OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 20, 2011

Mbwa mwitu wamevamia zizi la kondoo!

Katika siku za karibuni, kumekuwa na wimbi la migogoro katika jamii na hata kwenye nyumba za ibada ambayo kwa njia moja au nyingine imekuwa ikichafua hali ya hewa, na kuzorotesha kazi ya Mungu na hata maendeleo ya wanadamu katika sayari hii.
  Tumeshuhudia  ikiibuka migogoro mingi,  tena isiyo na sababu za kuibuka kwake. Uchunguzi rahisi unaonesha kuwa vyanzo vya migogoro hii ni baadhi ya watu wanaodai kuwa miongoni mwa waumini makanisani, ingawa tabia zao na mwenendo haiendani na Ukristo  kabisa. Ni watu hao ambao mara nyingi huibua migogoro, isiyo na kichwa wala miguu na kisha kukimbilia kwenye vyombo vya habari kutoa malalamiko dhidi ya viongozi na hata waumini wenzao.
  Ni kwa sababu hiyo, tumeamua kutumia nafasi hii kulionya Kanisa la Mungu kuwa macho, kwa kuwa limevamiwa na kundi la mbwa mwitu ambao ni mawakala wa ibilisi wenye lengo la kulichafua kanisa kwa kujifanya waumini na kisha kuibua migogoro ya ndani.
  Hatuna haja ya kutaja majina ya wahusika, ingawa wengi tunawafahamu na tunaushahidi wa kuthibitisha kuwa wamekubali kutumiwa na ibilisi kuwa mawakala, wakipenya makanisani na kumwaga sumu hasa kwa waumini wachanga.
  Tunawasihi waghairi njia zao mbaya na kumrudia Yesu Kristo, kwa kuwa yupo tayari kuwasamehe na kuwapa nguvu za Roho Mtakatifu, zitakazowawezesha kuushinda uovu, lakini wakishupaza shingo watapotea milele.
  Haya si mambo mageni sana, yalikuwepo tangu awali  na hata mitume 12, waliokuwa na Bwana Yesu alipokuwa katika umbo la mwili hapa ulimwenguni zaidi ya miaka 2000 iliyopita, alikuwepo mmoja ambaye alikuwa wakala wa shetani na mwisho alimsaliti.
  Lengo letu kuyaandika haya ni kulitahadharisha Kanisa la Kristo kuwa makini na watu wanaojiafanya waumini tena wengine wakijifanya kuokoka, kwa mbwembwe na kueleza historia ya uchawi mwingi waliokuwa wakiufanya huko nyuma, lakini baada ya muda utasikia ama kaiba na kukimbia au kaibuka na migogoro .
  Tunajua kuwa mambo haya hayafanyiki kwa bahati mbaya, la hasha, huu ni mkakati maalumu wa ibilisi wa kukabiliana na kansia. (tazama habari katika Uk. 1).
  Tunakuwa na ujasiri wa kuyasema haya, kwa kuwa  mawakala hawa wamejaribu mara nyingi  kupenyeza sumu zao kupitia vyombo vya habari likiwepo gazeti hili, lakini kwetu waligonga ukuta kwa kuwa tumejizatiti kuilinda imani na kamwe hatuwezi kuwa daraja la kufanikisha kazi za ibilisi.
  Tunavishauri pia vyombo vya habari nchini, kuwa makini na taarifa wanazoletewa, wasizikimbilie bali wazipime ili kubaini uhakika wake, wachunguze sababu za waleta taarifa zilizojificha nyuma ya pazia na ikiwezekana wawasaidie kwa kuwakemea, kwa kuwa  kazi wanayofanya ya kuchafua wengine haina tofauti na ile iliyofanywa na wale waliotunga mashtaka ya uongo ili Yesu kumtia Yesu mikononi mwa wauaji.
  Kabla ya kushika kalamu na kuandika tuzikumbuke zele Ole …..alizozitoa Bwana Yesu katika Biblia kwenye kitabu cha Mathayo.
  Pia waumini wenye mioyo safi, wanapaswa kuwa makini na kukwepa mitego ya mawakala hawa ambao hujaribu kuwatumia kama daraja ili kufanikisha malengo yao yasiyokuwa wazi.
 
 

 

No comments:

Post a Comment