OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, October 9, 2011

Waraka wa Mchungaji anayesubiri kunyongwa!


· Ameandika kutoka katika Gereza la Lakan anakoshikiliwa

· Asema: “Nitaungana na Bwana Yesu mbinguni hivi punde”

· Aomba: “Baba mapenzi yako yatimizwe, si kama nitakavyo mimi”

Jaji wa Mahakama Kuu aliniuliza: “Uko tayari kumkana Yesu na kurejea kwenye uislamu wako uepuke adhabu ya kunyongwa mpaka ufe?” Nikamuuliza nimkane Yesu! Hapana siko tayari…bora ninyongwe….”

Wakati ulimwengu ukifanya bidii kumnusuru Mchungaji Yusef Nadarkhani, mwenye umri wa miaka 34, anayeshikiliwa na serikali ya kiislamu ya Iran katika gereza la Lakan, lililoko kwenye mji wa Rasht. Baada ya kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, kwa kosa la kukataa kumkana Bwana Yesu hadharani, na kuwashawishi watu kuukana uislamu na kujiunga na ukristo, mchungaji huyo ameandika waraka mkali kwa Wakristo ulimwenguni kote ukidhihirisha uimara wa imani yake. Waraka huo uliotafsiriwa kutoka katika lugha ya Farsi inayotumiwa na Wairan wengi unasomeka:

“Dear brothers and sisters, Salam

KATIKA jina la BWANA wetu Yesu Kristo, naendelea kuwatakia neema na rehema mnaponikumbuka na wale wote wanaofanya juhudi za kunisaidia kwa njia ya maombi. Unyenyekevu wenu mbele za Mungu unanipa nguvu na tumaini ninapokinywea kikombe hiki cha mateso makali.

Kwa kuwa naamini kuwa mtapata thawabu mbele za Mungu, kama alivyoahidi katika Neno lake ambalo linasema wazi kuwa baraka zake ni kwa yule mwenye imani thabiti, kwa kile ambacho Mungu aliahidi. Tunaamini kuwa mbingu na nchi zitapita lakini Neno lake litasalia hata milele.

Wapenzi, napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha maandiko machache ya Neno la Mungu, japo nafahamu mnayajua vyema, kwamba kwa kila jambo mnajitahidi sasa kuliko wakati mwingine huko nyuma, kwa kuthibitisha wito wenu katika utumishi huu na pia kujitoa muhanga kwa ajili ya Injili ili ihubiriwe kwa kila kiumbe ulimwenguni.

Nafahamu ya kwamba si wote waliopata neema ya kulitunza Neno la Mungu, lakini kwa wale waliopata neema ya kufunuliwa juu ya uungu wa Bwana Yesu, nawatangazia kama ilivyoandikwa katika Biblia kwenye kitabu cha Yuda: “….Mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.”

Tunapita katika siku maalumu na nyeti sana. Ni siku ambazo kwa muumini anapaswa kuzisoma alama za nyakati, aamke na kuikuza imani yake kwa kuwa pengine hatapata wakati mwingine tena ambao imani yake itakuwa kwenye majaribu makali yanayohitaji kupimwa ili kuona kama inalingana na ahadi za Mungu.

Kwa muumini wa kweli hana haja ya kushangaa anapoteswa na hata kuchomwa moto kwa ajili ya Jina la Yesu kwa kuwa tunapitishwa katika hali isiyo ya kawaida. Muwe tayari kukinywea kikombe alich kinywea Bwana Wetu Yesu Kristo kwa kuwa tunahakika ya kuungana naye katika furaha na utukufu wake.

Wapenzi hukumu ni lazima ianzie katika nyumba ya Bwana na kama ndio imekwisha anza kwetu, mwisho utakuwaje kwao walioikataa Injili ya Bwana Yesu? itakuwaje kwao. Je, kama wenye haki wanatendewa hivi itakuwaje kwao waliomkataa Mungu na kuchagua maisha ya dhambi?

Kwao wanaotendewa mabaya leo kwa kuyatenda mapenzi ya Mungu muumba wao wanapaswa kufahamu kuwa wameahidiwa urithi mwema na wa pekee. Kama Neno lilivyosema: “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao.”

