OTHER WEBSITE LISTS


Tuesday, June 14, 2011

Foleni za magari Dar Polisi wafunua nyuma ya pazia


Msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, unatajwa kama moja ya majanga sugu yanayokuza umasikini wa wakazi wa jiji hilo kubwa na kitovu cha biashara nchini. Wengi wamenyooshewa vidole wakitajwa kama chanzo kikuu cha janga hilo. UNGANA NA MWANDISHI Flora Matara katika kukuchambulia makala haya.



Safari yangu ilianzia Kimara, nakumbuka niliamka alifajiri na mapema ilipotimu saa 12:30 tayari nilikuwa ndani ya basi la abiri maarufu kwa jina la ‘dala dala’ nikielekea katika mihadi yangu na maafisa wa usalama barabarani. Siku hiyo usafiri haukuwa shida sana …. Ninamshukuru Mungu kwa hilo, lakini hata hivyo zahma ndani ya gari inanifanya nijiulize ni saa ngapi nitafika kwa wakuu hao ambao suala la muda kwao ni moja ya masomo wanayozingatia?
   Gari lenyewe lilikuwa katika mwendo wa kobe …… Mara imesimama……mara inatembea, kwa kweli ilikuwa ni shida tupu, kituo kimoja hadi kingine ilikuwa ni shughuli. Sikutaka kuiangalia saa yangu kwani ni kama ilikuwa ikikimbia….wakati mwingine nilitamani kumlazimisha dereva aongeze mwendo, lakini ilikuwa ni chini ya uwezo wake…. Sikuwa na jinsi niliendelea kuwa mpole huku nikitafakari mwisho wa haya yote.
   Nikiwa kwenye dimbwi la sintofahamu mara ninafika magomeni,…… nasikia kelele za watu naamua kuangalia dirishani kumbe ni wanafunzi wanaogombania kuingia katika gari; kondakta hataki kuwaruhusu, wamekaa muda mrefu  bila mafanikio, shuleni wamechelewa. Linaposogea mbele kidogo nashindwa kuyaamini macho yangu…..nagongana macho kwa macho na mnyororo wa magari.
   Uvumilivu unanishinda nikiangalia saa yangu inaniambia ni 2:00, miadi yetu na wakubwa zikiwa zimebaki dakika thelathini tu, naanza kutafakari nifanyeje niweze kuwahi maana hata nikichukua kebu (tax) bado ni yale yale…… nawaangalia abiria wenzangu sikuona mwenye sura ya kutabasamu, wengi wamevuta mdomo.
   Nakosa namna naona ni bora niangalie uwezekano wa kuchukua pikipiki (bodaboda), lakini hata hivyo nawaza! Ripoti maalumu wiki iliyopita inaeleza kwamba takriban majeruhi 10 hupelekwa kila siku Muhimbili kutokana na ajali za usafiri huu…. Ni kweli lakini nitafanyaje.
   Halmashauri yangu ya kichwa inafikia muafaka, naamua kuchukua pikipiki … sina ujanja ni lazima niwahi miadi. Hata kama nitapitia njia gani kwa usafiri wa daladala nitakuwa ni kama najisumbua tu! hiki ni kilio cha wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam, Baada ya kama dakika 10 nafikia mwisho wa safari yangu; namlipa dereva pesa yake na kumuacha aendelee na mambo yake.
   Naingia kwenye moja ya kituo kikubwa cha usalama barabarani, ni Kituo cha Kati jijini Dar es Salaam, wengi wamezoea kukiita Central. Nafika kituoni hapo nawakuta maaskari (trafiki) wengi lakini mmoja wao alinipeleka hadi kwa Mkuuu wa Kituo hicho, Inspekta Leopord Fungu, baada ya kusalimiana nae na kujitambulisha kwake, ananikaribisha   kiti tunaanza mazungumzo.
