OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, June 26, 2011

Jibu la Maisha! Jibu la Maisha! Jibu la Maisha!

Gazeti lako la Kikristo la kila wiki
Wiki hii lina habari moto moto zifuatazo,
1 Hatimaye kesi ya Biblia yatinga Mahakama Kuu
2 Kauli ya TAG kuhusu habari iliyoandikwa na Habari Leo
* Gazeti lamuomba radhi Askofu Dk.Mhiche
* Katibu Mkuu atoa ilani kwa vyombo vya habari
3 Kanisa Dar lachomwa moto
* Kanisa labaki majivu, nyaraka za kanisa zateketea
4 Atupwa jela miaka 5 kwa kumchapa mwanawe
Mhariri naye asema Katiba mpya isigeuzwe hekaya ya Abunuasi
Gazeti hili pia lina makala mbalimbali za kuelimisha na kufundisha jamii kama;
* Utata wa waraka wa waabudu shetani
* Masuala yaliyopo siku za leo katika tafsiri za unabii
Jibu la Maisha pia lina matangazo kadha wa kadha na linasambazwa nchini
Ukilikosa Jibu la Maisha unakosa kuelimika

Atupwa‘jela’ miaka 5kwa kumchapa mwanae

* Jaji aamuru anyang’anywe watoto wote
Texas, Marekani
HUKU akionekana wazi kujawa na hasira kali, Jaji wa Mahakama ya Wilaya katika mji wa Corpus Christi, Texas, Jose Longoria amemhukumu Bi. Rosalina Gonzales, kutumikia ‘jela ya mafunzo maalumu’ kwa kipindi cha miaka mitano na kisha kumnyang’anya watoto wote baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumchapa mwanaye.
Kwa mujibu wa mtandao wa Christians Headlines, Mama huyo aliponzwa na jirani yake aliyemuona mtoto mwenye umri wa miaka miwili akiwa na michirizi ya fimbo mwilini, akashindwa kuvumilia akamnyakua na kumpeleka hospitalini ambapo madaktari walimchunguza na kugundua kuwa alikuwa amecharazwa viboko.
Jirani huyo baada ya baini hilo aliamua kumpeleka mtoto huyo katika kituo cha piolisi ambapo uchunguzi ulifanyika na Bi. Rosalina Gonzales, kutiwa mbaroni kisha kufikishwa mbele ya Jaji ambaye alikuwa mkali mahakamani kama mbogo akilaani hatua ya mtoto huyo kuadhibiwa na mama yake mzazi kwa kuchapwa fimbo.
Mbele ya Jaji majirani walidai kuwa Bi. Gonzales, amekuwa na tabia ya kuwachapa watoto wake wawili ovyo hali ambayo imekuwa ikiwakera mara kwa mara, ndio maana waliamua kufikisha suala hilo mbele ya Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
Jaji Longoria, kabla ya kutoa hukumu kwa mwanamke huyo, alimtolea maneno makali akimuonya kuwa hiyo ni ilani kwake na kwa wanawake wote wenye tabia kama hizo, kwa kile alichodai kuwa nyakati za kuchapa watoto fimbo zimepita.
Kisha Jaji huyo alisema: “Siku hizi hatuchapi watoto, huko nyuma tulikuwa tukifanya hivyo kwa sehemu, lakini jambo hilo lilitufanya tukutane na migongano mbalimbali, usipige tena watoto.”
Sheria iliyotumika kumtia hatiani mama huyo inajulikana kama: “Pretty simple, straightforward spanking case. ”
Sheria hiyo inasema kuwa mtu anayepatikana na hatia ya kuchapa watoto atahukumiwa kuwa katika jela maalumu yenye uangalizi wa mahakama kwa muda wa miaka mitano, huku watoto wake wakiangaliwa katika vituo vya kulelea watoto.
Mama huyo ambaye inaelezwa kwamba si mtu mwenye upendo kwa watoto au mwenye kujua namna ya kulea watoto, mbali na kupewa hukumu hiyo, aliomba kurudishiwa watoto wake, lakini mahakama imesema haitafanya hivyo hadi itakapomuona kwamba amebadilika.
Utamaduni wa kimagharibi unaojali haki za binadamu kupindukia mipaka, ambao unazuia mtoto kuadhibiwa kuwa fimbo umekuwa ukienea kwa kasi katika mataifa yanayoendelea, ambapo mara kadhaa wanaharakati wamekuwa wakiendesha kampeni ya kupinga adhabu ya watoto mashuleni.
Lakini utaratibu huo ni kinyume cha maandiko matakatifu ya Biblia, yanayoonya kuwa mtoto asinyimwe fimbo kwa kuwa itaondoa ujinga.
Andiko hilo linasema: “Ujinga unafichwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.” (Methali 22: 15).

Kanisa Dar lachomwa moto

* Madhababu yabaki majivu, nyaraka za kanisa zateketea
WATU wasiojulikana wamevamia na kuchoma moto kanisa moja maeneo ya Ilala, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita na kuangamiza madhababu yake ambayo ilibaki majivu matupu, ikiwa ni pamoja na nyaraka mbalimbali za kanisa kuteketea.
Unyama huo ambao unasadikiwa kufanywa majira ya saa nane usiku, ulitokea katika Kanisa la TAG, Shekila Makoka, kata ya Kimanga jijini Dar es Salaam, baada ya Mchungaji wa kanisa hilo, Erasto Kihongo, pamoja na baadhi ya washirika wake kwenda kanisa hapo kwa ajili ya maombi ya alfajiri.
“Ilikuwa ni alfajiri na mapema, majira ya saa 11:00 nilikuwa mimi na baadhi ya waumini tukienda kuomba kama kawaida, lakini kabla ya kufika katika jengo la kanisa tulishangaa kuona moto tena ukimalizikia, unajua kanisa hilo bado tulikuwa tukiendelea na ujenzi,” alisema Mchungaji huyo.
Alisema kwamba, walipozidi kusogea zaidi ndipo walipobaini kuwa, mtu au watu waliokuwa wakihusika na kitendo hicho walikusanya vitu kadha wa kadha na kuviweka pamoja madhabahuni na kisha kuviwashia moto.
“Inaonekana kwamba huyu mtu alikusanya vitu na vyombo mbalimbali vya madhabahuni ikiwa ni pamoja na vitambaa, alivikusanya pamoja na ndipo alipoamua kuvichoma, sijui lengo lake lilikuwa ni nini? Mimi sina ugomvi na mtu yoyote wala sikumbuki hata kama niliwahi kukwaruzana na mtu,” alisema Mchungaji huyo wa section ya Ilala.
Alisema kwamba, ingawa kitendo hicho kilifanyika wakati wao wakiwa wamejiandaa kabisa kuingia kwenye maombi, hakikuwafanya waache azma yao hiyo na hivyo waliingia kwenye maombi kama kawaida.
“Kuunguzwa kwa kanisa, hakutufanya tuahirishe maombi, tuliingia kwenye maombi na baada ya hapo tulijipanga, wengine walienda Polisi kutoa taarifa ya kuchomewa kanisa, na wengine walienda kwenye Serikali za mitaa” alisema na kuongeza:
“Tulienda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Tembo Mgwaza na tulipewa karatasi ya taarifa RB No. TMG/RB/1736/2011, na walituambia watatupeleka katika kituo kingine cha Stakishari ili tupewe mpelelezi, lakini mimi sikuona ulazima wa kufanya hivyo mimi jambo ninalomshukuru Mungu ni kuwa, kanisa halikuteketea lote, madhababu ndiyo imeharibiwa vibaya.”
Sambamba na hilo alisema kwamba, alikwisha kutoa taarifa kwa viongozi wake wa kanisa Seksheni ya Ilala kwa Mwangalizi Eliya Lugwami na taratibu zingine zinafanywa.

