OTHER WEBSITE LISTS


Monday, July 11, 2011

Kima cha chini cha mishahara moto mkali

WIKI iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Managementi ya Utumishi wa Umma, Bi.Hawa Ghasia, alitangaza bungeni juu ya kupanda kwa mishahara kwa asilimia 40.2, huku akichanganua kuwa wataajiri watumishi zaidi ya 60 elfu ikiwa ni pamoja na kupandisha vyeo watumishi takribani 80,050 ambapo hata hivyo hakuweka wazi juu ya kima cha chini na cha juu cha mshahara,hali inayozua sintofahamu.

Wakiongea na Jibu la Maisha, wadau mbalimbali juu ya suala hilo, walisema kwamba, ikiwa serikali imekuwa ya kwanza kuwataka watumishi wake; wakiwemo Wabunge kutaja mali walizonazo bila kificho chochote, ni dhahiri kuwa walipaswa kutokuwa na kificho juu ya ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi wake.

Mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kwamba, kutotangaza kiwango cha kima cha chini na cha juu mishahara na kutaja tu kwamba bajeti ni trillion 3.2 ni ukiukwaji wa haki, kutokana kwamba nyakati hizi ni za ukweli na uwazi, kama ambavyo Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa akifanya.

“Kwa nini waogope kutaja, kama kweli ni kiwango kinachokidhi mfumuko wa bei kwa nini iwe kificho, inaonekana ni kiwango kidogo sana kimewekwa ndio maana wanapata kigugumizi, sasa watajuaje kama wanapunjwa; kutosema ni kuficha uovu,” alisema na kuongeza:

“Hii ndio maana viongozi wengine wanashindwa kutangaza mali walizo nazo, jambo ambalo si uadilifu, kwamba mishahara imepanda ni siasa tu kwa namna moja au nyingine inaweza kuleta mafarakano katika ndoa.”

Askofu wa Jimbo la Mashariki wa kanisa la TAG, Lawrence Kametta akitoa maoni yake alisema kwamba, hata kama kiwango cha mishahara kitapanda kama Waziri wa nchi ofisi ya rais management ya utumishi wa umma, Hawa Ghasia alivyosema, lakini serikali bado ina wajibu wa kufunga mianya ya mfumuko wa bei kwani, kwa kima cha chini bado hakitaweza kumfanya mtu kuishi bila kukuna kichwa.

“Mtu ukimpandishia mshahara kutoka laki moja mpaka laki moja na nusu, kama gharama za maisha ziko juu ni wazi kuwa, hazitaweza kumsaidia kitu,” alisema Askofu Kametta na akaongeza:

“Hapo awali serikali ilitangaza kuwalipa walimu malimbikizo ya madeni yao pamoja na kuongeza mshahara lakini mwisho wa siku haikufanya hivyo mpaka walimu wakaitisha mgomo, pia kutotaja kiwango halisi ni unyonyaji, mara nyingi imekuwa maarufu sana kutamka lakini utekelezaji ni duni.”

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Profesa Malise Kaisi akiongea na Jibu la Maisha alisema kuwa, serikali kushindwa kusema hadharani kuwa kima cha chini na juu ni shilingi ngapi kwa sasa sio kitu, isipokuwa watu wasubiri hadi pale watakapoanza kupewa hilo ongezeko na ndipo waweze kutoa maoni yao.

Mimi naona watu wangeipa serikali muda, wasubiri hadi watakapopewa hilo ongezeko na hapo ndipo watajua kwamba linakidhi mahitaji au la,” alisema Profesa huyo mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Mchungaji Bruno Mwakibolwa wa Kanisa la EAGT, Mito ya Baraka la jijini Dar es Salaam, kwa upande wake alikuwa na haya ya kusema: “Serikali nayo ni mwanadamu, hivyo kwa namna moja au nyingine ina mapungufu na inaweza kukosea, hivyo katika hilo la mishahara pia tunapaswa kuwaombea kama tunavyoomba katika mambo mengine.”

Sambamba na hilo alisema, watu wengi huwa ni wepesi wa kulaumu, ambapo aliongeza kwamba Biblia inakataza kulaumu kwani; mtu wa jinsi hiyo mwisho wa siku naye huja kulaumiwa.

Wiki iliyopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais management ya utumishi wa umma, Hawa Ghasia alipokuwa akiwasilisha bajeti yake bungeni alishindwa kutangaza nyongeza ya mishahara ya watumishi wa Umma, ingawa kupitia Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo iliahidiwa kufanya hivyo, hata hivyo serikali ilisema itatumia shilingi trillion 3.2 katika mwaka huu wa fedha, huku ikisema kuwa, mishahara imeongezeka kwa asilimia 40.2.

No comments:

Post a Comment