   Miongoni mwa maswali yangu kwake ni; kwa nini jiji la Dar es Salaam, limekuwa na msongamano mkubwa wa magari?  Na jeshi la Polisi linanyooshewa vidole kuwa ni sababu kubwa, hasa uongozaji magari kwenye makutano ya bara bara wakati kuna taa maalumu?
   Majibu ya Inspekta Fungu ni haya:  “Unajua wananchi wa Tanzania, na hasa wakazi wa Dar… hawana shukrani….jeshi la polisi kikosi cha Usalama Bara barani tunafanyakazi kubwa kwa uwezo wetu wote, lakini hawaoni wanatazama kasoro tu….basi, lakini ndio ubinadamu wenyewe.
    …Sisi tulikuwa watu wa kupongezwa kwa mazuri japo sawa tungekemewa kwa mabaya, lakini wakazi wa jiji hili wanajua kulaumu tu,”
   Akichambua sababu za msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, Mkuu huyo anaeleza kwa ubovu wa barabara nyingi zinazoingia na kutoka kati kati ya jiji ni miongoni mwa sababu.
   Kwa kuwa bara bara nyingi hazifanyiwi ukarabati wa mara kwa mara zina mashimo makubwa ambayo huwalazimu madreva kuendesha kwa mwendo wa tahadhari  na  hivyo kuongeza msongamano, lakini pia barabara zingine zimejengwa chini ya viwango.
   “Kwa mfano barabara ya Kilwa muundo wake ni kama chupa ya soda , upande mmoja ni pana wakati upande mwingine umebanwa, Tanroads walitakiwa wapanue barabara hiyo hadi maeneo ya Kamata,”alisema  Ispekta huyo.
   Alifafanua kuwa sababu nyingine kubwa inayosababisha msongamano huo wa magari ni ukweli kuwa karibu ofisi zote za Serikali na watu binafsi zipo kati kati ya jiji (City centre) hivyo magari yote ya watu binafsi na ya Serikali hueleke huko, hasa asubuhi na kutoka jioni.
   “Ofisi zote za Serikali zipo City Centre, lakini ofisi zingekuwa kama ilivyo ile ya Wizara ya Kilimo….. basi msongamano usingekuwa kama ulivyo sasa,” alisema na kuongezea:
   “Mbaya zaidi ofisi hizo pamoja na kuwa katikati ya mji bado hakuna maegesho ya magari….. katika hali kama hiyo magari yanawekwa ovyo na sasa hata dhana ya kuwa na njia moja (one way) imepotea.”
   Mkuu huyo anafafanua kuwa hakuna haja ya Tanroads kuwa na patrol kutokana na kwamba hakuna kazi inayofanywa, pamoja na wao kuwepo barabarani, bado mashimo yapo na hakuna jitihada zozote wanazozichukua.
   Kwa upande wa ajali za pikipiki afande Fungu,  anafafanua kuwa, Jeshi la polisi kikosi cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na kampuni ya Apec wameanza kutoa mafunzo maalumu kwa maderva na kwamba hadi sasa zaidi ya maderva wa pikipiki 1500 wameshapata mafunzo hayo yaliyoanza rasmi mwishoni mwa mwaka 2010.
   Pia alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na ufuatiliaji mkubwa kwa wale wote wanaopewa leseni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wana vyeti vya kufuzu mafunzo ya udereva kuangalia umri wao na kujaribiwa kabla ya kupewa leseni hizo.
