OTHER WEBSITE LISTS


Thursday, December 29, 2011

Mauti si ya Kafulila ni mabaki ya ‘zidumu fikra za Mwl

WIKI iliyopita Mbunge wa Kigoma Kusini, (NCCR Mageuzi) Bw. David Kafulila, aligeuzwa ndama wa kafara ili kuhitimisha mgogoro uliokikumba chama chake, alipovuliwa uanachama na kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, hiyo inamaanisha kuwa kijana huyu mwenye umri wa miaka 29 tu, amepoteza ubunge wake, labda utokee muujiza.

Ni bahati mbaya kuwa mwisho wa Kafulila umekuwa hivyo, na haukuwa kama rafiki yake wa siku nyingi Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), ambaye aliweza kuruka vihunzi akafanikiwa kubaki chamani, japo mpango ulisukwa kumtoa. Naam si hao tu, Mbuge wa Jimbo la Wawi kupitia (CUF) Hamad Rashid, naye amekalia kamba ya katani mlimani wakati wowote inaweza kukatika, tayari hoja ya kumfukuza uanachama imewasilishwa chamani na vikao vinaandaliwa. Kisa katofautiana na viongozi wenzake.

Matukio haya matatu, pamoja na yale yanayoendelea ndani ya CCM, yanaashiria jambo moja kubwa! Tatizo la kimfumo na mabaki ya dhana ya iliyotamalaki katika awamu ya kwanza ya utawala wa Tanzania iliyosema; ‘zidumu fikra za Mwalimu,’ ambayo haikutoa nafasi kwa watu ndani ya chama kutofautiana kwa hoja na bado kuendelea kubaki pamoja.

Tukio hilo ambalo kabla ya kufikia uamuzi wake, kulikuwa na misuguano mingi ndani ya chama cha NCCR Mageuzi, huku kukiwa na pande mbili za wanaomuunga mkono Kafulila na wale wa upande wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Bw. James Mbatia, ambapo kwa ujumla wake ilionekana kwamba, Kafulila alikuwa akikinzana na iongozi wa chama hicho kimtazamo.

Itakumbukwa kuwa, mfumo wa siasa za vyama vingi ulianza mwaka 1985, ukirithi ule wa chama kimoja, ni mchanga na wala haujawa na mizizi mizito ndani ya viongozi, vyama na wananchi kwa ujumla. Dhana ya ujamaa ambayo hasa ilijenga msingi wa ‘zidumu fikra za Mwalimu’ umesalia hata kwenye katiba, japo kinachofanyika ni uchumi wa soko.

Pia katika siasa za nchi, mfumo unabaki ule ule wa ‘Zidumu fikra za Mwalimu, yaani mtu mmoja afikiri na wengine watekeleze, hakuna kuhoji wala kujadili mawazo mengine, badala yake utaitwa muasi na kikao kitaitwa kukushushia rungu kichwani.

Ninachotaka kujadili hapa ni ukweli uliofichwa nyuma ya pazia kuwa wabunge, wanachama na hata viongozi wa ngazi za chini katika vyama vyetu vya kisiasa hawako huru kifikra wanapaswa kudumisha fikra za wenyeviti wao na wapambe wao.

Simaanishi kuwa, hawa wahusika mmoja mmoja ambao wamefikishwa kwenye mabaraza ya juu wakitishiwa kuvuliwa uanachama hawana hatia, laa hasha! lakini ninalotaka kuonesha hapa ni kuwa kuna jambo la zaidi ya makosa au uasi wao.

Ninalotaka lionekane hapa ni ukweli mwingine kuwa, ndani ya vichwa vya akina Mbatia, Mbowe, Profesa Lipumba na hata Jakaya Mrisho Kikwete, kuna mabaki ya dhana ya ‘zidumu fikra za Mwalimu’ ambayo yanawanyima nafasi ya kutambua kuwa, wanaweza kutofautiana katika falsafa, lakini wakandelea kufanyakazi pamoja.

Kilichotokea kwa Kafulila, kiliwahi kutokea Zambia, ambapo rais aliyekuwa madarakani alitofautiana na wenzake chamani, lakini kwa kuwa mfumo wao wa sheria ulikuwa umeshaondolewa kwenye dhana ya zidumu fikra ukamuokoa, akaanzisha chama chake haraka na akaendelea kutawala akiwa na chama kipya.

