OTHER WEBSITE LISTS


Saturday, September 10, 2011

JIFUNZE SHERIA


v Jua haki na wajibu wako kwa mujibu wa sheria

v Jua namna ya kutumia sheria ili upate kufanikiwa.

v Jua ni wapi, lini, kivipi, kwa nani na kwa nini upate haki zako.

v Tambua madhara na hasara za kutojua na kutoitumia sheria ipasavyo.

“NAWE UTAIFAHAMU SHERIA NA SHERIA ITAKULINDA !!!”

SHERIA ZA ARDHI

Karibu katika JUKWAA LA SHERIA. Jukwaa hili litakupa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo sheria angalau kwa kiasi fulani, ambayo yatakuwezesha kupata mwangaza mkubwa wa maswala ya sheria. Utafahamu juu ya katiba, haki za binadamu, sheria za jinai, sheria za madai, biashara, mirathi, ndoa, mikataba, usajili na uendeshaji wa makanisa na taasisi nyinginezo na mangine mengi. Katika sehemu hii utajifunza juu ya Sheria za Ardhi. Umekutana na matatizo mengi katika masuala ya ardhi, Jukwaa hili laweza kuwa suluhisho la matatizo yako. Pata maarifa yatakayokusaidia wewe na jamii inayokuzunguka. Karibu !

Katika makala iliyopita tulijifunza juu ya sheria zinazoshughulikia maswala ya ardhi, maana ya ardhi na kanuni za sera ya ardhi na changamoto za ardhi. Naamini zimefanyika msaada mkubwa kwako. Katika makala hii tutaangalia tahadhari unazopaswa kuchukua kabla hujauza, kununua, kutoa au kupokea ardhi pamoja na haki na wajibu ulionao kwa mujibu wa sheria za ardhi. Karibu !

D: Chukua Tahadhari

Upo msemo wa Kiswahili ambao nadhani unaweza kuwa busara kama utautumia ili kukupa muongozo katika kushughulika na maswala ya ardhi. Msemo huu unasema “kinga ni bora kuliko tiba” pia upo mwingine usemao; “chukua tahadhari kabla ya hatari”. Maana halisi ya misemo hii ni kwamba ni bora uchukue hatua za awali za tahadhari kabla ya hatari kutokea. Hatua hizo za tahadhari zitakusaidia sana katika kuondokana au kuepukana na migogoro ya ardhi ambayo umekuwa ukikutana nayo au ambayo unaweza ukakutana nayo. Tahadhari hizo ni kama zifuatazo:-

  • Usinunue shamba, kiwanja au nyumba mpaka ujiridhishe juu ya mamlaka ya muuzaji kama kweli ana mamlaka ya kukuuzia kiwanja hicho.
  • Kama shamba, kiwanja au nyumba hiyo inahusisha mirathi ni muhimu sana anayeuza akawa ndiye msimamizi wa mirathi kwa mujibu wa barua ya usimamizi wa mirathi kutoka mahakamani.
  • Usinunue shamba, kiwanja au nyumba pasipo mkataba halali uliosainiwa kisheria na pande zote mbili na kushuhudiwa na kiongozi wa serikali ya mtaa, kata, hakimu au mwanasheria. (Napendekeza zaidi kwa mwanasheria kuliko sehemu nyingine).
  • Usinunue shamba, kiwanja au nyumba iliyopimwa pasipo kwenda kufanya uchunguzi katika ofisi za ardhi juu ya taarifa sahihi zinazohusu kiwanja hicho.
  • Usinunue au usiuze shamba, kiwanja au nyumba ya familia kwa makubaliano na mume/mke tu bila kupata ridhaa ya mke/mume wake.
  • Usiuziwe kiwanja, shamba au nyumba ambayo hujafika mahali ilipo au hujui mahali ilipo. Hakikisha unauziwa kitu ambacho unakifahamu.
  • Usikubali kupokea kama zawadi shamba, kiwanja au nyumba yoyote kwa maneno tu, pasipo maandishi ya aina yoyote na mashahidi katika makabidhiano hayo. (Napendekeza makabidhiano hayo yafanyike kwa mwanasheria).
  • Usikubali na wala usithubutu kutoa fedha kwa mauziano yoyote ya ardhi pasipo kwanza kukabidhiwa nyaraka za umiliki na mhusika. Pia usikubali kutoa nyaraka zako za umiliki wa ardhi yako pasipo kwanza kupokea malipo halali uliyokubaliana na huyo unayemuuzia eneo hilo.
  • Usinunue shamba, kiwanja au nyumba wala kujenga au kununua nyumba kimya kimya, bila kumshirikisha mume au mke (kwa wanandoa), watoto, ndugu au mtu mwingine yeyote anayehusika katika familia yako. Ukinunua ardhi kisirisiri, utaipoteza kisirisiri.
  • Hakikisha unapata ushauri wa kisheria kutoka kwa mwanasheria juu ya hatua za awali unazopaswa kuchukua kabla ya kununua, kuuza au kufanya matumizi yoyote ya ardhi. Pata pia ushauri kutoka kwa wataalamu wa maswala ya ardhi na mipango miji, viongozi wa serikali ya mtaa, kijiji, kata au wilaya wa eneo hilo ambalo unataka kulinunua kabla hujanunua eneo hilo.