Kauli ya TAG kuhusu habari iliyoandikwa na Habari Leo

* Gazeti lamuomba radhi Askofu Dk. Mhiche
* Katibu Mkuu atoa ilani kwa vyombo vya habari

Na Mwandishi Wetu
KANISA la Tanzania Assemblies of God, (TAG) limetoa ufafanuzi kuhusu habari iliyoandikwa kwa makosa na Gazeti la Habari leo katika toleo lake namba 01634, la Juni 12, mwaka huu na kisha kukanushwa na gazeti hilo hilo katika toleo lake la Juni 19, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TAG, Rev. Ron Swai, Kanisa limefanya hivyo kwa faida ya wachungaji wake, waumini na Watanzania kwa ujumla, hasa baada ya kuwa gazeti la Habari Leo lililoandika habari hiyo kwa makosa limekiri kosa, likakanusha na kuomba radhi kwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la T AG, Dk. Magnus Mhiche, ambaye habari hizo zilimlenga zaidi.
Mchungaji Ron, alisema kuwa ameona umuhimu wa kufafanua jambo hilo na hata kuchapisha tena taarifa ya kukanusha iliyoandikwa na Habari leo, sambamba na barua ya kuomba radhi kwa Makamu Askofu Dk. Mhiche, kwa kuwa baadhi ya vipengere katika habari husika, licha ya kugusa kanisa la mahali pamoja, TAG, Mbagala Kizuiani pia ziligusa Kanisa la TAG kwa ujumla pamoja na wachungaji.
“Nitumie tu nafasi hii kuwahakikishia wachungaji, waumini na Watanzania kwa ujumla kuwa taarifa husika zilikuwa zimeandikwa kwa makosa makubwa ya kisheria, kiandishi na kimaadili, kama ambavyo wahusika wamekuwa waungwana kukubaliana na makosa hayo kuomba radhi kama inavyoonyesha kwenye barua yao na taarifa ya kukanusha,”alisema katibu huyo na kuongeza:
“Ningependa pia kuwakumbusha waandishi wa habari, umuhimu wa kuwa makini zaidi katika kufuatilia mambo na kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa wahusika kabla ya kuandika, kwa kuwa madhara ya taarifa zisizo sahihi ni makubwa sana yanaweza kuleta madhara kwa vyombo husika na hata kuvuruga amani ya nchi. Sisi Tanzania Assemblies of God, tupo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanahabari wenye nia njema ya kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kuwapasha watu habari.”
Ifuatayo ni taarifa ya kiungwana ya Gazeti la Habari Leo iliyokanusha habari yao waliyoandika kwa makosa na Juni 12, mwaka huu:
Kumradhi Kanisa la TAG, Askofu Dk Mhiche
JUMAPILI ya Juni 12, gazeti hili liliandika habari yake kubwa ukurasa wa mbele kwamba ‘Kanisa lakumbwa na kashfa ya ngono’.
Habari hiyo ilihusisha Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) na pia kumtaja Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk Magnus Mhiche, kuwa anahusika na kuvunjika kwa ndoa ya muumini wake, Emilius Elisha.
Ilidai pia kuwa baada ya kuvunjika kwa ndoa ya Elisha na mkewe Rose, Askofu Dk Mhiche alimpangishia chumba na pia kumtafutia kazi St Matthew.
Baada ya uchunguzi wa kina, imebainika kwamba tuhuma hizo hazina ukweli, Askofu Dk Mhiche hajahusika na mambo yote hayo na pia Kanisa halihusiki kwa vyo vyote na kuvunjika kwa ndoa hiyo.
Ukweli ni kwamba Elisha si mshirika wa Kanisa hilo baada ya kufukuzwa ushirika Aprili 4 mwaka jana, kutokana na kukiuka maadili ya Kanisa na amekuwa akizusha tuhuma dhidi ya Dk Mhiche kutokana na hasira za kufukuzwa kanisani.
Pia ni kwamba Rose na Elisha wametengana kutokana na sababu za ndani ya ndoa yao na hivi sasa mkewe huyo amepanga chumba chake, baada ya kulipiwa kodi na kaka yake na anafanya shughuli ndogo za kuuza mitumba, kinyume na madai ya awali.
Kutokana na habari hiyo, Kanisa, waumini na Dk Mhiche, ndugu, jamaa na marafiki zake, walipata usumbufu mkubwa, hivyo tunachukua fursa hii kuwaomba radhi wote hao na kuwapa pole kwa usumbufu uliojitokeza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mhiche alisema kuwa inaonekana kwamba kuna watu wenye hila ambao wameamua kunichafua mimi na Kanisa kwa maslahi yao binafsi.
Aliwataka waumini, wachungaji na watanzania kwa ujumla kuwapuuza watu hao na kuendelea kuwa na imani kwa Kanisa huku akitoa mwito kwa wanaotaka kuombwewa kufika kanisani.
“Yawezekana kuna watu wamepanga kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari kama vyenu hivi, kulichafua jina la Kanisa na hata mimi binafsi kwa sababu ya matatizo yao binafsi ambayo hayakubaliki kikanisa.
“Haya ni majaribu ya shetani, hivyo wachungaji na waumini wasikate tamaa kumtumikia Mungu kwa sababu hizi ni nyakati za mwisho na mambo mengi yanaweza kujitokeza … tuwe imara kukabiliana nayo,” alisema Askofu Dk Mhiche.
Alitoa mwito pia kwa vyombo vya habari kuwa makini na watu wa aina hiyo, na kuchuja mambo kabla ya kuyatangaza, kwa sababu mengine ni uzushi ambao unaweza kusababisha athari mbaya kwa jamii. – Mhariri.”
Pamoja na habari hiyo, Gazeti la Habari leo pia liliandika barua kwa Makamu Askofu mkuu wa TAG, DK. Magnus Mhiche yenye kumbu kumbu namba; Kumb. Na. : JK/E-HL/TSN/455/2011, kumuomba kiongozi huyo wa kiroho msamaha na kumshukuru kwa kukubali kwake kusamehe. Ifuatayo ni barua hiyo:
“Makamu Askofu Mkuu – TAG (Askofu Dk. Magnus Mhiche),
Tanzania Assemblies of God (TAG),
S.L.P. 70144,
DAR ES SALAAM.
YAH: KUMRADHI NA SHUKRANI
JUMAPILI ya Juni 12, Gazeti letu la HABARI LEO Jumapili, liliandika katika ukurasa wa mbele habari iliyokuhusisha wewe na kanisa na kuvunjika kwa ndoa ya Emilius Elisha ikidai kuwa kuvunjika huko chanzo ni wewe.
Kwa niaba ya wenzangu wa gazeti hili, nakiri kwamba tulikosea kuiandika habari hiyo, huku ukweli ukiwa ni kwamba huhusiki namna yoyote na mtafaruku wa ndoa ya wawili hao na pia kanisa halina mchango wowote katika hilo.
Naelewa maumivu uliyoyapata siku habari hii ilipotoka, naelewa usumbufu uliokupata kutokana na simu ulizopigiwa zikiwamo za kukupa pole na kukutakia uvumilivu. Lakini naelewa pia usumbufu na mkanganyiko uliowapata waumini wako wa kanisa.
Yote haya yalitokana na nguvu za shetani ambazo zilitupofusha, na hata tukashindwa kubaini kuwa tulilokuwa tunalifanya ni kosa, lakini baad ya mazungumzo yetu na wewe (Rejea Juni 15, 2011), tukathibitisha, kuwa tulitumika bila kujua na hivyo kuharibu upande wa pili (wewe na Kanisa).
Tunarudi tena kwa mara nyingine, kukuomba radhi wewe binafsi, ndugu na jamaa zako, kanisa na waumini wake, kwa usumbufu uliosababishwa na habari hiyo na tunaahidi tutakuwa makini zaidi ili hali kama hiyo isijirudie na tutaimarisha uhusiano na ushirikiano wetu kikazi na kiroho pia.
Lakini tunapenda kukushuru wewe na wasaidizi wako, kwa uelewa wenu kwa maelezo yetu, na pia kwa kukubali kutusikiliza na hat akufikia makubaliano ya jinsi ya kumaliza tatizo hili. Hakika mlituonesha moyo wa uvumilivu, upendo na kusamehe.
Hivyo ndivyo binadamu katika dunia hii tunavyopaswa kuishi kwa kukubali makosa na pia kusameheana na hayo ndiyo mapenzi ya Mungu wetu.
Tunakuombea wewe, wasaidizi wako na waumini kwa ujumla kwa Mungu aendelee kukupeni nguvu hizo za kukubali kupokea wakosefu wenu na kukaa pamoja nao mezani na kukabili matatizo yaliyo mbele.
Tunaamini msamaha uliotupa ulikuwa ni wa dhati, nasi tunaahidi kuendelea kushirikiana na Kanisa kwa mema nay ale yanayoepusha migongano miongoni mwetu.
Ahsante sana. Mungu awaangazie
Joseph Kulangwa
MHARIRI MKUU HABARILEO.”

Monday, June 20, 2011

Kumtambua Mwenzi kwa Kutumia Karama za Roho Mtakatifu


Maono ya mchana: “Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasena, kuna nini Bwana? Akamwambia sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” Matendo 10:3-4.
 
Ni vema mkafunuliwa nyote wawili!
 
