OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 20, 2011

Viongozi wa dini wavunja ukimya posho za Wabunge

Na Waandishi Wetu
 
MJADALA kuhusu malipo ya posho kubwa kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali, ulioibuliwa  bungeni na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), na baadaye kuungwa mkono na kambi ya upinzani, umeingia  katika hatua mpya baada ya viongozi wa dini na wanaharakati wa makundi ya kutetea haki za binadamu, kuvunja ukimya na kutoa kauli kali.
  Wakiongea na na Jibu la Maisha, kwa nyakati tofauti viongozi hao wa dini na wanaharakati juu ya hoja hiyo ambayo imekuwa gumzo kwa watu mbalimbali walisema kwamba, ni lazima wabunge waangalie haki na usawa kwa watu wote na hasa mtanzania anayeishi chini ya dola moja kwa siku.
  Askofu Msaidizi Jimbo la Kagera, Methodius Kilaini alisema kwamba, kwa sasa imeonekana kana kwamba bungeni ni sehemu ya biashara na ndiyo maana watu hukanyagana kusaka kupata nafasi hizo, ambapo hata wanapozipata hawawazii tena wananchi isipokuwa namna ya wao kujineemesha na posho.
  “Hii sasa imekuwa kama ni biashara, wewe fikiria mwananchi wa kawaida anavyoishi kwa shida halafu bado watu wanaodai ni wawakilishi wao wanavyoishi; badala ya kuwatetea, wao wanaangalia matumbo yao pamoja na familia zao tu,” alisema Askofu huyo na kuongeza:

  “Hawa wana alawansi nyingi, mimi naona wangebaki na hizo tu badala ya kupewa nyingine katika vikao vyao,  sambamba na madai ya kuongezewa posho.”
  Alisema kwamba ikiwa wasomi wa taaluma mbalimbali nchini na wengine hutumia muda mwingi kukamilisha kile wanachokiita hulipwa pesa kidogo, iweje wabunge walipwe mamilioni kwa kukaa na kusikiliza mijadala kwa muda mchache?
  “Pesa wanazopata kwa mwezi zinawatosha kabisa, hizo posho wanazolipwa zipelekwe kwa watu wa kawaida; nadhani Zitto Kabwe kaona mbali alikuwa sahihi kabisa kugomea,” alisema mtumishi huyo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kagera.
  Mwanaharakati mwingine ambaye naye alitoa maoni yake ni Bw. Emmanuel Kibona ambaye alisema kwamba, Katika Biblia Yesu anashauri kuwa; asiyefanya kazi na asile, hivyo posho zinazotolewa kwa ajili ya mtu kukaa tu (sitting allawance) ni dhambi mbele za Mungu.
  “Hapo hakuna kazi, wazi kuwa kupokea posho hizo ni dhambi kwa kuwa hakuna kazi inayofanyika, kupokea malipo bila kufanya kazi ni dhambi na inaashiria kukosa uaminifu na umakini kwa wanadamu na Mungu pia,” alisema mwanaharakati huyo.
  Alibainisha kuwa, Wabunge huwaongoza wapiga kura ambao ni masikini kiasi kwamba, kupata mlo mmoja kwa siku ni shughuli, lakini wao kwa kutoogopa au kutomjali mwananchi  hukubali kulipwa posho kwa kukaa tu!
  Sambamba na hilo alibainisha kwamba, Posho wanazopewa wabunge katika vikao vyao ndizo zilizolifilisi taifa, kiasi cha kuweka matabaka ya wenye nacho na wasio nacho. Huku akiongeza kwamba ni bora posho hizo (sitting allowance) ziondolewe.
  “Sio hilo tu, pia hata pesa zinazotolewa kwa watendaji wa serikali ni heri nazo zikafutwa kabisa ili kulinda utawala bora na uadilifu, posho hizo zinasababisha watu wang’ang’anie madaraka serikalini na kutafuta ubunge kwa nguvu.
  Mwenyekiti chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, naye hakuwa nyuma akiongea na Jibu la Maisha alikuwa na haya ya kusema: “Hakuna haja ya POSHO, pesa hizo zinatakiwa zipelekwa kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa ikiwa ni pamoja na kwa wapiga kura.”
  Alisema kwamba, mashuleni kuna upungufu wa majengo ya madarasa, vyakula na vifaa vingine vya kusomea, hivyo ni bora likaangaliwa hilo ili pesa hizo zikapelekwa huko katika kuondoa changamoto zinazowakabili wananfuzi na walimu kwa ujumla.
  Pia aliongeza kwamba, wajawazito kwenye vituo vya afya wanapata shida wakati wa kujifungua, hiyo ikiwa busara kidogo itatumika  kwa wabunge basi wataona umuhimu wa kuchukua pesa hizo na kupeleka hospitalini.
  Akizidi kutoa mchanganuo Bi. Nkya aliongeza kuwa, suala hilo pia linaleta ubaguzi katika taifa kutokana na kwamba wako watu wengi ambao ni masikini, na wengine wachache ambao wananawiri kutokana na pesa hizo pasipo kujali wenzao.
  “Kuna wengine ambao hizo shilingi 70,000 wanazopewa wabunge kwa siku, ni mshahara wao wa mwezi mzima na unaishia kulipa madeni na anarudi nyumbani akiwa na kiasi cha shilingi 10,000; sasa hapa usawa uko wapi.
  Mchungaji Christoper Mtikila ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu alisema kwamba, kuongezeka kwa mambo ya kifisadi na rushwa  imesababishwa na vitu vinavyofanana na hivyo, watu kupenda sana pesa.
  “Mtu kasomea udaktari karibu miaka 21 lakini anacholipwa ni kama hakuna kitu, halafu mtu mwingine akae tu, muda mchache alafu akitoka hapo analipwa pesa nyingi, hii ni njia mojawapo ya kusababisha rushwa nchini, ndiyo maana kila mtu anapakimbilia huko,” alisema Mtikila.
  Wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe  Zitto, toka kambi ya upinzani CHADEMA aliibua hoja akitaka posho wanazopewa katika vikao zifutwe, huku akitaka pesa hizo zipelekwe kwenye mambo ya maendeleo kitu ambacho kiliungwa mkono na watu mbalimbali akiwemo Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba
  Wabunge wamekuwa wakilipwa mshahara shilingi Mil. 2.5  na shilingi milioni mbili za kutumia katika majimbo yao, sambamba na 150,000 za kujikimu kila Bunge linapokaa..

No comments:

Post a Comment