OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, June 26, 2011

Kanisa Dar lachomwa moto

* Madhababu yabaki majivu, nyaraka za kanisa zateketea
WATU wasiojulikana wamevamia na kuchoma moto kanisa moja maeneo ya Ilala, jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita na kuangamiza madhababu yake ambayo ilibaki majivu matupu, ikiwa ni pamoja na nyaraka mbalimbali za kanisa kuteketea.
Unyama huo ambao unasadikiwa kufanywa majira ya saa nane usiku, ulitokea katika Kanisa la TAG, Shekila Makoka, kata ya Kimanga jijini Dar es Salaam, baada ya Mchungaji wa kanisa hilo, Erasto Kihongo, pamoja na baadhi ya washirika wake kwenda kanisa hapo kwa ajili ya maombi ya alfajiri.
“Ilikuwa ni alfajiri na mapema, majira ya saa 11:00 nilikuwa mimi na baadhi ya waumini tukienda kuomba kama kawaida, lakini kabla ya kufika katika jengo la kanisa tulishangaa kuona moto tena ukimalizikia, unajua kanisa hilo bado tulikuwa tukiendelea na ujenzi,” alisema Mchungaji huyo.
Alisema kwamba, walipozidi kusogea zaidi ndipo walipobaini kuwa, mtu au watu waliokuwa wakihusika na kitendo hicho walikusanya vitu kadha wa kadha na kuviweka pamoja madhabahuni na kisha kuviwashia moto.
“Inaonekana kwamba huyu mtu alikusanya vitu na vyombo mbalimbali vya madhabahuni ikiwa ni pamoja na vitambaa, alivikusanya pamoja na ndipo alipoamua kuvichoma, sijui lengo lake lilikuwa ni nini? Mimi sina ugomvi na mtu yoyote wala sikumbuki hata kama niliwahi kukwaruzana na mtu,” alisema Mchungaji huyo wa section ya Ilala.
Alisema kwamba, ingawa kitendo hicho kilifanyika wakati wao wakiwa wamejiandaa kabisa kuingia kwenye maombi, hakikuwafanya waache azma yao hiyo na hivyo waliingia kwenye maombi kama kawaida.
“Kuunguzwa kwa kanisa, hakutufanya tuahirishe maombi, tuliingia kwenye maombi na baada ya hapo tulijipanga, wengine walienda Polisi kutoa taarifa ya kuchomewa kanisa, na wengine walienda kwenye Serikali za mitaa” alisema na kuongeza:
“Tulienda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Tembo Mgwaza na tulipewa karatasi ya taarifa RB No. TMG/RB/1736/2011, na walituambia watatupeleka katika kituo kingine cha Stakishari ili tupewe mpelelezi, lakini mimi sikuona ulazima wa kufanya hivyo mimi jambo ninalomshukuru Mungu ni kuwa, kanisa halikuteketea lote, madhababu ndiyo imeharibiwa vibaya.”
Sambamba na hilo alisema kwamba, alikwisha kutoa taarifa kwa viongozi wake wa kanisa Seksheni ya Ilala kwa Mwangalizi Eliya Lugwami na taratibu zingine zinafanywa.

No comments:

Post a Comment