  Mtume Petro pia aliona maono mchana waziwazi bila kuwa katika usingizi. Mungu anapotaka kukufunulia mwenzi wako kwa njia ya maono ya usiku au ya mchana (ya waziwazi), atafanya hivyo pia kwa mwenzi wako mtarajiwa ili asiwe na tashwishi utakapochukua hatua na kumwendea.
  Ndiyo maana Mungu aliposema na Kornelio kwa habari za wokovu wake, na kumuunganisha na Petro ambaye kwa mila za Kiyahudi hakuruhusiwa kuingia kwa watu wa mataifa, kwani Kornelio alikuwa Mrumi, Roho Mtakatifu aliyemfunulia Kornelio alifanya hima kumfunulia na Petro pia, ili asipate tashwishi na kukataa kufuatana na wajumbe waliyotumwa naye.
Tunsoma: “Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana, akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao wataambao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia kusema, ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikamwambia, vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokelewa tena mbinguni.
  Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
  Na Petro alikuwa  akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako… Hata siku ya ili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao… Matendo 10:9-23.
 
Karama mbili zimetumika
 
  Katika kisa hiki tumeona kuwa Kornelio na Petro, wote wawili, walipata maono waziwazi kwa nyakati tofauti. Kornelio saa tisa za mchana na Petro saa sita adhuhuri. Pia tumeona kuwa Baada ya Petro kupata ugumu wa kutambua maana ya yale maono, Bwana alimsaidia kwa kutumia karama nyingine tofauti, yaani ‘kusikia Sauti ya Roho Mtakatifu’ akimwambia kuwa nje kuna watu watatu ambao wanamtafuta na asiwe na tashwishi juu yao bali aende nao kwani yeye Bwana ndiye amewatuma kwake.
  Kweli akatoka nje na kukuta kuwa ni watatu kama alivyokuwa ameambiwa na Roho Mtakatifu, hivyo akasema kwa ujasiri “mimi hapa ndiye mnayemtafuta.” Lengo la Roho Mtakatifu kumwambia kuwa huko nje anasubiriwa na watu watatu, ni kumwezesha kuthibitisha kuwa kweli watu hao ni watatu na hivyo wametumwa na Mungu. Hii pia ilikuwa ni ishara ya kuthibitisha maono aliyopata.
  Hata katika kumtafuta mwenzi. Kama binti atafunuliwa na Roho Mtakatifu kwa njia ya ndoto, njozi, maono au sauti ya Mungu, si vema akuurupuke na kwenda kumtamkia mvulana kuwa yeye ndiye mchumba wake. Kawaida ya Waafrika mvulana ndiye humtamkia binti kwanza. Ukifanya tofauti, unaweza kutiliwa mashaka na kupoteza muujiza wako.
  Usiogope kwamba mtarajiwa wako anaweza kujua kuwa anatakiwa kukuchumbia, kwani Mungu yule aliyesema na wewe kwa njia ya ndoto, njozi, maono au karama nyingine yoyote, atasema na mwenzio pia, ili yeye ndiye aje, kama wewe ni binti. Na kama mvulana ndiye kafunuliwa, asimlazimishe binti kuamini kuwa kweli kafunuliwa na Mungu. Kwa nini? Kwa vile mafunuo hayo ni sharti kwanza yathibitishwe kwa binti naye kufunuliwa. Kama hajafunuliwa na moyo wake ukajisikia vibaya juu ya jambo hilo na kukosa amani, huyo anaweza kuwa si Mungu aliyekufunulia.
  Ndiyo maana ni lazima pande zote mbili zithibithishe na kujiridhisha kila upande kuwa kweli Mungu ndiye ameanzisha jambo hilo. Kinyume chake unaweza kudanganywa na mtu aliyepata maono batili kutokana na jinsi anavyokupenda au anavyokutamani, mkaoana nje ya mapenzi ya Mungu, ndoa yenu ikawa ngumu kupindukia na kuwafanya muishi katika mateso maisha yenu yote!
  Mimi nilipoona maono kuhusu binti ambaye sasa ndiye mke wangu, nilikuta kuwa yeye alitangulia kushuhudiwa moyoni mwake, lakini akaogopa kunitamkia. Nilipopata uhakikisho wa Roho Mtakatifu na kumtamkia, hakupoteza muda kuomba kwani alikuwa tayari anafahamu jambo hilo. Na hata Shetani alipojaribu kupinga tusioane, alishindwa waziwazi kwani tulimshambulia sote wawili mpaka tukafanikiwa kuoana. Na sasa tunaishi maisha mazuri ya ndoa na ya utumishi.
  Baadhi ya ndugu walikuwa wamenuia kuuvuruga uchumba wetu ati kwa sababu tumekaa muda mrefu bila kuoana wakati yeye (mchumba wangu) akisoma nje ya nchi. Tulimlilia Mungu kwa sauti moja na mchumba wangu mpaka nikapangiwa mahali na siku ya arusi. Alirudi nchini tukafunga ndoa, mambo yote yakeenda vizuri, tukaziona baraka za Bwana. Hata kwako Bwana atafanya kama unamtumikia kwa uaminifu.
 
Roho Mtakatifu habadiliki!
 
  Watumishi wote wa Mungu wa Agamo la Kale na wa Agano Jipya walitumiwa na Mungu kwa maono, njozi ndoto na mafunuo. Hata wewe Mungu anaweza kukutumia leo hata ukaweza kutambua kirahisi mwenzi wako wa maisha. Tunasoma kuwa Danieli alikuwa na ufahamu “katika maono na ndoto.” (Danieli 1:17). Mtume Paulo alijaliwa kupata “maono na mafunuo ya Bwana,” yakamsaidia sana katika huduma yake (2Kor.12:1). Wewe pia Mungu anakutambua na atakuwa tayari kukutumia kama umeamua kumtumikia kwa uaminifu. Bwana atakuongoza, sio tu katika kumtambua mwenzi wako wa maisha, bali katika kila jambo utakaloamua kufanya kwa ajili ya Bwana na kwa ajili yako mwenyewe.
 
  Itaendelea.....
 

Mbwa mwitu wamevamia zizi la kondoo!

Katika siku za karibuni, kumekuwa na wimbi la migogoro katika jamii na hata kwenye nyumba za ibada ambayo kwa njia moja au nyingine imekuwa ikichafua hali ya hewa, na kuzorotesha kazi ya Mungu na hata maendeleo ya wanadamu katika sayari hii.
  Tumeshuhudia  ikiibuka migogoro mingi,  tena isiyo na sababu za kuibuka kwake. Uchunguzi rahisi unaonesha kuwa vyanzo vya migogoro hii ni baadhi ya watu wanaodai kuwa miongoni mwa waumini makanisani, ingawa tabia zao na mwenendo haiendani na Ukristo  kabisa. Ni watu hao ambao mara nyingi huibua migogoro, isiyo na kichwa wala miguu na kisha kukimbilia kwenye vyombo vya habari kutoa malalamiko dhidi ya viongozi na hata waumini wenzao.
  Ni kwa sababu hiyo, tumeamua kutumia nafasi hii kulionya Kanisa la Mungu kuwa macho, kwa kuwa limevamiwa na kundi la mbwa mwitu ambao ni mawakala wa ibilisi wenye lengo la kulichafua kanisa kwa kujifanya waumini na kisha kuibua migogoro ya ndani.
  Hatuna haja ya kutaja majina ya wahusika, ingawa wengi tunawafahamu na tunaushahidi wa kuthibitisha kuwa wamekubali kutumiwa na ibilisi kuwa mawakala, wakipenya makanisani na kumwaga sumu hasa kwa waumini wachanga.
  Tunawasihi waghairi njia zao mbaya na kumrudia Yesu Kristo, kwa kuwa yupo tayari kuwasamehe na kuwapa nguvu za Roho Mtakatifu, zitakazowawezesha kuushinda uovu, lakini wakishupaza shingo watapotea milele.
  Haya si mambo mageni sana, yalikuwepo tangu awali  na hata mitume 12, waliokuwa na Bwana Yesu alipokuwa katika umbo la mwili hapa ulimwenguni zaidi ya miaka 2000 iliyopita, alikuwepo mmoja ambaye alikuwa wakala wa shetani na mwisho alimsaliti.
  Lengo letu kuyaandika haya ni kulitahadharisha Kanisa la Kristo kuwa makini na watu wanaojiafanya waumini tena wengine wakijifanya kuokoka, kwa mbwembwe na kueleza historia ya uchawi mwingi waliokuwa wakiufanya huko nyuma, lakini baada ya muda utasikia ama kaiba na kukimbia au kaibuka na migogoro .
  Tunajua kuwa mambo haya hayafanyiki kwa bahati mbaya, la hasha, huu ni mkakati maalumu wa ibilisi wa kukabiliana na kansia. (tazama habari katika Uk. 1).
  Tunakuwa na ujasiri wa kuyasema haya, kwa kuwa  mawakala hawa wamejaribu mara nyingi  kupenyeza sumu zao kupitia vyombo vya habari likiwepo gazeti hili, lakini kwetu waligonga ukuta kwa kuwa tumejizatiti kuilinda imani na kamwe hatuwezi kuwa daraja la kufanikisha kazi za ibilisi.
  Tunavishauri pia vyombo vya habari nchini, kuwa makini na taarifa wanazoletewa, wasizikimbilie bali wazipime ili kubaini uhakika wake, wachunguze sababu za waleta taarifa zilizojificha nyuma ya pazia na ikiwezekana wawasaidie kwa kuwakemea, kwa kuwa  kazi wanayofanya ya kuchafua wengine haina tofauti na ile iliyofanywa na wale waliotunga mashtaka ya uongo ili Yesu kumtia Yesu mikononi mwa wauaji.
  Kabla ya kushika kalamu na kuandika tuzikumbuke zele Ole …..alizozitoa Bwana Yesu katika Biblia kwenye kitabu cha Mathayo.
  Pia waumini wenye mioyo safi, wanapaswa kuwa makini na kukwepa mitego ya mawakala hawa ambao hujaribu kuwatumia kama daraja ili kufanikisha malengo yao yasiyokuwa wazi.
 
