OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, June 26, 2011

Kauli ya TAG kuhusu habari iliyoandikwa na Habari Leo

* Gazeti lamuomba radhi Askofu Dk. Mhiche
* Katibu Mkuu atoa ilani kwa vyombo vya habari

Na Mwandishi Wetu
KANISA la Tanzania Assemblies of God, (TAG) limetoa ufafanuzi kuhusu habari iliyoandikwa kwa makosa na Gazeti la Habari leo katika toleo lake namba 01634, la Juni 12, mwaka huu na kisha kukanushwa na gazeti hilo hilo katika toleo lake la Juni 19, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TAG, Rev. Ron Swai, Kanisa limefanya hivyo kwa faida ya wachungaji wake, waumini na Watanzania kwa ujumla, hasa baada ya kuwa gazeti la Habari Leo lililoandika habari hiyo kwa makosa limekiri kosa, likakanusha na kuomba radhi kwa Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa la T AG, Dk. Magnus Mhiche, ambaye habari hizo zilimlenga zaidi.
Mchungaji Ron, alisema kuwa ameona umuhimu wa kufafanua jambo hilo na hata kuchapisha tena taarifa ya kukanusha iliyoandikwa na Habari leo, sambamba na barua ya kuomba radhi kwa Makamu Askofu Dk. Mhiche, kwa kuwa baadhi ya vipengere katika habari husika, licha ya kugusa kanisa la mahali pamoja, TAG, Mbagala Kizuiani pia ziligusa Kanisa la TAG kwa ujumla pamoja na wachungaji.
“Nitumie tu nafasi hii kuwahakikishia wachungaji, waumini na Watanzania kwa ujumla kuwa taarifa husika zilikuwa zimeandikwa kwa makosa makubwa ya kisheria, kiandishi na kimaadili, kama ambavyo wahusika wamekuwa waungwana kukubaliana na makosa hayo kuomba radhi kama inavyoonyesha kwenye barua yao na taarifa ya kukanusha,”alisema katibu huyo na kuongeza:
“Ningependa pia kuwakumbusha waandishi wa habari, umuhimu wa kuwa makini zaidi katika kufuatilia mambo na kupata ufafanuzi wa kina kutoka kwa wahusika kabla ya kuandika, kwa kuwa madhara ya taarifa zisizo sahihi ni makubwa sana yanaweza kuleta madhara kwa vyombo husika na hata kuvuruga amani ya nchi. Sisi Tanzania Assemblies of God, tupo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanahabari wenye nia njema ya kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kuwapasha watu habari.”
Ifuatayo ni taarifa ya kiungwana ya Gazeti la Habari Leo iliyokanusha habari yao waliyoandika kwa makosa na Juni 12, mwaka huu:
Kumradhi Kanisa la TAG, Askofu Dk Mhiche
JUMAPILI ya Juni 12, gazeti hili liliandika habari yake kubwa ukurasa wa mbele kwamba ‘Kanisa lakumbwa na kashfa ya ngono’.
Habari hiyo ilihusisha Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) na pia kumtaja Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk Magnus Mhiche, kuwa anahusika na kuvunjika kwa ndoa ya muumini wake, Emilius Elisha.
Ilidai pia kuwa baada ya kuvunjika kwa ndoa ya Elisha na mkewe Rose, Askofu Dk Mhiche alimpangishia chumba na pia kumtafutia kazi St Matthew.
Baada ya uchunguzi wa kina, imebainika kwamba tuhuma hizo hazina ukweli, Askofu Dk Mhiche hajahusika na mambo yote hayo na pia Kanisa halihusiki kwa vyo vyote na kuvunjika kwa ndoa hiyo.
Ukweli ni kwamba Elisha si mshirika wa Kanisa hilo baada ya kufukuzwa ushirika Aprili 4 mwaka jana, kutokana na kukiuka maadili ya Kanisa na amekuwa akizusha tuhuma dhidi ya Dk Mhiche kutokana na hasira za kufukuzwa kanisani.
Pia ni kwamba Rose na Elisha wametengana kutokana na sababu za ndani ya ndoa yao na hivi sasa mkewe huyo amepanga chumba chake, baada ya kulipiwa kodi na kaka yake na anafanya shughuli ndogo za kuuza mitumba, kinyume na madai ya awali.
Kutokana na habari hiyo, Kanisa, waumini na Dk Mhiche, ndugu, jamaa na marafiki zake, walipata usumbufu mkubwa, hivyo tunachukua fursa hii kuwaomba radhi wote hao na kuwapa pole kwa usumbufu uliojitokeza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Mhiche alisema kuwa inaonekana kwamba kuna watu wenye hila ambao wameamua kunichafua mimi na Kanisa kwa maslahi yao binafsi.
Aliwataka waumini, wachungaji na watanzania kwa ujumla kuwapuuza watu hao na kuendelea kuwa na imani kwa Kanisa huku akitoa mwito kwa wanaotaka kuombwewa kufika kanisani.
“Yawezekana kuna watu wamepanga kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari kama vyenu hivi, kulichafua jina la Kanisa na hata mimi binafsi kwa sababu ya matatizo yao binafsi ambayo hayakubaliki kikanisa.
“Haya ni majaribu ya shetani, hivyo wachungaji na waumini wasikate tamaa kumtumikia Mungu kwa sababu hizi ni nyakati za mwisho na mambo mengi yanaweza kujitokeza … tuwe imara kukabiliana nayo,” alisema Askofu Dk Mhiche.
Alitoa mwito pia kwa vyombo vya habari kuwa makini na watu wa aina hiyo, na kuchuja mambo kabla ya kuyatangaza, kwa sababu mengine ni uzushi ambao unaweza kusababisha athari mbaya kwa jamii. – Mhariri.”
Pamoja na habari hiyo, Gazeti la Habari leo pia liliandika barua kwa Makamu Askofu mkuu wa TAG, DK. Magnus Mhiche yenye kumbu kumbu namba; Kumb. Na. : JK/E-HL/TSN/455/2011, kumuomba kiongozi huyo wa kiroho msamaha na kumshukuru kwa kukubali kwake kusamehe. Ifuatayo ni barua hiyo:
“Makamu Askofu Mkuu – TAG (Askofu Dk. Magnus Mhiche),
Tanzania Assemblies of God (TAG),
S.L.P. 70144,
DAR ES SALAAM.
YAH: KUMRADHI NA SHUKRANI
JUMAPILI ya Juni 12, Gazeti letu la HABARI LEO Jumapili, liliandika katika ukurasa wa mbele habari iliyokuhusisha wewe na kanisa na kuvunjika kwa ndoa ya Emilius Elisha ikidai kuwa kuvunjika huko chanzo ni wewe.
Kwa niaba ya wenzangu wa gazeti hili, nakiri kwamba tulikosea kuiandika habari hiyo, huku ukweli ukiwa ni kwamba huhusiki namna yoyote na mtafaruku wa ndoa ya wawili hao na pia kanisa halina mchango wowote katika hilo.
Naelewa maumivu uliyoyapata siku habari hii ilipotoka, naelewa usumbufu uliokupata kutokana na simu ulizopigiwa zikiwamo za kukupa pole na kukutakia uvumilivu. Lakini naelewa pia usumbufu na mkanganyiko uliowapata waumini wako wa kanisa.
Yote haya yalitokana na nguvu za shetani ambazo zilitupofusha, na hata tukashindwa kubaini kuwa tulilokuwa tunalifanya ni kosa, lakini baad ya mazungumzo yetu na wewe (Rejea Juni 15, 2011), tukathibitisha, kuwa tulitumika bila kujua na hivyo kuharibu upande wa pili (wewe na Kanisa).
Tunarudi tena kwa mara nyingine, kukuomba radhi wewe binafsi, ndugu na jamaa zako, kanisa na waumini wake, kwa usumbufu uliosababishwa na habari hiyo na tunaahidi tutakuwa makini zaidi ili hali kama hiyo isijirudie na tutaimarisha uhusiano na ushirikiano wetu kikazi na kiroho pia.
Lakini tunapenda kukushuru wewe na wasaidizi wako, kwa uelewa wenu kwa maelezo yetu, na pia kwa kukubali kutusikiliza na hat akufikia makubaliano ya jinsi ya kumaliza tatizo hili. Hakika mlituonesha moyo wa uvumilivu, upendo na kusamehe.
Hivyo ndivyo binadamu katika dunia hii tunavyopaswa kuishi kwa kukubali makosa na pia kusameheana na hayo ndiyo mapenzi ya Mungu wetu.
Tunakuombea wewe, wasaidizi wako na waumini kwa ujumla kwa Mungu aendelee kukupeni nguvu hizo za kukubali kupokea wakosefu wenu na kukaa pamoja nao mezani na kukabili matatizo yaliyo mbele.
Tunaamini msamaha uliotupa ulikuwa ni wa dhati, nasi tunaahidi kuendelea kushirikiana na Kanisa kwa mema nay ale yanayoepusha migongano miongoni mwetu.
Ahsante sana. Mungu awaangazie
Joseph Kulangwa
MHARIRI MKUU HABARILEO.”

No comments:

Post a Comment