E: Haki na Wajibu Wako Kwa Mujibu wa Sheria za Ardhi

Kumbuka kwamba sheria za ardhi zinaeleza juu ya haki ulizo nazo. Ni wajibu wako kuzifahamu haki hizi ili uweze kujua namna ya jinsi ya kuzipata. Haki na wajibu wako kwa mujibu wa sheria zinaanzia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho ambayo inakupa haki yako ya kimsingi ya kumiliki mali ambazo ni pamoja na ardhi (ibara ya 24). Haki na wajibu kwa mujibu wa sheria za ardhi zinaweza kuelezwa kama ifuatavyo:-

HAKI

  • Kupatiwa umiliki wa ardhi bila kujali wewe ni mwanamke au mwanaume.
  • Mwanamke kupata, kutumia, kuuza au kutoa ardhi kama ilivyo kwa mwanamume (kifungu cha 3(2).
  • Kupatiwa hati ya umiliki wa ardhi yenye jina, sahihi na picha yako mara baada ya kumilikishwa ardhi.
  • Kuuza, kununua, kutoa au kubadilisha umiliki baada ya kujiridhisha juu ya umiliki halali wa yule anaye kuuzia.
  • Kufungua kesi ya madai ya ardhi yako katika vyombo vya sheria endapo utaona haki yako ya umiliki wa ardhi hiyo inaingiliwa.
  • Kukata rufaa kutoka katika chombo kimoja cha sheria hadi kingine endapo utakuwa hujaridhika na maamuzi yaliyotolewa na chombo husika.
  • Kuweka rehani au dhamana ardhi yako kwa ajili ya kujipatia kipato au shughuli za kibiashara.
  • Kutoingiliwa katika eneo lako unalolimiliki kisheria.
  • Kulipwa fidia stahiki inayoendana na thamani ya ardhi pamoja na mazao au jengo lililopo katika ardhi hiyo endapo eneo lako litachukuliwa na serikali kwa ajili wa matumizi ya umma au shughuli nyingine yoyote ya kiserikali.
  • Kumiliki ardhi kwa pamoja au kibinafsi kati ya mke na mume.
  • Kupata nakala za mikataba au hati yoyote ya umiliki wa yule anayekuuzia, anayekupa au anayekukabidhi ardhi hiyo mara baada ya makabidhiano au mauzo ya eneo hilo.

3 comments:

  1. Mwanzoni mwa mwaka huu, naibu waziri Angelina Mabula alipiga marufuku tozo za Tzs elfu 30 zilizokuwa zinatozwa na mabaraza ya kata kwa akili ya kupeleka files za kesi mahakama za wilaya. Alibainisha kuwa tozo hizo hazipo kisheria. Naomba kujua, jee Ni tozo zipi zipo kisheria ambazo mabaraza ya kata yanaruhusiwa kutoza? Jee malipo ya tozo za mabaraza ya Ardhi ya kata yanalipwa pasipo ulazima wa kata kutoa receipt kwamba wamelipwa pesa kwa tozo Fulani? Jee tozo ya Tzs elfu 30 kwa mlalamikaji na kiasi hicho hicho cha tozo kwa mlalamikiwa kwa ajili ya baraza kuhamisha kesi kwenda eneo la mgogoro Ni halali kisheria? Au linaruhusiwa hata pasipo sheria? Au Ni utaratibu unaoruhusiwa kufanyika kimazoea na pasipo ulazima wowote WA kutoa receipt yeyote kwa mlipaji wa tozo hizo?

    ReplyDelete
  2. Je naweza kupata nakala ya hii sheria ya ardhi nyumba na makazi

    ReplyDelete