OTHER WEBSITE LISTS


Saturday, September 10, 2011

SUALA ZIMA LA KIFO

SUALA LA KIFO

Nimekuwa nikifuatilia kwa makini kuhusu sUala la kufa, na haya ndiyo nikajifunza katika kufuatilia kwangu. La kwanza kabisa ni jinsi sUala hili lisivyotakiwa kuzungumzwa kufuatana na utamaduni na maadili ya kikwetu wa-Tanzania kama siyo Afrika. Kwenye nchi mojawapo jirani, mtu mmoja ambaye aliwahi hata kuwa waziri katika serikali ya nchi hiyo na ni mtu mwenye uwezo, alijiamulia kwamba badala ya kungoja akifa huku nyuma watu waamue wanamzikaje, yeye aliamua kutengeneza kwa kuchimba kaburi lake vizuri na kuta za ndani akazipamba kwa vioo. Kisha akajitengenezea jeneza zuri la kioo na ndani yake akaweka sanda nzuri, suti, viatu, shati na tai, vyote vya gharama kubwa toka nje ya nchi, kisha kuliweka hilo jeneza ndani ya hilo kaburi na kuegesha mfuniko mzuri wa nakshi juu ya hilo kaburi lakini likiwa ndani ya nyumba ndogo na nyumba hiyo iko ndani ya ua wake. Jambo lililotokea, wana kijiji walipata habari ya tukio hilo. Kwa bahati mbaya sana kukatokea wazungu wanasema “coincidence.” Mvua nayo ikakataa kunyesha sehemu hiyo wakati wa vipindi vyake kwa miaka kadhaa kuanzia kaburi hilo lilipochimbwa. Wanakijiji wakaunganisha kutokunyesha kwa mvua na hilo kaburi. Walichokifanya, walimwendea mheshimiwa huyo ambaye kwa miaka mingi kabla kustaafu toka kwenye siasa, alikuwa mbunge wao akipita pasipo kupingwa katika kila uchaguzi hadi hapo alipostaafu (sasa mheshimiwa huyo umri umekwenda ingawa anaonekana bado kwenye shughuli mbalimbali). Wanakijiji walimlazimisha kuvunja jeneza lake na kaharibu kabisa kaburi. Hivi navyoandika, hakuna kaburi wala jeneza lililotayarishwa (Fedha nyingi zimepotea hapo). Kijiji kilitikisika kwa jamko alilolifanya mheshimiwa huyo. Kubwa hapa ni jinsi utamaduni wa Kiafrika usivyoruhusu jambo kama hilo kufanyika/kutokea wala kuzungumzwa.

Kufa ni Lazima: Mwanzo 3:19

Msomaji, hakuna ushindi mkubwa unaozidi kujitayarisha kukabiliana na kifo. Moja ya mambo makubwa mwanadamu anaweza kuonekana alifanya maamuzi magumu na yenye tija, ni kule kujitayarisha ki-usahihi kukabiliana na kifo. Hakuna majuto makubwa kwa mwanadamu yanayoweza kuzidi majuto ya mtu kujikuta hajajitayarisha kukabiliana na kifo.

Nampenda sana Mungu. Yeye hakutuficha katika hili. Aliliweka wazi kabisa kwetu ili kwa mwenye ufahamu aweze kukabiliana nacho. Tutazungumzia vizuri hapo mbele kuhusu kukabiliana na kifo. Lakini Mungu mwenyewe Muumba wa mbingu na nchi na vyote vilivyomo, aliona umuhimu wa mwanadamu kuelewa kuhusu kufa. Alijua umuhimu wa jambo lenyewe na jinsi mwanadamu anavyotakiwa kujiandaa kukabiliana nacho, yaani asije akakutwa na majuto yasiyo na majibu wala masahihisho.

Biblia Neno la Mungu Linaweka Wazi Kusema

Mungu akimtahadharisha Adamu alimwonya kwamba akikiuka agizo lake na kula matunda ya mti aliomkataza, atakufa (Mwanzo 2:17). Adamu na mkewe (Hawa) wakalifanyia mzaha Neno la Mungu, lakini waliona malipo yake kwa macho yao wenyewe wakati mtoto wao Habili alipokufa. Kwa kuwa hawakuwa wamewahi kuona mtu aliyekufa, lazima iliwachukua muda kuelewa nini kimetokea kwa mtoto wao kwamba hafumbui macho, ahemi wala kutikisika. Ndipo wakakumbuka Mungu alizungumzia neno “Kufa.” Nadhani ndiyo hii!! Wakajikuta wanapasuka kwa kilio kikubwa kisicho kifani wala msaada wowote kwa kuondokewa na mtoto wao mpendwa. Nadhani Mungu aliruhusu jambo hili lisiwaanze wao ili wawe mashuhuda ya matokeo ya madhara waliyoyaleta. Kwa lugha ya mtaani, “Waote joto ya jiwe,” kwa kudharau kwao maonyo na Neno la Mungu. Katika dunia tunayoishi, mwanadamu amejitahidi sana kupambana na kifo, hatukatai wataalamu, wanafanya sehemu yao. Wanatoa vyandarua vya mbu bure ili tusiumwe na mbu wa malaria na tukafa. Wana usemi kwamba wanapunguza idadi ya vifo kutoka asilimia Fulani hadi asilimia Fulani. Wamevumbua madawa na mitambo ya ajabu ya nguvu ya kumpima na kumtibu mwanadamu, hiyo yote ni katika jitihada za kupambana na kifo. Wameweka mpaka vitochi barabarani kuchunguza kasi za magari, hiyo yote ni katika kupambana na kifo. Swala kubwa hapa linalozungumziwa si kupinga jitihada zinazofanywa na wataalamu pamoja na viongozi wetu katika kupambana na kufa. Linalozungumzwa hapa ni kwamba unakubaliana nami kwamba lazima utakufa? Hapa ndipo nataka tusaidiane/umejiweka tayari kukabiliana na kifo? Nalipenda Neno la Mungu lilivyo wazi likimshughulikia mwanadamu kwa kumwambia, “Walio hai wanajua watakufa bali wafu hawajui lolote. Hawana zawadi ingine, hata kumbukumbu juu yao imesahaulika . . . wala hawatakuwa na sehemu yoyote ile kwa yanayoendelea chini ya jua (Mhubiri 9:5). Kifo hakichagui tajiri wala maskini, mtu mashuhuri wala asiye na umashuhuri wowote, mwenye cheo na asiye na wadhfa wowote. Kifo hakina heshima kwa mtu. Ndiyo maana mtu fulani maarufu mwanamume aliyejaa kiburi na kumnyanyasa sana binti mfanyakazi wa nyumbani kwake, wakati wa kukaribia kufa kwake, huku walinzi wakiwa nje na bunduki zao na mke wake akiwa kazini na watoto wake (watu wazima) wakiwa makwao, hali akiwa chooni bila nguo chumbani mwake (master bedroom ya gharama), huku amezidiwa, mauti yanapiga hodi kwa nguvu kumdhulumu roho yake, alilazimika kumwita huyo huyo binti akamwokota humo chooni, akamburuza hadi chini ya kitanda akiwa uchi vilevile bila nguo yoyote ile, na maneno ya mwisho, huku akihema kwa shida alimsimulia binti huyo huyo mbaya wake. Leo Jukwaa linauliza, umejitayarisha kukabiliana na kifo. Mtu anakabiliana na kifo namna gani? Tumwombe Mungu atupe uzima tukutane Jumapili ijayo. Hii ni muhimu sana. Mwambie na rafiki yako na watu wa nyumbani mwako wasome.

No comments:

Post a Comment