OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 20, 2011

Ask.Kulola asema acheni kunywesha wenzenu

Na Calvin Nyorobi
 
ASKOFU  Mkuu wa Kanisa la EAGT nchini Dk. Moses Kulola, ameonya watu wenye tabia ya kishetani, ambao amedai kuwa wanawanywesha wenzao maji machafu yaliyooshea maiti kwa madai kuwa ni maji ya Baraka.
  Akihubiri katika ufunguzi wa mkutano wa Injili uliofanyika katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, Dk. Kulola alisema kuwa katika siku za karibuni imeibuka tabia mbaya inayofanywa na kundi la kishetani linalojivika ngozi ya kondoo na kujifanya kama ‘kanisa’ mjini Mwanza, lakini likiendesha matukio ya kustaajabisha sana ikiwa ni pamoja na kunywesha watu maji yaliyooshea maiti.
  Bila ya kutaja majina Askofu huyo alisistiza kuwa kundi hilo linalofanya ibada za kishetani, limekuwa likiendesha ibada zake usiku na likiigiza mambo yanayofanyika katika makanisa ya kiroho ikiwa ni pamoja na kuombea watu, lakini amepata ushahidi kuwa wanatumia mambo ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kuwanywesha watu maji yaliyooshea maiti.
  Gazeti la Jibu la Maisha linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu kundi hilo ambalo, kwa mujibu wa Askofu Kulola ni mawakala wa makundi ya kishetani yanayoibuka kwa kasi kubwa katika nyakati hizi za hatari.
  Alisema kwamba ni vema wale walio na Mungu wakaendelea kuangalia wokovu wao ili wasije kuanguka, kwani siku za leo shetani amekuwa akiwatafuta watu waliookoka ili awaangushe.
  “Nasikitishwa na habari za Kundi moja lililopo Mwanza ambalo limeibuka na kioja cha kuwanywesha watu maji ya kuoshea maiti, wakidai eti ni maji ya Baraka; huu ni uchafu mkubwa kwa watu wa Mungu,” alisema mtumishi huyo.
  Akielezea matukio yanayoashiria mwisho wa dunia, Askofu Kulola alisema kuwa kulingana na matukio ya kushangaza yanayozidi kujitokeza likiwemo la unabii wa uongo uliodai kuwa wateule wangenyakuliwa Mei 21, ni wazi kuwa dalili za hatari zimekaribia sana hivyo aliye mtakatifu azidi kujitakasa na yule mwenye kusita sita akimbilie haraka kwa Yesu akajiokoe.
  Kiongozi huyo mwanzilishi wa Kanisa la EAGT, alionya kuwa wanaokimbilia kunywa kikombe cha dawa huko Loliondo Arusha, kwa Mchungaji mstaafu wa kanisa la KKKT, Ambilikile Mwasapila, ni mfululizo wa matukio ya kustaajabisha sana yenye mkono wa ibilisi.
  “Siku moja nilipigiwa simu na waandishi wa habari, nilipoipokea wakanisalimia shikamoo Askofu, niligundua kuwa hawajaokoka hivyo nikawaitikia tu kwa haraka, nao wakasema …… Askofu tumewaona Wachungaji (majina nimeyahifadhi) kutoka Dar nao wamejipanga kupokea kikombe;  na wakaongeza tena kwamba…. hivi Mchungaji mnatupeleka wapi…..? nikawajibu kuwa hao wamepotoka; Mungu wangu mimi haponyi kwa miti shamba,” alisema Askofu Kulola.
  Hata hivyo alieleza kwamba, kikombe ambacho kinapaswa kunywewa na Wakristo wote ambacho hata yeye (Kulola) anacho ni kimoja tu, ambacho ni cha mateso ya Yesu Kristo, na wala si dawa ya miti shamba.
  “Yesu haponyi hivyo, Mchungaji wa Loliondo alitokewa na kitu kingine kabisa na wala si Mungu, aliyemtokea anamjua yeye. Sisi hatuhusu wala hatumuamini,” alisema.
  Katika mahubiri yake aliendelea kufafanua kwamba matukio yanayotokea hivi sasa ni ishara tosha ya siku za mwisho, kulingana na vita zinavyoendelea kupiganwa katika nchi na Falme za kiarabu, na kuwa Wakristo wanapaswa kujipanga ikiwa ni pamoja na kuiombea nchi.
  “Wapendwa nchi yetu ni nzuri mno kuliko nchi zingine, tunaamini sana ndio maana tunapata hata nafasi ya kusali na kuhubiri injili kuliko nchi zingine, tuiombeeni nchi yetu tena kwa machozi; Mungu ainusuru na majanga mabaya yanayojitokeza  sehemu mbali mbali duniani,” alisisitiza.
 

No comments:

Post a Comment