Wapenzi, msitikiswe imani yenu na mateso, simameni imara kwa kuwa maumivu haya ndiyo waliyopitia mitume wa mwanzo wa imani yetu. Waliteswa na kuuawa kwa ajili ya haki. Lakini ni jinsi gani muumini atalielewa Neno hili.

Si, tu kwamba tunayatazama maisha ya Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani, bali tunayachukua hayo na kuwa maisha yetu hapa juu ya uso wa nchi. Kama alivyosema: Waitwao ni wengi lakini wateule ni wachache:

“Je Haikuandikwa kuwa njia iendayo uzimani ni nyembamba na iliyosongwa, na wapitao humo ni wachache. Bali njia ni pana iendayo upotevuni na wengi wanaokimbia majaribu hupitia humo. Kwa kuwa hakuna atakayeshinda kwa kukimbia majaribu, lakini kwa subira na uvumilivu atawezeshwa kuyashinda majaribu yote na kupata ushindi.

Kwa hiyo sisi tulio wafuasi wa Kristo, haitupasi kujisikia kuwa wapweke, bali yatupasa kudumu katika maombi ili Mungu atupe msaada na uhitaji wetu tunapokuwa kwenye dhiki.

Kwa mujibu wa Mtume Paulo; kila jaribu Mungu mwenyewe hutengeneza njia ya uvumilivu na jinsi ya kutoka. Ndugu wapendwa, magumu tunayopitia yasitunyong’onyeze, kwa kuwa yanafunua uhalisia wa utu wetu..

Ni vizuri kwetu yanapotukabili mateso na kudhalilishwa, hali hiyo isituvunje moyo bali itupe kujichunguza hali zetu, tuyaone ya kawaida na kutuimarisha kiroho.

Wapenzi, kaka zangu na dada zangu, ni lazima tuwe makini wakati huu kuliko mwingine wowote uliowahi kuwako, kwa kuwa hizi ni siku ambazo mioyo na mawazo yao itafunuliwa wazi, kwa maana imani zenu zinajaribiwa, na pale ambapo hazina yako ilipo ndipo na moyo wako utakapokuwa. Weka hazina yako mahali ambapo kutu na panya hawataingia.

Ningependa kuwakumbusha aya chache za Biblia ambazo kwa hakika tunazijadili karibu kila siku: “Baba yetu uliye mbinguni jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama yanavyotimizwa mbinguni.” Ndugu, tukitanguliza mapenzi yetu kwanza, mapenzi ya Mungu hayatatimizwa.

Kama tulivyojifunza kutoka Gethsemane, alisalimisha mapenzi yake kwa baba yake, ili mapenzi ya baba yake yatimizwe. “ Baba yangu, ikiwa ni mapenzi yako kikombe hiki kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi yako yatimizwe.”

Kinachotupata leo ni kigumu sana, lakini siyo yale tusiyoweza kwa kuwa hatukujaribiwa kupita uwezo wetu wa kustahimili, kwa kuwa ilishaahidiwa kwamba hayakutupata majaribu tusiyoyaweza. Na hali tunayopitia haitupasi kushindwa bali ituimarishe katika neema na kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Zingatia kuwa vifungo na vikwazo ni fursa ya kushuhudia ukuu wa jina la Yesu. Yeye alisema: “Kama mtu atanionea aibu mimi na Neno langu, nami nitamuonea aibu mbele za malaika na Mungu Baba katika utukufu wake.”

Mimi niliyemtumwa wa Bwana, ninatumikia sehemu yangu hapa gerezani, kuubeba mzigo ulionipasa. Nasema kwa imani katika Neno la Mungu kuwa anakuja upesi. Suala ni; Je, ajapo mwana wa Adamu ataikuta imani duniani?

Uwe mwaminifu katika Neno la Mungu, kuwa na moyo wa subira, kwa kuwa hakuna tendo lolote la mwanadamu litakalobakia kuwa siri, bali yote yatafunuliwa wazi.

Neema na Baraka za Mungu zizidishwe kwako katika jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Ni mimi Mchungaji. Yusef Nadarkhani
niliyeko kwenye gereza la Lakan, katika mji wa Rasht. Iran.

Maelfu ya watu kutoka duniani kote wanamimina barua kwenye balozi za Marekani kuomba huruma, ili mchungaji huyo asinyongwe. Hata hivyo mamlaka za kiislamu za Irani zimekuwa zikizidisha shinikizo kwa kumpachikia makosa mapya . Wiki iliyopita walimpachikia makosa mawili wakimsingizia eti alibaka, lakini hawakuweza kuonesha mlalamikaji.

Mawakili wake walipogundua hilo waliamua kutafsiri hukumu ya mahakama iliyomtia hatiani ambayo ilionesha kuwa alishtakiwa kwa makosa ya kuusaliti uislamu na Mtume Muhamad kwa kuacha dini ya Kiislamu na kuwa Mkristo.

Kosa lingine lililopo kwenye hukumu hiyo linaelezwa kuwa, ni kuwashawishi watu wengi wauchukie uislamu na kujiunga na Ukristo, jambo ambalo ni kosa kubwa sana katika taifa hilo la kiislamu.

Lakini ili kuhakikisha kuwa mchungaji huyo ananyongwa haraka mamlaka hizo zimempachikia kosa lingine jipya ambalo ni kubwa zaidi pengine kuliko makosa yote katika utawala huo.

Taarifa mpya zinadai kuwa mchungaji huyo ameshtakiwa kwa kosa la kufanya ujasusi kwa niaba ya Israeli, akipatikana na kosa hilo anatakiwa kunyongwa dakika chache tangu saa ya hukumu. Washtaki pia wanatafuta jinsi ya kumshtaki mkewe kwa kosa kama hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Right Watch, mchungaji huyo katika hatua za mwisho za hukumu yake aliitwa na jaji mkuu akaulizwa iwapo yupo tayari kumkana Bwana Yesu na kurejea katika uislamu ili asinyongwe, lakini akasema hapana, hawezi kumkana Yesu.

Jaji wa Mahakama Kuu aliniuliza: “Uko tayari kumkana Yesu na kurejea kwenye uislamu wako, uepuke adhabu ya kunyongwa mpaka ufe?” Nikamuuliza nimkane Yesu! Hapana siko tayari…bora ninyongwe….”

Miongoni mwa wale walioko mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanaokoa maisha ya mchungaji huyo ni Spika wa Bunge la Marekani, ambaye ameungana na maseneta sita, kuandika barua kali, kuiomba Iran isimnyonge mchungaji huyo, lakini mwisho akaonya kuwa ikiwa atauawa damu yake itakuwa ukiulilia utawala wa kiislamu wa Iran na kamwe hautapata nafasi ya kujihifadhi katika uso wa sayari hii.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa na dini wanaeleza kuwa ikiwa mchungaji huyo atauawa basi hiyo inaweza kuwa alama ya mwisho kabisa ya uhai wa utawala wa Iran, ambao umesalia wenye msimamo makali baada ya Iraq, Misri na Libya kusambaratika vibaya.

Mchungaji Nadarkhani ameoa na ana watoto wawili ambao ni Daniel (9) na Joel (7). Wote wanaishi nchini Irani pamoja na mama yao na wako kwenye huzuni kubwa wakimlilia baba yao aokoke . Mchungaji Nadarkhani ni mwanachama wa kanisa la chini kwa chini huko Irani

Ikiwa unataka kuungana na maelfu ya watu wanaofunga na kuomba kwa ajili ya mchungaji huyo na pia kuandika barua kwenye ubalozi wa Iran katika Umoja wa mataifa na ule wa Washington Marekani kushinikiza kuachiwa kwa Mchungaji huyo unaweza kutumia anuani zifuatazo:

Permanent Mission of the Islamic Republic of Iran in the United Nations
622 Third Ave. New York, NY 10017
Telephone: (212) 687-2020
email: iran@un.int

Iran's embassy in Washington, D.C:

Interests Section of Islamic Republic of Iran
2209 Wisconsin Avenue Northwest, Washington, DC 20007-4127
Telephone: (202) 965-4991

No comments:

Post a Comment