OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 13, 2011

Biblia yazua kizazaa kortini

 
MVUTANO mkali unaohusisha vifungu vya sheria na maandiko matakatifu ya Biblia umeibuka katika Mahakama ya Ardhi Tanga, baada ya  kiongozi mmoja wa dini nchini kukataa kuapa kwa Biblia akidai kuwa, kufanya hivyo ni kukiuka maagizo ya BWANA Yesu Kristo aliyoyatoa mlimani, yaliyoelezwa wazi katika kitabu cha Mathayo 5:33-37.
  Utata huo wa kisheria uliibuka hivi karibuni katika Mahakama ya Ardhi mkoani Tanga, baada ya Askofu  Dk. Erick Mwambigija, kukataa kuapa mbele ya Hakimu, Biteki Kishenyi, anayesikiliza shauri namba 111, la mwaka 2011, lililofunguliwa na kanisa la  Church of God of Prophesy, dhidi ya aliyekuwa mtumishi wake mkoani Tanga , Bw. Danford Makota,  ambaye anatuhumiwa kuuza  eneo la kanisa kwa Muarabu ili ajenge kituo cha mafuta.
  Mbele ya Hakimu Kishenyi,  Askofu Mwambigija ambaye ni Mwangalizi Mkuu wa Makanisa ya  Church of God Tanzania, alitakiwa kushika Biblia na kuapa, kabla ya kutoa ushahidi wake, lakini alikataa akimweleza hakimu kuwa hawezi kushika Biblia Takatifu kisha anyooshe mkono kuelekea mbinguni na kuapa kwa kuwa, kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha Biblia katika kitabu cha Mathayo 5:33-37.
  Baada ya Askofu huyo kugoma kuapa akitaka utumike utaratibu mwingine wa kumuuliza maswali, badala ya kumuapisha kwa kuwa kufanya hivyo ni kumuasi Mungu anayemtumikia. Hakimu huyo aliwataka mashahidi wengine kuapa kisha kuendelea na ushahidi, lakini wote walifuata nyayo za kiongozi wao na kukataa kuapishwa.
  Hali hiyo ilizua mvutano wa kisheria baada ya hakimu kuonya kuwa kutokula kiapo kunaweza kuathiri kesi hiyo na ikafutiliwa mbali, lakini mwanasheria wa kanisa, Bw Wenceslaus Mramba, alipinga hoja hiyo kisheria akisema sheria inatambua pia utaratibu unaojulikana  kama “Assirnation” (kuthibitisha) badala ya kutumia neno kuapa na hailazimishi shahidi kuapishwa.
  Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Wakili Mramba, alisema kuwa kisheria  mtu halazimiki kuapa kwa kuwa hakuna sheria inayotoa sharti la kiapo kama njia pekee ya  kutumika kabla ya kutoa ushahidi mahakamani.
  Baada ya hakimu kubaini kuwa mvutano huo ni mkali, kwa kuwa unagusa hoja za kiimani,  aliamua kuahirisha kesi hadi Juni 21, mwaka huu ili apate nafasi ya kuperuzi vitabu vya kisheria kisha atatoa uamuzi ikiwa shauri hilo linaweza kuendelea na mashahidi wangetoa ushahidi wao  bila kuapa kwa Biblia.
 