 

 

Viongozi wa dini wavunja ukimya posho za Wabunge

Na Waandishi Wetu
 
MJADALA kuhusu malipo ya posho kubwa kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali, ulioibuliwa  bungeni na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), na baadaye kuungwa mkono na kambi ya upinzani, umeingia  katika hatua mpya baada ya viongozi wa dini na wanaharakati wa makundi ya kutetea haki za binadamu, kuvunja ukimya na kutoa kauli kali.
  Wakiongea na na Jibu la Maisha, kwa nyakati tofauti viongozi hao wa dini na wanaharakati juu ya hoja hiyo ambayo imekuwa gumzo kwa watu mbalimbali walisema kwamba, ni lazima wabunge waangalie haki na usawa kwa watu wote na hasa mtanzania anayeishi chini ya dola moja kwa siku.
  Askofu Msaidizi Jimbo la Kagera, Methodius Kilaini alisema kwamba, kwa sasa imeonekana kana kwamba bungeni ni sehemu ya biashara na ndiyo maana watu hukanyagana kusaka kupata nafasi hizo, ambapo hata wanapozipata hawawazii tena wananchi isipokuwa namna ya wao kujineemesha na posho.
  “Hii sasa imekuwa kama ni biashara, wewe fikiria mwananchi wa kawaida anavyoishi kwa shida halafu bado watu wanaodai ni wawakilishi wao wanavyoishi; badala ya kuwatetea, wao wanaangalia matumbo yao pamoja na familia zao tu,” alisema Askofu huyo na kuongeza:

  “Hawa wana alawansi nyingi, mimi naona wangebaki na hizo tu badala ya kupewa nyingine katika vikao vyao,  sambamba na madai ya kuongezewa posho.”
  Alisema kwamba ikiwa wasomi wa taaluma mbalimbali nchini na wengine hutumia muda mwingi kukamilisha kile wanachokiita hulipwa pesa kidogo, iweje wabunge walipwe mamilioni kwa kukaa na kusikiliza mijadala kwa muda mchache?
  “Pesa wanazopata kwa mwezi zinawatosha kabisa, hizo posho wanazolipwa zipelekwe kwa watu wa kawaida; nadhani Zitto Kabwe kaona mbali alikuwa sahihi kabisa kugomea,” alisema mtumishi huyo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kagera.
  Mwanaharakati mwingine ambaye naye alitoa maoni yake ni Bw. Emmanuel Kibona ambaye alisema kwamba, Katika Biblia Yesu anashauri kuwa; asiyefanya kazi na asile, hivyo posho zinazotolewa kwa ajili ya mtu kukaa tu (sitting allawance) ni dhambi mbele za Mungu.
  “Hapo hakuna kazi, wazi kuwa kupokea posho hizo ni dhambi kwa kuwa hakuna kazi inayofanyika, kupokea malipo bila kufanya kazi ni dhambi na inaashiria kukosa uaminifu na umakini kwa wanadamu na Mungu pia,” alisema mwanaharakati huyo.
  Alibainisha kuwa, Wabunge huwaongoza wapiga kura ambao ni masikini kiasi kwamba, kupata mlo mmoja kwa siku ni shughuli, lakini wao kwa kutoogopa au kutomjali mwananchi  hukubali kulipwa posho kwa kukaa tu!
  Sambamba na hilo alibainisha kwamba, Posho wanazopewa wabunge katika vikao vyao ndizo zilizolifilisi taifa, kiasi cha kuweka matabaka ya wenye nacho na wasio nacho. Huku akiongeza kwamba ni bora posho hizo (sitting allowance) ziondolewe.
  “Sio hilo tu, pia hata pesa zinazotolewa kwa watendaji wa serikali ni heri nazo zikafutwa kabisa ili kulinda utawala bora na uadilifu, posho hizo zinasababisha watu wang’ang’anie madaraka serikalini na kutafuta ubunge kwa nguvu.
  Mwenyekiti chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, naye hakuwa nyuma akiongea na Jibu la Maisha alikuwa na haya ya kusema: “Hakuna haja ya POSHO, pesa hizo zinatakiwa zipelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kwa wapiga kura.”
  Alisema kwamba, mashuleni kuna upungufu wa majengo ya madarasa, vyakula na vifaa vingine vya kusomea, hivyo ni bora likaangaliwa hilo ili pesa hizo zikapelekwa huko katika kuondoa changamoto zinazowakabili wananfuzi na walimu kwa ujumla.
  Pia aliongeza kwamba, wajawazito kwenye vituo vya afya wanapata shida wakati wa kujifungua, hiyo ikiwa busara kidogo itatumika  kwa wabunge basi wataona umuhimu wa kuchukua pesa hizo na kupeleka hospitalini.
  Akizidi kutoa mchanganuo Bi. Nkya aliongeza kuwa, suala hilo pia linaleta ubaguzi katika taifa kutokana na kwamba wako watu wengi ambao ni masikini, na wengine wachache ambao wananawiri kutokana na pesa hizo pasipo kujali wenzao.
  “Kuna wengine ambao hizo shilingi 70,000 wanazopewa wabunge kwa siku, ni mshahara wao wa mwezi mzima na unaishia kulipa madeni na anarudi nyumbani akiwa na kiasi cha shilingi 10,000; sasa hapa usawa uko wapi.
  Mchungaji Christoper Mtikila ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu alisema kwamba, kuongezeka kwa mambo ya kifisadi na rushwa  imesababishwa na vitu vinavyofanana na hivyo, watu kupenda sana pesa.
  “Mtu kasomea udaktari karibu miaka 21 lakini anacholipwa ni kama hakuna kitu, halafu mtu mwingine akae tu, muda mchache alafu akitoka hapo analipwa pesa nyingi, hii ni njia mojawapo ya kusababisha rushwa nchini, ndiyo maana kila mtu anapakimbilia huko,” alisema Mtikila.
  Wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe  Zitto, toka kambi ya upinzani CHADEMA aliibua hoja akitaka posho wanazopewa katika vikao zifutwe, huku akitaka pesa hizo zipelekwe kwenye mambo ya maendeleo kitu ambacho kiliungwa mkono na watu mbalimbali akiwemo Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba
  Wabunge wamekuwa wakilipwa mshahara shilingi Mil. 2.5  na shilingi milioni mbili za kutumia katika majimbo yao, sambamba na 150,000 za kujikimu kila Bunge linapokaa..

