna kuokoka, kisha wanadai kusherehekea Krismas hawajiulizi kuwa wao ni Kusanyiko la nani? Au wamesahau kuwa Krismas ni "Kusanyiko la Kristo?"

Monday, October 31, 2011

Paka weusi sasa wasakwa


·



Hupelekwa mpakani mwa Kenya na Sudan

· Wengine wahaha kufika Muhimbili kuwasaka nyakati za usiku

BAADA ya Tanzania kutikisa dunia kwa biashara chafu ya viungo vya binadamu hasa wale wenye ulemavu wa ngozi (albino), sasa imeibuka biashara ya paka weusi mkoani Mara wilayani Tarime, ambao husafirishwa hadi mpakani mwa Sudan na Kenya, Jibu la Maisha limeshuhudia.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa safarini kutoka Nairobi nchini Kenya alishuhudia vijana wa Tarime mkoani Mara wakiwa na mifuko yenye paka hai ambao muda wote walikuwa wakilia kwa sauti kali, wakichanja mbuga huku wengine wakitangaza kwa sauti kuwa mwenye paka mweusi ampeleke atanunuliwa kwa shilingi 50,000 tasilimu.

“Soko la paka hawa lipo wazi kuna vituo kadhaa hapa Tarime na maeneo mengine ambayo wanunuzi wana pesa mkononi na ukifikisha tu paka mweusi unakula 50,000 bila maswali…” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mkono ambaye tayari alikuwa na paka wawili waliokuwa ndani ya mfuko wa sanflati.

Jibu la Maisha liliambiwa kuwa paka hao wakishanunuliwa husafirishwa hadi mpakani mwa Sudani na Tanzania na pia mpakani mwa Kenya na Tanzania ambapo kuna wanunuzi wa uhakika wa wanyama hao.

Jibu la maisha lilipofuatilia kwa kina biashara hiyo liliambiwa kuwa katika eneo la Tarime mjini mnunuzi mkubwa ni Mzee Nyongige, ambaye ametoa matangazo kadhaa kwa vijana kuwa mwenye paka mweusi ampeleke, lakini ugumu wa biashara hiyo ni kuwa lazima paka awe mweusi kabisa asiye na doa lolote.

“Unajua sio siri hakuna mtu ambaye hapendi pesa, upatikanaji wa paka si mgumu lakini... kwa kuwa, kwa kipindi hiki wanatafutwa kwa udi na uvumba watakuwa ni adimu, mimi nitahakikisha kwamba ninapata paka na ninawapeleka kwa babu,” alisema Dereva tax mmoja aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Kisha aliongeza: “Kweli kila mtu ni lazima ataichangamkia biashara hii, kwa kuwa kuna paka wengi ambao wamekuwa wakizunguka huku na kule hawana mahala pa kuishi ….hao watasakwa na kuuzwa, tena jijini Dar es Salaam, kwenye hospitali ya Muhimbili kuna paka wengi sana nadhani ninaweza kufikiria kwenda huko.”

Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaonesha kuwa paka hao wanatumika kwa shughuli za kishirikina na kwa kipindi cha mwezi sasa paka wamekuwa wakisakwa kwa udi na uvumba mkoani Mara.

Juhudi za kumpata msemaji wa idara ya wanyama ya mkoa wa Mara hazikufanikiwa, lakini Kamanda wa Polisi wa Tarime Deudedatus Kato, alipoulizwa na Jibu la Maisha kuhusu harakati hizo alisema kuwa, anafuatilia kwa undani habari hizo ili kuona kama zinakiuka sheria za usafirishaji wanyama nchini.

Baadhi ya wazee wa kanda ya ziwa walidai kuwa kuibuka kwa biashara ya paka weusi ambao hutumika katika masuala ya kishirikina kumepunguza kidogo mawindo dhidi ya walemavu wa ngozi yaliyokuwa yakifanywa na watu wenye uchu wa madaraka.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitangaza dau kubwa la fedha kwa mtu atakayetoa taarifa zenye kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaofanya unyama dhidi ya Albino na walemavu wengine kwa lengo la kujipatia fedha bila jasho.