   Mbali na hayo, Mkuu huyo anaeleza kwamba ikiwa Manispaa za jiji la Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wakala wa barabara (Tanroads) watatekeleze wajibu wao kama vile; kutengeneza barabara mara inapohitajika, basi ni wazi itasaidia kuondoa kama si kupunguza kabisa suala la foleni barabarani.
   “Mamlaka husika zinajisahau, mimi mwenyewe nimezifuata mara nyingi  kwa mafano; kwa barabara za Tazara, Msimbazi na Mnazi moja toka mwaka juzi tunaiomba lakini hakuna utekelezaji, pia kwa sasa ni wakati mzuri kwa serikali kutengeneza Fly over Bridges ili kupunguza msongamano huu,” alisema.
   Inspekta Fungu anaeleza pia kuwa, watu wengi wanalalamika kwamba kuwepo kwa watu wa usalama barabarani (traffic) kunaongeza foleni kuliko wanapotumia taa za bararani, katika kuwaongoza na hivyo kutaka askari hao wa usalama barabarani wasiongoze magari, hata hivyo anasema, madai hayo yalishawahi kutokea hata siku za nyuma na watu wakamfuata Tibaigana (aliyekuwa kamanda wa kanda maalumu ya Polisi Dar es Salaam) wakamwambia kuwa trafiki wasiongoze magari, lakini cha kushangaza baada ya siku mbili tu, wananchi hao hao waliomba tena trafiki waendelee na kazi yao.
   Mmoja wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, aliyezungumzia adha ya msongamano wa magari Dar ni Dk. Yunus Chambi, Mhadhari wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine, ambaye alisema:
   “Mimi ni mchumi na nimefanya utafiti na kuandika ripori kuhusu athari za uchumi kutokana na msongamano wa magari Dar…..nikubwa kuliko watu wanavyofikiria.
   Mfano; wakati naishi Botswana miaka mitano iliyopita nilikuwa nafundisha vyuo vinne kwa siku na niliweza kulipwa fedha nyingi, nilikuwa namaliza kipindi chuo kimoja na nasafiri kwa basi la kawaida tu naenda mji mwingine nawahi vipindi nafundisha nikimaliza naenda tena kwingine, lakini Dar es Salaam huwezi kufanya hivyo.
   Katika utafiti wangu niligundua kuwa kuna maelfu ya watu wenye taaluma ambao wangeweza kufanyakazi sehemu mbali mbali kama washauri, laikini kwa Tanzania ni ngumu. Ni kwa sababu hiyo serikali inalipa wataalamu washauri wa kigeni, kiasi cha Shilingi Milioni 40, kwa mwezi kwa kuwa hawezi kufanya kazi mbili. Nilazim ifafanye hivyo tu.
   “Siku moja nilimfuata mke wangu ambaye ni mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam, sehemu  ya Ualimu Chang’ombe, nakumbuka niliondoka pale saa 10, jioni  na foleni ilikuwa ya ajabu sana, nilifika nyumbani Mbezi Beach saa nne usiku na nilipoangalia gari nilikuwa nimetumia mafuta ya Shilingi  40,000. Hiki ni kiasi kikubwa sana  cha matumizi ya mafuta kwa safari moja tu,” alisema na kuongeza:
   “Kutokana na hali hii watumishi wengi wa umma wanabaki masikini kwa kuwa hata kama wanauwezo wa kujifanyia kazi nyingine ya kuingiza kipato baada ya kazi, hawawezi lazima akitoka kazini saa tisa afikirie vita ya kupanda dala dala  na kubanwa huku jasho jingi likimtiririka na  magari hayaendi.”
  