Mchungaji Christopher Mtikila, aliliona hili mapema, akaamua kufungua kesi mahakamani akipinga dhana ya kikatiba ya kuzuia mgombea binafsi, akashinda kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini jopo la majaji, lililoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Augustine Ramadhani, aliamua kuwa Mahakama haina mamlaka ya kikatiba ya kuiamuru serikali kuondoa kifungu cha katiba kinachozuia mgombea binafsi na wakati huo, kulikuwa na siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu kuitishwa.

Ni hukumu hii tata ambayo ilidai eti suala hilo ni la kisiasa, hivyo linastahili kujadiliwa katika majukwaa ya kisiasa iliyoendeleza dhana hii chafu hadi leo, ambayo kwa hakika ni mauti mazito katika siasa za Tanzania.

Ninaamini moyoni mwangu kuwa, ni mauti hii ya demokrasia inayokuza ufisadi kuanzia ndani ya vyama hadi serikalini kwa kuwa watu wamewekwa kufuli mzito midomoni wakithubutu kupinga jambo lolote, wanaitwa waasisi wanafukuzwa na wale wenye mamalaka wanalindwa na mfumo uliopo .

Lakini kama Jaji Ramadhani, katika hukumu yake angezingatia ukweli mwingine kuwa Mahakama ndicho chombo chenye mamalaka ya kisheria, kutafsiri sheria na kutoa haki iliyominywa, angeruhusu mgombea binafsi kwa kuwa hiyo ndiyo hukumu ya haki.

Kwamba kuna mgogoro wa kikatiba na kifungu cha kisheria kimewekwa kwa madhumuni ya kuminya haki za wengine, na kinakiuka haki za kibinadamu na shauri lipo mbele ya Mahakama, ni chombo hicho chenye haki ya kutafsiri na kutoa hukumu na wala si kingine.

Kwa maoni yangu, Jaji Augustine Ramadhani, hawezi kusahaulika kutokana na hukumu hii na nadhani iko siku ataungana nami kujutia maamuzi yake, ambayo leo yanamsindikiza Kafulila mitaani na kuliacha jengo la bunge Dodoma, kubaki katika historia tu huku ikikiacha chama cha NCCR Mageuzi, kubakia na wabunge watatu tu.

Sio Kafulila ambaye amekutana na maswahiba ya namna hiyo, madiwani watano wa CHADEMA, wakitokea Arusha nao walishindwa kufurukuta baada ya maamuzi ya chama hicho, kuwavua uanachama na kuwafanya wapoteze ridhaa ya wananchi ya kuwachagua kuwa, madiwani wao kwenye maeneo yao mkoani humo.

Watu wengine ndani ya NCCR- Mageuzi, ambao waliambatana na Kafulila ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa chama hicho, kwa nafasi ya urais 2010, Hashimu Rungwe, ukiachilia mbali wengine 16 waliopewa onyo kali.

Tanzania kwa ujumla tunapaswa kutambua kwamba, kiongozi si mtu anayejua yote, kuna wakati anaweza kukosea na tujifunze kukubali makosa, pale tunapokuwa tumekosea na si kung’ang’ania eti kwa kuwa ni kiongozi.

Ufisadi mkubwa ambao leo tunaweza kuuona kwenye maeneo mbalimbali ni kutokana na watu kuogopa kusema ukweli, mtu anaogopa kwa kile anachohisi kwamba watu wengine watamuona muasi, tena mwenye kimbelembele. Ni wakati ambao tunatakiwa kubadilika kutoka kwenye fikra za; nitaonekanaje na tujijenge kwenye ukweli na uwazi pale penye ukweli.

Vyama vingi vya siasa Tanzania tumejaribu demokrasi, tunaona tutaweza na hata kusonga mbele, ikiwa tu tutaachana na siasa za woga na kusimamia haki hatakama itatugharimu kwa muda. Ni wazi kuwa huu ni wakati wa kujenga upya siasa zetu tukiwa tayari kulipa gharama ya demokrasia kama ile watangulizi wetu waliyolipa. Ninapowaaga nawashauri watanzania wote kujitambua kuwa wao ndio wajenzi wa siasa safi na utamaduni wa ukweli na uwazi, wanapaswa kusema ndio wakamaanisha ndio na hapana wakamaanisha hapana, wasimpigie makofi fisadi wakimtazama usoni, lakini akiwapa kisogo wanamsonda vidole.

Niweke kalamu yangu chini nikisisitiza kuwa maadui wa Tanzania ya leo ni Watanzania wenzao, ambao wamebobea kwenye unafiki na uzandiki wa kutisha ambao wakiibiwa wanacheka, wakidhulumiwa wanacheka na wakidanganywa wanashangilia usoni japo mioyoni wanalia!

No comments:

Post a Comment