Ask.Kulola asema acheni kunywesha wenzenu

Na Calvin Nyorobi
 
ASKOFU  Mkuu wa Kanisa la EAGT nchini Dk. Moses Kulola, ameonya watu wenye tabia ya kishetani, ambao amedai kuwa wanawanywesha wenzao maji machafu yaliyooshea maiti kwa madai kuwa ni maji ya Baraka.
  Akihubiri katika ufunguzi wa mkutano wa Injili uliofanyika katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, Dk. Kulola alisema kuwa katika siku za karibuni imeibuka tabia mbaya inayofanywa na kundi la kishetani linalojivika ngozi ya kondoo na kujifanya kama ‘kanisa’ mjini Mwanza, lakini likiendesha matukio ya kustaajabisha sana ikiwa ni pamoja na kunywesha watu maji yaliyooshea maiti.
  Bila ya kutaja majina Askofu huyo alisistiza kuwa kundi hilo linalofanya ibada za kishetani, limekuwa likiendesha ibada zake usiku na likiigiza mambo yanayofanyika katika makanisa ya kiroho ikiwa ni pamoja na kuombea watu, lakini amepata ushahidi kuwa wanatumia mambo ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kuwanywesha watu maji yaliyooshea maiti.
  Gazeti la Jibu la Maisha linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu kundi hilo ambalo, kwa mujibu wa Askofu Kulola ni mawakala wa makundi ya kishetani yanayoibuka kwa kasi kubwa katika nyakati hizi za hatari.
  Alisema kwamba ni vema wale walio na Mungu wakaendelea kuangalia wokovu wao ili wasije kuanguka, kwani siku za leo shetani amekuwa akiwatafuta watu waliookoka ili awaangushe.
  “Nasikitishwa na habari za Kundi moja lililopo Mwanza ambalo limeibuka na kioja cha kuwanywesha watu maji ya kuoshea maiti, wakidai eti ni maji ya Baraka; huu ni uchafu mkubwa kwa watu wa Mungu,” alisema mtumishi huyo.
  Akielezea matukio yanayoashiria mwisho wa dunia, Askofu Kulola alisema kuwa kulingana na matukio ya kushangaza yanayozidi kujitokeza likiwemo la unabii wa uongo uliodai kuwa wateule wangenyakuliwa Mei 21, ni wazi kuwa dalili za hatari zimekaribia sana hivyo aliye mtakatifu azidi kujitakasa na yule mwenye kusita sita akimbilie haraka kwa Yesu akajiokoe.
  Kiongozi huyo mwanzilishi wa Kanisa la EAGT, alionya kuwa wanaokimbilia kunywa kikombe cha dawa huko Loliondo Arusha, kwa Mchungaji mstaafu wa kanisa la KKKT, Ambilikile Mwasapila, ni mfululizo wa matukio ya kustaajabisha sana yenye mkono wa ibilisi.
  “Siku moja nilipigiwa simu na waandishi wa habari, nilipoipokea wakanisalimia shikamoo Askofu, niligundua kuwa hawajaokoka hivyo nikawaitikia tu kwa haraka, nao wakasema …… Askofu tumewaona Wachungaji (majina nimeyahifadhi) kutoka Dar nao wamejipanga kupokea kikombe;  na wakaongeza tena kwamba…. hivi Mchungaji mnatupeleka wapi…..? nikawajibu kuwa hao wamepotoka; Mungu wangu mimi haponyi kwa miti shamba,” alisema Askofu Kulola.
  Hata hivyo alieleza kwamba, kikombe ambacho kinapaswa kunywewa na Wakristo wote ambacho hata yeye (Kulola) anacho ni kimoja tu, ambacho ni cha mateso ya Yesu Kristo, na wala si dawa ya miti shamba.
  “Yesu haponyi hivyo, Mchungaji wa Loliondo alitokewa na kitu kingine kabisa na wala si Mungu, aliyemtokea anamjua yeye. Sisi hatuhusu wala hatumuamini,” alisema.
  Katika mahubiri yake aliendelea kufafanua kwamba matukio yanayotokea hivi sasa ni ishara tosha ya siku za mwisho, kulingana na vita zinavyoendelea kupiganwa katika nchi na Falme za kiarabu, na kuwa Wakristo wanapaswa kujipanga ikiwa ni pamoja na kuiombea nchi.
  “Wapendwa nchi yetu ni nzuri mno kuliko nchi zingine, tunaamini sana ndio maana tunapata hata nafasi ya kusali na kuhubiri injili kuliko nchi zingine, tuiombeeni nchi yetu tena kwa machozi; Mungu ainusuru na majanga mabaya yanayojitokeza  sehemu mbali mbali duniani,” alisisitiza.
 

Waraka wa waabudu shetani wasambazwa kwa siri Dar


* Ni maandalizi ya kikao cha Julai nchini
* Wahimizana kufika na damu ya kafara


Na Waandishi Wetu

KILE kinachoelezwa kuwa ni waraka wa siri unaowaalika washiriki wa dini za waabudu shetani  katika mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania, katika kongamano kuu linalotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam, Julai 30, mwaka huu unasambazwa kwa siri kubwa  kama dawa za kulevya, huku ukiambatana na vitisho vikali kwa atakayevujisha siri.
  Gazeti la Jibu la Maisha, limefanikiwa kuunasa waraka huo, unaoonyesha kuwa  umeandaliwa na taasisi inayojulikana kama ‘The Saints Darknes in the world,  Section  (sehemu) ya  WXXX69, ukiwa umeandikwa Mei 23, 2011, ukielekezwa kwa waabudu shetani wa sirini na wale wa wazi wanaoishi na kufanya kazi zao katika mataifa hayo matatu, ambayo ni waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  Katika aya ya kwanza Waraka huo, unaanza kwa kuwapongeza watendakazi katika ulimwengu wa shetani ukisema:
   “Tunawapa pongezi kwa juhudi zenu juu ya kazi ngumu; tuliyonayo nyakati hizi za mwisho juu ya kuja kwake adui yetu kulichukua kundi lake. Tuna mbinu ambazo kufikia sasa zinaendelea kufaulu na bado zingine zina shida sana upande wetu kuzifanikisha, tungependa kuwaalika rasmi kwenye “kongamano kuu la Afrika Mashariki na kati” mwishoni mwa mwezi 30/07/2011.”
  Kisha unaendelea: “Jambo hili sio la kawaida kwetu,  japokuwa itakuwa mwisho wa mwaka. Lakini mambo yetu yanazidi kuharibika kwa upande wetu na baadhi yetu tukashindwa kutekeleza wajibu wenu, wengine kukosa nguvu kwa kukawia kutoa sadaka zao.”
  Katika maelekezo kuhusu usalama, waraka huo unaagiza: “ Kwa usalama wetu acha tukutane nje ya mji katika lango kuu la kuzimu “Mushitara-Dar es Salaam” saa 6:30 usiku hadi saa 9:00 bila kusahau chupa ya lita 5 za damu na mchanga wa kanisani. Kulingana na lengo letu mambo ambayo tutayazungumzia ni mbinu ambazo tungelifanya ili kuzuia maombi ya adui zetu na kuvunja amani ya jamii kupitia migogoro na migongano ya familia zao hasa kwa viongozi wakuu wa makanisa ya kiroho na kuliwahi kundi lao.”
  Miongoni mwa vipengele tata katika waraka huo uliosainiwa kwa mwandiko unaoashiria lugha ya kiarabu ni kile kinachosomeka: “ Kwa kulifanikisha jambo hili; na watakieni nguvu kupitia kwa alama yetu DWSUD na unasema mara sita; ukiwa umesimama na mara sita umechuchumaa; mara sita ukiwa umelala huku ukiwa uchi (666).”
  Pia waraka huo unatoa amri  kwa wanachama: “ AMRI: Sasa nendeni kwao ili kuharibu nguvu zao kwa kutumia sheria No. 999 WD ili kujificha (usionekane) unapozidi kuwasogelea na kuwafunga wanaume, wanawake na watoto wao. Kumbukeni yule Mwenyekiti wetu wa Afrika Mashariki na kati aliyechukuliwa na adui yetu tangu alipoanza maombi yake mmerudi nyuma sana! Huenda mambo yetu yakawa mabaya zaidi ndio maana tunawahitaji mkapokee nguvu.
  Maeneo hayo tumempa jukumu kupambana naye ni madam- No 1-14-14-18, ambaye kufikia sasa anaendelea kutafuta njia ya kumnasa na kumharibia mipango yake. Hata hivyo kuna mbinu mpya tunayotaka kuwaelezea watu wa eneo hilo. Jaribuni kufanya haraka sana ili kutoa kwa mara nyingine sadaka zenu ili kujiwekea ulinzi.”
  Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa waraka huu hugawanywa kwa watu maalumu tena bila maelezo ya sauti bali hutumia lugha ya ishara.
  Baadhi ya mambo yaliyomo kwenye waraka huo, wenye namba kadhaa za wale wanaelezwa kuwa ni mawakala wa dini za mashetani na waabudu shetani katika ukanda wa Afrika  Mashariki zinazosomeka hivi : “Madam-  No 1-14-14-18.”
  KWA NINI JIBU LA MAISHA LIANDIKE WARAKA HUU TENA NA KUUPA UZITO KATIKA UK. WA KWANZA?
  Baadhi ya mambo yaliyoanishwa katika waraka huu ni yale yanayoonekana makanisani, ambayo yamekuwa yakisababisha migogoro na vurugu kila kukicha. Mfano; miongoni mwa mbinu kuu zinazoelekezwa katika mambo hayo; ni  kwa mawakala hao wa ibilisi kujifanya wameokoka na kujichanganya na makanisa kwa lengo la kuanzisha vita vya ndani.
  Mawakala hawa wanaelekezwa kuhakikisha kuwa wanakuwa na wawakilishi katika kila kanisa lenye idadi kubwa ya waumini au linalokua kwa kasi, na kuhakikisha kuwa wanakuwa marafiki na hata kuhakikisha kuwa wanashiriki kila jambo waaminiwe na baadaye kuanzisha upinzani dhidi ya watumishi wa Mungu.
  Baadhi ya makanisa yanayolengwa  yametajwa katika mfumo ambao huwezi kuyatambua kama si sehemu ya mawakala. Miongoni mwa lugha zilizotumika kuelekeza makanisa ya kushambulia ni hii: “ Jina la kanisa alipo ni M-D-S, na DW-SU: 13-1-3-18-18-9-1.”
  Baadhi ya mikakati inayobainishwa katika waraka huo ni:
1.   Kuzusha magombano baina ya waombezi ili kuwavunja wasiendelee kumtafuta Mungu wao.
2.  Sababisheni hadithi kwa wingi wanapoingia ndani ya makanisa yao wakati wa kuja kumuomba Mungu  wao
3. Msiwaruhusu kuomba wakati wa kulala kwao (janatus) maana hamuwezi kuwaona wakifunikwa na nguvu za Mungu wao
4. Msiwape nafasi ya kusoma Biblia; badala yake wapeni wakati mwingi wa kusoma magazeti; kuangalia televisheni zao.
5.  Sababisheni ufukara; mateso na pesa zao kupotea bila wao kujua ili wasimtolee Mungu wao na walio na pesa roho ya ubahiii ya kutokutoa.
6. Ibada zao ziwe baridi kabisa ili roho wa mungu wao asipate nafasi ya kuongea na kusikia kutoka kwake.
Mwisho waraka huo, unamaliza kwa kuweka namba za msambaza maandishi ambaye anatajwa kama SENIOR URGENT:  KUTOKA MAKAO MAKUU: no. DW-SU: 13-1-3-18-18-9-1
  Ingawa ni vigumu kumpata mwandishi wa waraka huo ili kutoa ufafanuzi, lakini uchunguzi wa Jibu la Maisha, umebaini kuwa karibu mambo yote yanayoelezwa katika waraka huo ndiyo  yanayotokea makanisani na kuwa  kikwazo kikubwa cha kazi ya Mungu.
  Makanisa mengi yamekuwa na migogoro isiyo na sababu ambayo hupoteza muda mwingi katika kuikabili na hata wakati mwingine kuwatoa watakatifu rohoni ili wakajitetee katika hali ya mwili kisheria mahakamani.
 