   SULUHISHO
   Mchumi huyu anasema kuwa  kupanua barabara pekee si suluhisho la tatizo, jiji kama  Dar linahitaji mipango yakinifu na utekelezaji wa kujitoa, unaolenga kuweka miundombinu ya kisasa kama vile gari moshi linalotoka Morogoro mpaka  kati kati ya jiji na lingine linalokatisha  jiji kutoka Bagamoyo hadi Kongowe Mbagala ambayo  yenyewe itawavutia watu kutoka  mjini na kuishi  nje.
   Anasema kuwa mfumo huo hauendani na mipango ya muda mrefu ya kuondoa ofisi muhimu kati kati ya jiji na kuweka mabasi makubwa yenye mazingira mazuri yatakayoshawishi watu kupunguza matumizi ya magari binafsi.
   Baadhi ya madareva wa mabasi waliolalamikia  msongamano wa magari wanasema kuwa  kuna nyakati ambazo wanalazimika  kuegesha magari wasubiri hali ibadilike kwa kuwa  bei ya mafuta ni kubwa sana kwa sasa hivyo ni hasara kuliacha gari kwenye foleni.
   Mmoja wa Madereva hao, Bw. John Shaaban,  mkazi wa Kimara alisema kuwa  anawaonea huruma wanafunzi ambao huvaa  unifomu  nyeupe  na kuingia kwenye vita ya kupanda gari asubuhi  kisha wanachafuka wakifika shuleni wanachapwa kwa uchafu.
   “Mara nyingi nimewahurumia wanafunzi wanyonge hasa mabinti unakuta inafika saa tatu hajaondoka kituoni wenzake wenye mabavu tayari wameshamaliza kipindi darasani. Wengine unakuta wanajiingiza kwenye vitendo vya ngono na madereva ili tu wapate lift ya kuwafikisha shule inasikitisha sana,”alisema.
   Akizungumzia  hali hiyo, Mwalimu mmoja wa Shule ya sekondari ya Makongo jijini Dar es Salaam, jina tunalihifadhi kwa sasa alisema kuwa  wakati mwingine anapoona wanafunzi waliochelewa wakiadhibiwa na askari(MP)  inauma kwa kuwa  unajua kuwa wengi si makusudi yao kuchelewa, lakini ni foleni.
   Kisha anaongeza: “Kwa kweli weanafunzi ni watu wa kipato cha chini  wanateseka sana. Wakati mwingine wanaacha kufikiria masomo anafikiria jinsi atakavyopambana kupata gari, kwenye mitihani ya mwisho wanafanya mtihani mmoja hii sio sawa.”
   Afisa Mipango wa jiji la Dar es Salaam,  hakupatikana kuzungumzia suala hili, lakini mmoja wa maofisa wa ofisi  yake aliliambia Jibu la Maisha  kuwa hata serikali inapasua kichwa kutafuata suluhisho la msongamano huo.
   “Kwa upande wa Serikali inajitahidi  sana ilipanua bara bara  ya Mlandizi, sasa inapanua barabara ya Tegeta kwa msaada wa Japan, lakini hata yenyewe haitakuwa suluhisho la kudumu. Kwani hakuna udhibiti wa uagizaji magari; unajua mimi nashangaa ninapoambiwa eti Tanzania watu ni masikini wakati kila siku wananunua magari ya kifahari na ndiyo yaliyojaa bara barani,”alisema na kuongeza:
   “Mimi  nakaa Ubungo  kwenye nyumba ya kupanga tu, lakini akina dada  wapangaji wenzangu  wanne wote kila mmoja ana gari  na analitumia kwenda kazini mjini…fikiria wote hawa wanafanya kazi za kawaida hotelini, lakini nwanamiliki magari na wanatoka nayo kila siku unadhani foleni itapungua? Watanzania nao wanapenda sana anasa. Mtu hana hata kibanda, lakini anamiliki gari mbili moja inambeba mkewe, na moja anatumia yeye ….tena wote wanaenda kazini eneo moja unadhani foleni itaisha.”
   Anasema kuwa majiji makubwa kama New York, Marekani ustaarabu uko kwanza kwenye vichwa vya watu, wanajali taifa lao, hawawezi kugeuza jiji lao kuwa jalala la magari mabovu au  ya wizi toka nje. Wao wenyewe ni wapambanaji wa foleni.
   Jiji la Dar es Salam, ni miongoni mwa majiji katika ukanda huu wa Afrika Mashariki yenye watu wengi wanaotoka kila kona ya Tanzania kitu ambacho kwa namna moja au nyingine ni sababisho la msongamano wa watu na magari.

No comments:

Post a Comment