OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, August 28, 2011

Mashirika ya misaada yahaha kuokoa Wasomali wanaokufa kwa njaa



· Kundi la al-Shabaab latoza misaada kodi


MAKUNDI ya watoa misaada wa kimataifa nchini Somalia yanahaha kuokoa maisha ya watoto wanaoangamia kwa njaa kali, huku wakitatizwa na kundi la kigaidi la al- Shabaab ambalo linataka wahisani wanaoingiza chakula cha misaada kulipa kodi.

Somalia imekuwa na tatizo la njaa kwa miongo sita sasa, kutokana na ukame ambao umepelekea watu zaidi ya milioni 11 kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa chakula, wengi wao wakiwa ni watoto na wazee wasiokuwa na uwezo wa kupigania chakula hicho.

Hadi sasa watu zaidi ya 1,000 wamekwisha poteza maisha nchini humo na wengine kulingana na hali kuzidi kuwa mbaya wamejikuta wakiyakimbia makazi yao na kuhamia mataifa jirani yakiwemo Tanzania na Kenya.

“Wamekuwa wakikimbia kwa kuwa wengi wamejikuta wakipoteza mifugo kutokana na ukame kuwa mkali katika maeneo mengi, na hilo limekuja baada ya kuona hakuna namna yoyote ya matumaini,” alisema Bw. Mark Bowden mratibu kutoka Umoja wa Mataifa ambaye amekuwa bega kwa bega na waathirika ili kuwapa msaada.

Alisema kwamba, kwa muda mrefu Somalia imekuwa haina mvua na si hilo tu, pia wamekuwa na migogoro ya wao kwa wao, hali hiyo imewafanya watu wengi kukumbwa na utapiamlo na ikiwa mama atakuwa na ugonjwa huo ni dhahiri kuwa hata mtoto hatokuwa na msaada.

Wasomalia wamekuwa wakilia kuomba msaada kwa watu mbalimbali, kilio chao kikubwa ni kwa UN ambapo waliiomba ijitokeze kuwasaidia ili kuokoa maisha yao na kwamba dunia iwaangalie.

Hata hivyo juhudi za UN kuiokoa Somalia zimekuwa zikikwamishwa na kundi la kigaidi la kiislamu nchini humo, al-Shabaab, kutokana na kwamba mara wanapokuwa wameleta misaada ya chakula, kundi hilo limekuwa likiwataka walipe kodi au wakati mwingine kuwaomba rushwa jambo ambalo lilielezwa kuwa, si limewakatisha tamaa watu wengi.

Watoaji wengine wa misaada nchini humo kama; shirika la mpango wa chakula ulimwenguni (UN-WFP) wamekuwa wakilalamika kwamba nchi hiyo ni hatari sana kutokana matatizo wanayokumbana nayo wakati wa kutoa misaada, huku wakilalamikia vitendo vya utekaji nyara wa mara kwa mara.

Inadaiwa kwamba watu zaidi ya kumi wamekufa kutokana na kushambuliwa wakati wa kuwasaidia wasomali wengi zaidi wamekuwa wakikimbilia Ethiopia na Kenya.

Shirika la Word Vision ni moja kati ya mengi ambayo yamekuwa yakitoa msaada kwa waathirika wa baa la njaa nchini Somalia.

Ili kuweza kutia mkono wako kwa watoto na wazee wanaokufa kwa njaa nchini Somali unaweza kutuma SMS kupiti "4africa" to 20222 pia unaweza kutembelea tovuti ya the World Vision, ama kwa kupiga simu 1-888-56-CHILD (1-888-562-4453).


No comments:

Post a Comment