Tuesday, June 14, 2011

Foleni za magari Dar Polisi wafunua nyuma ya pazia


Msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, unatajwa kama moja ya majanga sugu yanayokuza umasikini wa wakazi wa jiji hilo kubwa na kitovu cha biashara nchini. Wengi wamenyooshewa vidole wakitajwa kama chanzo kikuu cha janga hilo. UNGANA NA MWANDISHI Flora Matara katika kukuchambulia makala haya.



Safari yangu ilianzia Kimara, nakumbuka niliamka alifajiri na mapema ilipotimu saa 12:30 tayari nilikuwa ndani ya basi la abiri maarufu kwa jina la ‘dala dala’ nikielekea katika mihadi yangu na maafisa wa usalama barabarani. Siku hiyo usafiri haukuwa shida sana …. Ninamshukuru Mungu kwa hilo, lakini hata hivyo zahma ndani ya gari inanifanya nijiulize ni saa ngapi nitafika kwa wakuu hao ambao suala la muda kwao ni moja ya masomo wanayozingatia?
   Gari lenyewe lilikuwa katika mwendo wa kobe …… Mara imesimama……mara inatembea, kwa kweli ilikuwa ni shida tupu, kituo kimoja hadi kingine ilikuwa ni shughuli. Sikutaka kuiangalia saa yangu kwani ni kama ilikuwa ikikimbia….wakati mwingine nilitamani kumlazimisha dereva aongeze mwendo, lakini ilikuwa ni chini ya uwezo wake…. Sikuwa na jinsi niliendelea kuwa mpole huku nikitafakari mwisho wa haya yote.
   Nikiwa kwenye dimbwi la sintofahamu mara ninafika magomeni,…… nasikia kelele za watu naamua kuangalia dirishani kumbe ni wanafunzi wanaogombania kuingia katika gari; kondakta hataki kuwaruhusu, wamekaa muda mrefu  bila mafanikio, shuleni wamechelewa. Linaposogea mbele kidogo nashindwa kuyaamini macho yangu…..nagongana macho kwa macho na mnyororo wa magari.
   Uvumilivu unanishinda nikiangalia saa yangu inaniambia ni 2:00, miadi yetu na wakubwa zikiwa zimebaki dakika thelathini tu, naanza kutafakari nifanyeje niweze kuwahi maana hata nikichukua kebu (tax) bado ni yale yale…… nawaangalia abiria wenzangu sikuona mwenye sura ya kutabasamu, wengi wamevuta mdomo.
   Nakosa namna naona ni bora niangalie uwezekano wa kuchukua pikipiki (bodaboda), lakini hata hivyo nawaza! Ripoti maalumu wiki iliyopita inaeleza kwamba takriban majeruhi 10 hupelekwa kila siku Muhimbili kutokana na ajali za usafiri huu…. Ni kweli lakini nitafanyaje.
   Halmashauri yangu ya kichwa inafikia muafaka, naamua kuchukua pikipiki … sina ujanja ni lazima niwahi miadi. Hata kama nitapitia njia gani kwa usafiri wa daladala nitakuwa ni kama najisumbua tu! hiki ni kilio cha wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam, Baada ya kama dakika 10 nafikia mwisho wa safari yangu; namlipa dereva pesa yake na kumuacha aendelee na mambo yake.
   Naingia kwenye moja ya kituo kikubwa cha usalama barabarani, ni Kituo cha Kati jijini Dar es Salaam, wengi wamezoea kukiita Central. Nafika kituoni hapo nawakuta maaskari (trafiki) wengi lakini mmoja wao alinipeleka hadi kwa Mkuuu wa Kituo hicho, Inspekta Leopord Fungu, baada ya kusalimiana nae na kujitambulisha kwake, ananikaribisha   kiti tunaanza mazungumzo.
   Miongoni mwa maswali yangu kwake ni; kwa nini jiji la Dar es Salaam, limekuwa na msongamano mkubwa wa magari?  Na jeshi la Polisi linanyooshewa vidole kuwa ni sababu kubwa, hasa uongozaji magari kwenye makutano ya bara bara wakati kuna taa maalumu?
   Majibu ya Inspekta Fungu ni haya:  “Unajua wananchi wa Tanzania, na hasa wakazi wa Dar… hawana shukrani….jeshi la polisi kikosi cha Usalama Bara barani tunafanyakazi kubwa kwa uwezo wetu wote, lakini hawaoni wanatazama kasoro tu….basi, lakini ndio ubinadamu wenyewe.
    …Sisi tulikuwa watu wa kupongezwa kwa mazuri japo sawa tungekemewa kwa mabaya, lakini wakazi wa jiji hili wanajua kulaumu tu,”
   Akichambua sababu za msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, Mkuu huyo anaeleza kwa ubovu wa barabara nyingi zinazoingia na kutoka kati kati ya jiji ni miongoni mwa sababu.
   Kwa kuwa bara bara nyingi hazifanyiwi ukarabati wa mara kwa mara zina mashimo makubwa ambayo huwalazimu madreva kuendesha kwa mwendo wa tahadhari  na  hivyo kuongeza msongamano, lakini pia barabara zingine zimejengwa chini ya viwango.
   “Kwa mfano barabara ya Kilwa muundo wake ni kama chupa ya soda , upande mmoja ni pana wakati upande mwingine umebanwa, Tanroads walitakiwa wapanue barabara hiyo hadi maeneo ya Kamata,”alisema  Ispekta huyo.
   Alifafanua kuwa sababu nyingine kubwa inayosababisha msongamano huo wa magari ni ukweli kuwa karibu ofisi zote za Serikali na watu binafsi zipo kati kati ya jiji (City centre) hivyo magari yote ya watu binafsi na ya Serikali hueleke huko, hasa asubuhi na kutoka jioni.
   “Ofisi zote za Serikali zipo City Centre, lakini ofisi zingekuwa kama ilivyo ile ya Wizara ya Kilimo….. basi msongamano usingekuwa kama ulivyo sasa,” alisema na kuongezea:
   “Mbaya zaidi ofisi hizo pamoja na kuwa katikati ya mji bado hakuna maegesho ya magari….. katika hali kama hiyo magari yanawekwa ovyo na sasa hata dhana ya kuwa na njia moja (one way) imepotea.”
   Mkuu huyo anafafanua kuwa hakuna haja ya Tanroads kuwa na patrol kutokana na kwamba hakuna kazi inayofanywa, pamoja na wao kuwepo barabarani, bado mashimo yapo na hakuna jitihada zozote wanazozichukua.
   Kwa upande wa ajali za pikipiki afande Fungu,  anafafanua kuwa, Jeshi la polisi kikosi cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na kampuni ya Apec wameanza kutoa mafunzo maalumu kwa maderva na kwamba hadi sasa zaidi ya maderva wa pikipiki 1500 wameshapata mafunzo hayo yaliyoanza rasmi mwishoni mwa mwaka 2010.
   Pia alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na ufuatiliaji mkubwa kwa wale wote wanaopewa leseni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wana vyeti vya kufuzu mafunzo ya udereva kuangalia umri wao na kujaribiwa kabla ya kupewa leseni hizo.
   Mbali na hayo, Mkuu huyo anaeleza kwamba ikiwa Manispaa za jiji la Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wakala wa barabara (Tanroads) watatekeleze wajibu wao kama vile; kutengeneza barabara mara inapohitajika, basi ni wazi itasaidia kuondoa kama si kupunguza kabisa suala la foleni barabarani.
   “Mamlaka husika zinajisahau, mimi mwenyewe nimezifuata mara nyingi  kwa mafano; kwa barabara za Tazara, Msimbazi na Mnazi moja toka mwaka juzi tunaiomba lakini hakuna utekelezaji, pia kwa sasa ni wakati mzuri kwa serikali kutengeneza Fly over Bridges ili kupunguza msongamano huu,” alisema.
   Inspekta Fungu anaeleza pia kuwa, watu wengi wanalalamika kwamba kuwepo kwa watu wa usalama barabarani (traffic) kunaongeza foleni kuliko wanapotumia taa za bararani, katika kuwaongoza na hivyo kutaka askari hao wa usalama barabarani wasiongoze magari, hata hivyo anasema, madai hayo yalishawahi kutokea hata siku za nyuma na watu wakamfuata Tibaigana (aliyekuwa kamanda wa kanda maalumu ya Polisi Dar es Salaam) wakamwambia kuwa trafiki wasiongoze magari, lakini cha kushangaza baada ya siku mbili tu, wananchi hao hao waliomba tena trafiki waendelee na kazi yao.
   Mmoja wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, aliyezungumzia adha ya msongamano wa magari Dar ni Dk. Yunus Chambi, Mhadhari wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine, ambaye alisema:
   “Mimi ni mchumi na nimefanya utafiti na kuandika ripori kuhusu athari za uchumi kutokana na msongamano wa magari Dar…..nikubwa kuliko watu wanavyofikiria.
   Mfano; wakati naishi Botswana miaka mitano iliyopita nilikuwa nafundisha vyuo vinne kwa siku na niliweza kulipwa fedha nyingi, nilikuwa namaliza kipindi chuo kimoja na nasafiri kwa basi la kawaida tu naenda mji mwingine nawahi vipindi nafundisha nikimaliza naenda tena kwingine, lakini Dar es Salaam huwezi kufanya hivyo.
   Katika utafiti wangu niligundua kuwa kuna maelfu ya watu wenye taaluma ambao wangeweza kufanyakazi sehemu mbali mbali kama washauri, laikini kwa Tanzania ni ngumu. Ni kwa sababu hiyo serikali inalipa wataalamu washauri wa kigeni, kiasi cha Shilingi Milioni 40, kwa mwezi kwa kuwa hawezi kufanya kazi mbili. Nilazim ifafanye hivyo tu.
   “Siku moja nilimfuata mke wangu ambaye ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam, sehemu  ya Ualimu Chang’ombe, nakumbuka niliondoka pale saa 10, jioni  na foleni ilikuwa ya ajabu sana, nilifika nyumbani Mbezi Beach saa nne usiku na nilipoangalia gari nilikuwa nimetumia mafuta ya Shilingi  40,000. Hiki ni kiasi kikubwa sana  cha matumizi ya mafuta kwa safari moja tu,” alisema na kuongeza:
   “Kutokana na hali hii watumishi wengi wa umma wanabaki masikini kwa kuwa hata kama wanauwezo wa kujifanyia kazi nyingine ya kuingiza kipato baada ya kazi, hawawezi lazima akitoka kazini saa tisa afikirie vita ya kupanda dala dala  na kubanwa huku jasho jingi likimtiririka na  magari hayaendi.”
  
