OTHER WEBSITE LISTS


Monday, October 31, 2011

Paka weusi sasa wasakwa


·



Hupelekwa mpakani mwa Kenya na Sudan

· Wengine wahaha kufika Muhimbili kuwasaka nyakati za usiku

BAADA ya Tanzania kutikisa dunia kwa biashara chafu ya viungo vya binadamu hasa wale wenye ulemavu wa ngozi (albino), sasa imeibuka biashara ya paka weusi mkoani Mara wilayani Tarime, ambao husafirishwa hadi mpakani mwa Sudan na Kenya, Jibu la Maisha limeshuhudia.

Mwandishi wa habari hizi aliyekuwa safarini kutoka Nairobi nchini Kenya alishuhudia vijana wa Tarime mkoani Mara wakiwa na mifuko yenye paka hai ambao muda wote walikuwa wakilia kwa sauti kali, wakichanja mbuga huku wengine wakitangaza kwa sauti kuwa mwenye paka mweusi ampeleke atanunuliwa kwa shilingi 50,000 tasilimu.

“Soko la paka hawa lipo wazi kuna vituo kadhaa hapa Tarime na maeneo mengine ambayo wanunuzi wana pesa mkononi na ukifikisha tu paka mweusi unakula 50,000 bila maswali…” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Mkono ambaye tayari alikuwa na paka wawili waliokuwa ndani ya mfuko wa sanflati.

Jibu la Maisha liliambiwa kuwa paka hao wakishanunuliwa husafirishwa hadi mpakani mwa Sudani na Tanzania na pia mpakani mwa Kenya na Tanzania ambapo kuna wanunuzi wa uhakika wa wanyama hao.

Jibu la maisha lilipofuatilia kwa kina biashara hiyo liliambiwa kuwa katika eneo la Tarime mjini mnunuzi mkubwa ni Mzee Nyongige, ambaye ametoa matangazo kadhaa kwa vijana kuwa mwenye paka mweusi ampeleke, lakini ugumu wa biashara hiyo ni kuwa lazima paka awe mweusi kabisa asiye na doa lolote.

“Unajua sio siri hakuna mtu ambaye hapendi pesa, upatikanaji wa paka si mgumu lakini... kwa kuwa, kwa kipindi hiki wanatafutwa kwa udi na uvumba watakuwa ni adimu, mimi nitahakikisha kwamba ninapata paka na ninawapeleka kwa babu,” alisema Dereva tax mmoja aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Kisha aliongeza: “Kweli kila mtu ni lazima ataichangamkia biashara hii, kwa kuwa kuna paka wengi ambao wamekuwa wakizunguka huku na kule hawana mahala pa kuishi ….hao watasakwa na kuuzwa, tena jijini Dar es Salaam, kwenye hospitali ya Muhimbili kuna paka wengi sana nadhani ninaweza kufikiria kwenda huko.”

Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaonesha kuwa paka hao wanatumika kwa shughuli za kishirikina na kwa kipindi cha mwezi sasa paka wamekuwa wakisakwa kwa udi na uvumba mkoani Mara.

Juhudi za kumpata msemaji wa idara ya wanyama ya mkoa wa Mara hazikufanikiwa, lakini Kamanda wa Polisi wa Tarime Deudedatus Kato, alipoulizwa na Jibu la Maisha kuhusu harakati hizo alisema kuwa, anafuatilia kwa undani habari hizo ili kuona kama zinakiuka sheria za usafirishaji wanyama nchini.

Baadhi ya wazee wa kanda ya ziwa walidai kuwa kuibuka kwa biashara ya paka weusi ambao hutumika katika masuala ya kishirikina kumepunguza kidogo mawindo dhidi ya walemavu wa ngozi yaliyokuwa yakifanywa na watu wenye uchu wa madaraka.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitangaza dau kubwa la fedha kwa mtu atakayetoa taarifa zenye kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaofanya unyama dhidi ya Albino na walemavu wengine kwa lengo la kujipatia fedha bila jasho.

No comments:

Post a Comment