OTHER WEBSITE LISTS


Monday, June 13, 2011

Bunge la bajeti lisigeuke maonyesho ya kisiasa


      KWA wakati huu mamia ya wawakilishi wa Watanzania zaidi ya milioni 40, wanakutana kwa muda mrefu mjini Dodoma kuhudhuria vikao vya bunge vinavyojadili bajeti.
  Kwa lugha nyingine wawakilishi zaidi kidogo ya 300, wanakutana jikoni kugawana chakula ambacho ni haki ya Watanzania ili kila mmoja afaidi matunda yatokanayo na rasilimali za taifa lake, kodi yake anayolipa, pamoja na kumpa fursa ya kufurahia kuumbwa kwake katika sayari hii.
  Kimsingi jikoni ndipo mahali panapoamua afya za wanafamilia, mgawanyo wa chakula ukiwa mbaya, wapo wengine wataneemeka na wengine watakonda na hata kufa kwa utapia mlo na kadhalika. Pia wapishi wanaweza wasikumbwe na dhambi ya ubaguzi inayowafanya wagawanye chakula kwa upendeleo, lakini wakaingia katika hatua nyingine mbaya zaidi ya kujipendelea wao wakajijazia mabeseni huku wengine wakipakuliwa kwenye visosi vya chai.
  Wapishi wanakabiliwa na hatari nyingine, wanaweza wasijipendelee, wasibague lakini wakasinzia jikoni hadi chakula kikaungua au kuporwa na wanyang’anyi waliojaa kila kona wakikimezea mate kama mbwa mwenye njaa. Wakishtuka usingizini na kukuta wanyang’anyi wameshakila wanasalia katika maonyesho ya suti jikoni na werevu wa kuongopa kwa kutumia dhana za kisiasa.
  Wabunge wanaotumia mamilioni ya shilingi kila siku Dodoma kujadili mgawanyo wa zaidi ya Trilioni 13.5, tunawaasa wajiepushe na yote tuliotaja hapo juu ili waendelee kuwa na sifa ya kuwa wapishi bora na wenye kuleta tumaini kwa wale waliowatuma.
  Wachangie hoja wakiwa wanadamu huru wenye kuwasilisha hoja za wale waliowatuma na si matakwa ya vyama vya kisiasa ambavyo vingi vimeoza kwa rushwa na  ulevi wa madaraka.
  Tunawaasa wasikubali saini zao kutumika kama muhuri wa kuidhinisha matumizi ya kifisadi wakati maelfu ya Watanzania wanashinda njaa, hospitalini si tu kwamba hakuna dawa, bali hata vipimo vya kubaini Virusi Vya Ukimwi hakuna.
  Wanaweza wakadhani kuwa werevu wao wa kupindua katika siasa utawasaidia kupindua maneno na kutoa rushwa kwa baadhi ya Watanzania waliokufa kimaadili na kupata kura kila wakati, la hasha! watajidanganya.
  Teknolojia ya habari inakua kwa kasi na ifikapo 2015, wakati wa uchaguzi Watanzania watakuwa werevu zaidi kuliko sasa, hata mkazi wa kijijini  atakuwa na  uwezo wa kulinganisha ahadi za kisiasa na matokeo ya utekelezaji na hapo atafanya hukumu ya haki  itakayokuwa kilio na janga kwa wanasiasa wanaoendekeza maonesho ya suti, ubingwa wa kusinzia bungeni (tukumbuke kanuni ya Bunge inasema kulala si kukosa, kosa ni kukoroma ukiwa usingizini) na wale ambao ni kama mihuri ya kupitisha maamuzi ya vyama  vyao, badala ya kujali maslahi ya Watanzania.
  Kwa sababu hizo maslahi ya Tanzania yanaweza kulindwa kwa ubora zaidi na mbunge wa bunge la makabwela kule London kuliko mtanzania anayeendekeza maonesho bungeni. Tulishuhudia katika sakata la rada, hatupendi kukumbusha machungu haya kwa watanzania.
  Itoshe tu kukumbushana kuwa kila mtanzania anawajibu fulani ambao asipokuwa tayari kuutolea hesabu kwa wanadamu wenzake leo au akiwa mjanja wa kukwepa hoja sasa, wakati unakuja ambao atasimama mbele ya yule anayejua vyote; ni hapo atakapodaiwa kutoa hesabu ya kweli kulingana na nafasi alizopata kwa kuwa, yeye ndiye asimamishaye wafalme na kuwaangusha.
  Tunasisitiza kuwa, ufisadi si kuuza Twiga hai uarabuni au kuingia mikataba kwa maslahi binafsi pekee, bali hata kupokea mshahara wa mbunge, posho kubwa ya kila siku milioni 70 hivi, anapomaliza miaka mitano, wakati ambapo bungeni anakwenda kushiriki kwenye maonesho ya suti, vitambi na ubingwa wa kulala bila kukoroma, huku hoja muhimu kwa maslahi ya maskini na wanyonge, zikipitishwa bila kupingwa kama glasi ya juisi kwenye koo la  msafiri jangwani.
  Huo nao ni ufisadi  unaodai malipo ya haki  na  siku moja wahusika watalipa  hata kama itakuwa ni kwa machozi. 

No comments:

Post a Comment