   SULUHISHO
   Mchumi huyu anasema kuwa  kupanua barabara pekee si suluhisho la tatizo, jiji kama  Dar linahitaji mipango yakinifu na utekelezaji wa kujitoa, unaolenga kuweka miundombinu ya kisasa kama vile gari moshi linalotoka Morogoro mpaka  kati kati ya jiji na lingine linalokatisha  jiji kutoka Bagamoyo hadi Kongowe Mbagala ambayo  yenyewe itawavutia watu kutoka  mjini na kuishi  nje.
   Anasema kuwa mfumo huo hauendani na mipango ya muda mrefu ya kuondoa ofisi muhimu kati kati ya jiji na kuweka mabasi makubwa yenye mazingira mazuri yatakayoshawishi watu kupunguza matumizi ya magari binafsi.
   Baadhi ya madareva wa mabasi waliolalamikia  msongamano wa magari wanasema kuwa  kuna nyakati ambazo wanalazimika  kuegesha magari wasubiri hali ibadilike kwa kuwa  bei ya mafuta ni kubwa sana kwa sasa hivyo ni hasara kuliacha gari kwenye foleni.
   Mmoja wa Madereva hao, Bw. John Shaaban,  mkazi wa Kimara alisema kuwa  anawaonea huruma wanafunzi ambao huvaa  unifomu  nyeupe  na kuingia kwenye vita ya kupanda gari asubuhi  kisha wanachafuka wakifika shuleni wanachapwa kwa uchafu.
   “Mara nyingi nimewahurumia wanafunzi wanyonge hasa mabinti unakuta inafika saa tatu hajaondoka kituoni wenzake wenye mabavu tayari wameshamaliza kipindi darasani. Wengine unakuta wanajiingiza kwenye vitendo vya ngono na madereva ili tu wapate lift ya kuwafikisha shule inasikitisha sana,”alisema.
   Akizungumzia  hali hiyo, Mwalimu mmoja wa Shule ya sekondari ya Makongo jijini Dar es Salaam, jina tunalihifadhi kwa sasa alisema kuwa  wakati mwingine anapoona wanafunzi waliochelewa wakiadhibiwa na askari(MP)  inauma kwa kuwa  unajua kuwa wengi si makusudi yao kuchelewa, lakini ni foleni.
   Kisha anaongeza: “Kwa kweli weanafunzi ni watu wa kipato cha chini  wanateseka sana. Wakati mwingine wanaacha kufikiria masomo anafikiria jinsi atakavyopambana kupata gari, kwenye mitihani ya mwisho wanafanya mtihani mmoja hii sio sawa.”
   Afisa Mipango wa jiji la Dar es Salaam,  hakupatikana kuzungumzia suala hili, lakini mmoja wa maofisa wa ofisi  yake aliliambia Jibu la Maisha  kuwa hata serikali inapasua kichwa kutafuata suluhisho la msongamano huo.
   “Kwa upande wa Serikali inajitahidi  sana ilipanua bara bara  ya Mlandizi, sasa inapanua barabara ya Tegeta kwa msaada wa Japan, lakini hata yenyewe haitakuwa suluhisho la kudumu. Kwani hakuna udhibiti wa uagizaji magari; unajua mimi nashangaa ninapoambiwa eti Tanzania watu ni masikini wakati kila siku wananunua magari ya kifahari na ndiyo yaliyojaa bara barani,”alisema na kuongeza:
   “Mimi  nakaa Ubungo  kwenye nyumba ya kupanga tu, lakini akina dada  wapangaji wenzangu  wanne wote kila mmoja ana gari  na analitumia kwenda kazini mjini…fikiria wote hawa wanafanya kazi za kawaida hotelini, lakini nwanamiliki magari na wanatoka nayo kila siku unadhani foleni itapungua? Watanzania nao wanapenda sana anasa. Mtu hana hata kibanda, lakini anamiliki gari mbili moja inambeba mkewe, na moja anatumia yeye ….tena wote wanaenda kazini eneo moja unadhani foleni itaisha.”
   Anasema kuwa majiji makubwa kama New York, Marekani ustaarabu uko kwanza kwenye vichwa vya watu, wanajali taifa lao, hawawezi kugeuza jiji lao kuwa jalala la magari mabovu au  ya wizi toka nje. Wao wenyewe ni wapambanaji wa foleni.
   Jiji la Dar es Salam, ni miongoni mwa majiji katika ukanda huu wa Afrika Mashariki yenye watu wengi wanaotoka kila kona ya Tanzania kitu ambacho kwa namna moja au nyingine ni sababisho la msongamano wa watu na magari.