  KESI YA MSINGI
  Mlalamikaji katika Shauri hilo ni Kanisa la Church of God, ambalo linadai kuwa Bw. Makota, ambaye alikuwa mtumishi wa kanisa hilo aliuza eneo la kanisa kwa Mwarabu ambaye alikusudia kujenga  kituo cha mafuta kisha kutoroka. Eneo lililouzwa limetajwa mahakamani hapo kuwa linathamani ya shilingi milioni 40.
  Mlalamikaji anadai kuwa  eneo hilo ni  mali ya kanisa, hivyo muuzaji hakuwa na haki wala mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, na anataka lirudishwe kwa mmiliki halali.
  Akiongea na Jibu la Maisha, baada ya kesi kuahirishwa Askofu Mwambigija alisema kuwa, msimamo wake uko wazi, ni kama ule wa akina Daniel mbele ya mfalme, kamwe hawezi kumuasi Mungu wake kwa sababu ya jambo lolote lile.
  “Sikia Bwana, hapa mambo yako wazi….Biblia ndiyo mwamuzi wetu wa mwisho; sisi tunaomfuata BWANA Yesu, tukiwa wanafunzi wake. Pale mlimani alituagiza akisema:
   “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo ila mtimizie BWANA  nyapo zake, lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;  wala kwa nchi, maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalem, kwa maana ndio mji wa Mfalame mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe wala mweusi. Bali maneno yenu yawe ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.” (Mathayo 5: 33-37)
  Kisha aliongeza: “Mimi naamini kuwa Mkristo halazimiki kuingia katika mgogoro na Mungu wake kwa ajili ya kuapa….sioni umuhimu wa wanadamu kuapishwa kwa Biblia kwa kuwa, kufanya hivyo ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na tunapomuasi Mungu tunaalika mabalaa katika taifa letu…”
  Akifafanua alisema kuwa, maelezo aliyonukuu kwenye kifungu cha Biblia aliyasema Bwana Yesu Kristo akiwa mlimani na ni agizo kwa yeyote anayeifuata  imani  ya Ukristo, hivyo hakuna  nafasi ya kupingana naye, ni ama kuufuata au kuukana Ukristo.
  “Kwa kweli kama nitapata nafasi ya kutoa maoni yangu katika mchakato huu wa katiba mpya nitasema wazi ya kwamba, hakuna haja ya kuwa na kifungu cha sheria kinachomtaka mkristo aape  mahakamani au mahala popote anapoteuliwa katika wadhifa fulani,” alisema  na kuongeza:
  “Ni afadhali kupata hasara yoyote ile katika maisha kuliko kuingia katika mgogoro na Bwana Yesu….alishasema tusiape, basi hilo ni la mwisho, mimi nilishapata hasara ya shilingi milioni moja kwa kukataa kuapa katika Mahakama kwa kuwa siwezi kuikiuka Biblia.”
  Akifafanua alisema kuwa, kipindi cha nyuma alikuwa na kesi katika Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, mbele ya hakimu Suma Sene (kwa sasa ni marehemu), ambaye alimlazimisha ashike Biblia aape, lakini alikataa na hakimu huyo akaifutilia mbali kesi hiyo na alikubali kupata hasara ya shilingi milioni moja ili kulinda Ukristo wake.
  Sambamba na hilo aliongeza kuwa, haoni faida ya wale walioapa kwa Biblia kwa kuwa wengi wao wameibuka kuwa mafisadi mashuhuri na wala rushwa wasiohofia kiapo hicho.
 
  MAONI YA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU
  Mmoja wa wanasheria mashuhuri nchini ambaye pia ni Mhadhiri wa Sheria, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benedict Mapunda, akitoa maoni yake kuhusiana na mkasa huo alisema:
  “Kuapa mahakamani ni amri ya  Kaisari, ambayo haipingani na Mungu … ila ukishaapa usiseme uongo, sema kweli tupu. Lakini pia si lazima kuapa mahakani kama imani yako hairuhusu. Kuna kitu kinaitwa “to affirm”(kuahidi kusema kweli bila kumtaja Mungu) na ushahidi wako unakubalika, ingawa mahakimu wamezoea kuapisha Wakristo wote.”
  Mwingine aliyechangia hoja hiyo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Theolojia cha kimataifa Global Harvest University” Samuel Mwaluvanda, ambaye alisema kuwa, kimsingi kuapa ni kinyume cha Neno la Mungu kwa kuwa Bwana Yesu alishakataza.
  Alisema kuwa, alishaonya hata wakati Waislamu wenye msimamo mkali walipoibuka kudai mahakama ya Kadhi kuwa, wakishikilia hilo Wakristo nao wataibuka na hoja ya kutaka kiapo kwa kutumia vitabu vya Mungu vifutwe.
  “Nijuavyo mimi kitheolojia, kuapa kwa Biblia iwe ni Mahakamani au pengine popote ni kukiuka Neno la Mungu aliye hai,” alisema mhadhiri huyo.

5 comments: