OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 20, 2011

Kumtambua Mwenzi kwa Kutumia Karama za Roho Mtakatifu


Maono ya mchana: “Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasena, kuna nini Bwana? Akamwambia sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” Matendo 10:3-4.
 
Ni vema mkafunuliwa nyote wawili!
 
  Mtume Petro pia aliona maono mchana waziwazi bila kuwa katika usingizi. Mungu anapotaka kukufunulia mwenzi wako kwa njia ya maono ya usiku au ya mchana (ya waziwazi), atafanya hivyo pia kwa mwenzi wako mtarajiwa ili asiwe na tashwishi utakapochukua hatua na kumwendea.
  Ndiyo maana Mungu aliposema na Kornelio kwa habari za wokovu wake, na kumuunganisha na Petro ambaye kwa mila za Kiyahudi hakuruhusiwa kuingia kwa watu wa mataifa, kwani Kornelio alikuwa Mrumi, Roho Mtakatifu aliyemfunulia Kornelio alifanya hima kumfunulia na Petro pia, ili asipate tashwishi na kukataa kufuatana na wajumbe waliyotumwa naye.
Tunsoma: “Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana, akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao wataambao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia kusema, ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikamwambia, vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokelewa tena mbinguni.
  Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
  Na Petro alikuwa  akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma. Petro akawashukia wale watu, akanena, mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani? Wakasema Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako… Hata siku ya ili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao… Matendo 10:9-23.
 
Karama mbili zimetumika
 
  Katika kisa hiki tumeona kuwa Kornelio na Petro, wote wawili, walipata maono waziwazi kwa nyakati tofauti. Kornelio saa tisa za mchana na Petro saa sita adhuhuri. Pia tumeona kuwa Baada ya Petro kupata ugumu wa kutambua maana ya yale maono, Bwana alimsaidia kwa kutumia karama nyingine tofauti, yaani ‘kusikia Sauti ya Roho Mtakatifu’ akimwambia kuwa nje kuna watu watatu ambao wanamtafuta na asiwe na tashwishi juu yao bali aende nao kwani yeye Bwana ndiye amewatuma kwake.
  Kweli akatoka nje na kukuta kuwa ni watatu kama alivyokuwa ameambiwa na Roho Mtakatifu, hivyo akasema kwa ujasiri “mimi hapa ndiye mnayemtafuta.” Lengo la Roho Mtakatifu kumwambia kuwa huko nje anasubiriwa na watu watatu, ni kumwezesha kuthibitisha kuwa kweli watu hao ni watatu na hivyo wametumwa na Mungu. Hii pia ilikuwa ni ishara ya kuthibitisha maono aliyopata.
  Hata katika kumtafuta mwenzi. Kama binti atafunuliwa na Roho Mtakatifu kwa njia ya ndoto, njozi, maono au sauti ya Mungu, si vema akuurupuke na kwenda kumtamkia mvulana kuwa yeye ndiye mchumba wake. Kawaida ya Waafrika mvulana ndiye humtamkia binti kwanza. Ukifanya tofauti, unaweza kutiliwa mashaka na kupoteza muujiza wako.
  Usiogope kwamba mtarajiwa wako anaweza kujua kuwa anatakiwa kukuchumbia, kwani Mungu yule aliyesema na wewe kwa njia ya ndoto, njozi, maono au karama nyingine yoyote, atasema na mwenzio pia, ili yeye ndiye aje, kama wewe ni binti. Na kama mvulana ndiye kafunuliwa, asimlazimishe binti kuamini kuwa kweli kafunuliwa na Mungu. Kwa nini? Kwa vile mafunuo hayo ni sharti kwanza yathibitishwe kwa binti naye kufunuliwa. Kama hajafunuliwa na moyo wake ukajisikia vibaya juu ya jambo hilo na kukosa amani, huyo anaweza kuwa si Mungu aliyekufunulia.
  Ndiyo maana ni lazima pande zote mbili zithibithishe na kujiridhisha kila upande kuwa kweli Mungu ndiye ameanzisha jambo hilo. Kinyume chake unaweza kudanganywa na mtu aliyepata maono batili kutokana na jinsi anavyokupenda au anavyokutamani, mkaoana nje ya mapenzi ya Mungu, ndoa yenu ikawa ngumu kupindukia na kuwafanya muishi katika mateso maisha yenu yote!
  Mimi nilipoona maono kuhusu binti ambaye sasa ndiye mke wangu, nilikuta kuwa yeye alitangulia kushuhudiwa moyoni mwake, lakini akaogopa kunitamkia. Nilipopata uhakikisho wa Roho Mtakatifu na kumtamkia, hakupoteza muda kuomba kwani alikuwa tayari anafahamu jambo hilo. Na hata Shetani alipojaribu kupinga tusioane, alishindwa waziwazi kwani tulimshambulia sote wawili mpaka tukafanikiwa kuoana. Na sasa tunaishi maisha mazuri ya ndoa na ya utumishi.
  Baadhi ya ndugu walikuwa wamenuia kuuvuruga uchumba wetu ati kwa sababu tumekaa muda mrefu bila kuoana wakati yeye (mchumba wangu) akisoma nje ya nchi. Tulimlilia Mungu kwa sauti moja na mchumba wangu mpaka nikapangiwa mahali na siku ya arusi. Alirudi nchini tukafunga ndoa, mambo yote yakeenda vizuri, tukaziona baraka za Bwana. Hata kwako Bwana atafanya kama unamtumikia kwa uaminifu.
 
Roho Mtakatifu habadiliki!
 
  Watumishi wote wa Mungu wa Agamo la Kale na wa Agano Jipya walitumiwa na Mungu kwa maono, njozi ndoto na mafunuo. Hata wewe Mungu anaweza kukutumia leo hata ukaweza kutambua kirahisi mwenzi wako wa maisha. Tunasoma kuwa Danieli alikuwa na ufahamu “katika maono na ndoto.” (Danieli 1:17). Mtume Paulo alijaliwa kupata “maono na mafunuo ya Bwana,” yakamsaidia sana katika huduma yake (2Kor.12:1). Wewe pia Mungu anakutambua na atakuwa tayari kukutumia kama umeamua kumtumikia kwa uaminifu. Bwana atakuongoza, sio tu katika kumtambua mwenzi wako wa maisha, bali katika kila jambo utakaloamua kufanya kwa ajili ya Bwana na kwa ajili yako mwenyewe.
 
  Itaendelea.....
 

No comments:

Post a Comment