Monday, June 13, 2011

Biblia yazua kizazaa kortini

 
MVUTANO mkali unaohusisha vifungu vya sheria na maandiko matakatifu ya Biblia umeibuka katika Mahakama ya Ardhi Tanga, baada ya  kiongozi mmoja wa dini nchini kukataa kuapa kwa Biblia akidai kuwa, kufanya hivyo ni kukiuka maagizo ya BWANA Yesu Kristo aliyoyatoa mlimani, yaliyoelezwa wazi katika kitabu cha Mathayo 5:33-37.
  Utata huo wa kisheria uliibuka hivi karibuni katika Mahakama ya Ardhi mkoani Tanga, baada ya Askofu  Dk. Erick Mwambigija, kukataa kuapa mbele ya Hakimu, Biteki Kishenyi, anayesikiliza shauri namba 111, la mwaka 2011, lililofunguliwa na kanisa la  Church of God of Prophesy, dhidi ya aliyekuwa mtumishi wake mkoani Tanga , Bw. Danford Makota,  ambaye anatuhumiwa kuuza  eneo la kanisa kwa Muarabu ili ajenge kituo cha mafuta.
  Mbele ya Hakimu Kishenyi,  Askofu Mwambigija ambaye ni Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya  Church of God Tanzania, alitakiwa kushika Biblia na kuapa, kabla ya kutoa ushahidi wake, lakini alikataa akimweleza hakimu kuwa hawezi kushika Biblia Takatifu kisha anyooshe mkono kuelekea mbinguni na kuapa kwa kuwa, kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Biblia katika kitabu cha Mathayo 5:33-37.
  Baada ya Askofu huyo kugoma kuapa akitaka utumike utaratibu mwingine wa kumuuliza maswali, badala ya kumuapisha kwa kuwa kufanya hivyo ni kumuasi Mungu anayemtumikia. Hakimu huyo aliwataka mashahidi wengine kuapa kisha kuendelea na ushahidi, lakini wote walifuata nyayo za kiongozi wao na kukataa kuapishwa.
  Hali hiyo ilizua mvutano wa kisheria baada ya hakimu kuonya kuwa kutokula kiapo kunaweza kuathiri kesi hiyo na ikafutiliwa mbali, lakini mwanasheria wa kanisa, Bw Wenceslaus Mramba, alipinga hoja hiyo kisheria akisema sheria inatambua pia utaratibu unaojulikana  kama “Assirnation” (kuthibitisha) badala ya kutumia neno kuapa na hailazimishi shahidi kuapishwa.
  Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Wakili Mramba, alisema kuwa kisheria  mtu halazimiki kuapa kwa kuwa hakuna sheria inayotoa sharti la kiapo kama njia pekee ya  kutumika kabla ya kutoa ushahidi mahakamani.
  Baada ya hakimu kubaini kuwa mvutano huo ni mkali, kwa kuwa unagusa hoja za kiimani,  aliamua kuahirisha kesi hadi Juni 21, mwaka huu ili apate nafasi ya kuperuzi vitabu vya kisheria kisha atatoa uamuzi ikiwa shauri hilo linaweza kuendelea na mashahidi wangetoa ushahidi wao  bila kuapa kwa Biblia.
 
  KESI YA MSINGI
  Mlalamikaji katika Shauri hilo ni Kanisa la Church of God, ambalo linadai kuwa Bw. Makota, ambaye alikuwa mtumishi wa kanisa hilo aliuza eneo la kanisa kwa Mwarabu ambaye alikusudia kujenga  kituo cha mafuta kisha kutoroka. Eneo lililouzwa limetajwa mahakamani hapo kuwa linathamani ya shilingi milioni 40.
  Mlalamikaji anadai kuwa  eneo hilo ni  mali ya kanisa, hivyo muuzaji hakuwa na haki wala mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, na anataka lirudishwe kwa mmiliki halali.
  Akiongea na Jibu la Maisha, baada ya kesi kuahirishwa Askofu Mwambigija alisema kuwa, msimamo wake uko wazi, ni kama ule wa akina Daniel mbele ya mfalme, kamwe hawezi kumuasi Mungu wake kwa sababu ya jambo lolote lile.
  “Sikia Bwana, hapa mambo yako wazi….Biblia ndiyo mwamuzi wetu wa mwisho; sisi tunaomfuata BWANA Yesu, tukiwa wanafunzi wake. Pale mlimani alituagiza akisema:
   “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo ila mtimizie BWANA  nyapo zake, lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;  wala kwa nchi, maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalem, kwa maana ndio mji wa Mfalame mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe wala mweusi. Bali maneno yenu yawe ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.” (Mathayo 5: 33-37)
  Kisha aliongeza: “Mimi naamini kuwa Mkristo halazimiki kuingia katika mgogoro na Mungu wake kwa ajili ya kuapa….sioni umuhimu wa wanadamu kuapishwa kwa Biblia kwa kuwa, kufanya hivyo ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na tunapomuasi Mungu tunaalika mabalaa katika taifa letu…”
  Akifafanua alisema kuwa, maelezo aliyonukuu kwenye kifungu cha Biblia aliyasema Bwana Yesu Kristo akiwa mlimani na ni agizo kwa yeyote anayeifuata  imani  ya Ukristo, hivyo hakuna  nafasi ya kupingana naye, ni ama kuufuata au kuukana Ukristo.
  “Kwa kweli kama nitapata nafasi ya kutoa maoni yangu katika mchakato huu wa katiba mpya nitasema wazi ya kwamba, hakuna haja ya kuwa na kifungu cha sheria kinachomtaka mkristo aape  mahakamani au mahala popote anapoteuliwa katika wadhifa fulani,” alisema  na kuongeza:
  “Ni afadhali kupata hasara yoyote ile katika maisha kuliko kuingia katika mgogoro na Bwana Yesu….alishasema tusiape, basi hilo ni la mwisho, mimi nilishapata hasara ya shilingi milioni moja kwa kukataa kuapa katika Mahakama kwa kuwa siwezi kuikiuka Biblia.”
  Akifafanua alisema kuwa, kipindi cha nyuma alikuwa na kesi katika Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, mbele ya hakimu Suma Sene (kwa sasa ni marehemu), ambaye alimlazimisha ashike Biblia aape, lakini alikataa na hakimu huyo akaifutilia mbali kesi hiyo na alikubali kupata hasara ya shilingi milioni moja ili kulinda Ukristo wake.
  Sambamba na hilo aliongeza kuwa, haoni faida ya wale walioapa kwa Biblia kwa kuwa wengi wao wameibuka kuwa mafisadi mashuhuri na wala rushwa wasiohofia kiapo hicho.
 
  MAONI YA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU
  Mmoja wa wanasheria mashuhuri nchini ambaye pia ni Mhadhiri wa Sheria, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benedict Mapunda, akitoa maoni yake kuhusiana na mkasa huo alisema:
  “Kuapa mahakamani ni amri ya  Kaisari, ambayo haipingani na Mungu … ila ukishaapa usiseme uongo, sema kweli tupu. Lakini pia si lazima kuapa mahakani kama imani yako hairuhusu. Kuna kitu kinaitwa “to affirm”(kuahidi kusema kweli bila kumtaja Mungu) na ushahidi wako unakubalika, ingawa mahakimu wamezoea kuapisha Wakristo wote.”
  Mwingine aliyechangia hoja hiyo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Theolojia cha kimataifa Global Harvest University” Samuel Mwaluvanda, ambaye alisema kuwa, kimsingi kuapa ni kinyume cha Neno la Mungu kwa kuwa Bwana Yesu alishakataza.
  Alisema kuwa, alishaonya hata wakati Waislamu wenye msimamo mkali walipoibuka kudai mahakama ya Kadhi kuwa, wakishikilia hilo Wakristo nao wataibuka na hoja ya kutaka kiapo kwa kutumia vitabu vya Mungu vifutwe.
  “Nijuavyo mimi kitheolojia, kuapa kwa Biblia iwe ni Mahakamani au pengine popote ni kukiuka Neno la Mungu aliye hai,” alisema mhadhiri huyo.