OTHER WEBSITE LISTS


Monday, July 11, 2011

Mchungaji afungwa jela kwa kuombea mgonjwa

MCHUNGAJI Yerzhan Ushanov, anayemtumikia Mungu katika kanisa la New Life Protestant la jijini Taraz, nchini Kazakhstan, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumwombea mgonjwa kwa jina la Yesu akapokea uponyaji na kuwa mzima.

Mashtaka ya Mchungaji huyo inaelezwa kuwa ni ya kutungwa kama yale aliyoshtakiwa nayo mtangulizi wa imani yake, yaani Bwana Yesu Kristo Mbele Ya Baraza la Sanhedrin na kuhukumiwa adhabu ya kusulubiwa hadi kufa.

Walioshuhudia mkasa huo uliotokea katika mji wa Taraz,nchini Kazakhstan, walisema kuwa Mchungaji Ushanov,ambaye amekuwa akiendesha huduma ya maombezi kwa makundi na kwa mtu mmoja mmoja alitegwa na polisi wa kikosi cha siri chenye jukumu la kukabiliana na Ukristo nchini humo (KNB)ili kipate sababu za kumshtaki.

Katika mashtaka yao KNB, wanadai kuwa Mchungaji Ushanov, alimzuru mtu mmoja ambaye alimuombea kwa jina la Yesu jambo ambalo ni kosa kwa kuwa maombi hayo yalimdhalilisha mumewe

KNB KUPEKUA NYUMBANI KWA MCHUNGAJI

Siku chache kabla ya Mchungaji Ushanov, kufunguliwa mashtaka na polisi wa kikosi cha KNB, huku wakiwa wameambatana na makaptani wawili, Aleksandr Bychko na Galymzhan Jumashev, walivamia nyumba ya Mtumishi huyo wa Mungu na kupekua kila kitu ambapo walimwambia kwamba, kuna mwanaume mmoja Aleksandr Kereyev ameshtaki kwamba mke wake Nauryzbayeva afya yake imekuwa ni mbaya baada ya kutoka katika kanisa lake

Sambamba na hilo waumini wa kanisa hilo, ambao hawakuwa radhi kutaja majina yao walisema kwamba, madai hayo ni ya uongo na kuwa hata kitendo cha Polisi kuingia na kufanya upekuzi kwa Mchungaji ilikuwa ni kutafuta ushahidi feki kinyume na mtumishi huyo.

“Wakati wa kupekuwa walimuamuru Mchungaji aende nje ili awaambie waumini waliokuwa wamezunguka nyumba yake wasimsumbue, na aliporudi ndani na kuangalia kwenye shelfu yake ya vitabu aliona kitabu kipya asichokijua kikiwa kimeandikwa ‘Modern Hypnosis in Russian Kitu ambacho hata yeye hakujua kimetoka wapi,” ilielezwa Forum 18 na kuongeza:

“KNB walichukua laptop computer mbili, external computer hard drive 150 DVDs ambayo ilikuwa na mambo mbalimbali ya kikristo yapatayo 20, pia walichukua vitabu na kumbukumbu za waumini ikiwa ni pamoja na namba zao za simu na anwani.

ATAKIWA AACHE KAZI YA KICHUNGAJI AU KUHAMA MJI

Tangu kashi kashi hilo la Mchungaji, Kapteni Jumashev na mwenzake colleagues, wamekuwa wakimuonya mtumishi huyo kubadilisha kazi ili aweze kuishi vizuri, lakini akishindwa kabisa basi itampasa kuhama mji kwa usalama wake

Sambamba na hilo waumini wa kanisa hilo waliliambia Forum kwamba makaptani hao wamekuwa wakienda kanisani hapo na kuwawekea alama watu wanaomwamini Kristo, na kwamba wamekuwa kinyume na kanisa lao.

MWANZO WA KUVAMIWA KWA NEW LIFE

Katikati mwa mwezi April na Mei kundi hilo la Polisi wa KNB walivamia makusanyiko manne tofauti yaliyokuwa yamepangwa kihalali na kanisa la New Life katika maeneo ya Kazakhstan, na kama hilo halitoshi April 29 walivamia tena kanisa la new Life lililopo eneo la jirani wakamkamata Mchungaji, mkewe na watoto kisha kuwapeleka Polisi.

Sambamba na hilo Kaskazini mwa mji wa Kazakhstan, kwenye maeneo ya Petropavl, Idara ya KNB walivamia na kumsumbua mkurugenzi mmoja wa shule binafsi wakimtaka kuvunja mkataka na Kanisa la New Life, ambalo lilikuwa lifanye mkutano katika viunga vya shule hiyo;

baada ya kufikwa na taftani hiyo, waliomba wapewe muda wa saa moja ili waweze kukutana katika mgahawa uliokuwa ndani ya shule hiyo, lakini hata hivyo kabla hawajafanya zoezi hilo, walipigiwa simu ya vitisho kutoka kwa polisi wa KNB jambo ambalo hawakuweza kufanya mkutano maeneo mengine.

Hatima ya Mchungaji aliyekamtwa na kushtakiwa kuombea mgonjwa ambaye wala hakufikishwa mahakamani na wala kesi haikuendeshwa katika mazingira ya uwazi, bado ni kitendawili kisicho na majibu na hakuna ajueye mahali alipo kwa sasa.

Wakati huo huo Mahakama Kuu nchini Iran, imemuhukumu kifo Mchungaji Yousef Nadarkhani wa Kanisa la Church of Iran, kwa kufanya uinjilisti kwa watu pasipo idhini ya serikali, jambo ambalo hata hivyo limepingwa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo, jumuiya ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Christian Solidarity Worldwide, Mchungaji Yousef alikamatwa mwezi Oktoba mwaka 2009 kutokana na kuanzisha kanisa la nyumbani katika mji Rasht na kumfungulia kesi kwa madai kuwa alikwenda kinyume cha sheria ya kiislamu ya nchi hiyo ambayo inakataza injili kuhubiri kwa wana wa Iran.

Mchungaji huyo ambaye sasa anashikiliwa katika Gereza la mjini Lakan, imepelekea makanisa mengine kuwa na wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa wimbi la wapinga ukristo.

MWANAMKE AUZA NYUMBA ILI KUHUBIRI INJILI AFRIKA

KAMA ilivyo kwa baadhi ya waafrika kuwa na ndoto, kiu ya kupeleka injili ya Yesu kristo nchi za Magharibi hasa katika nchi za bara la Ulaya ndivyo ilivyo mtokea Bi. Rosemary Gibbons wa Australia ambaye baada ya kupewa wito na Bwana aliamua kuuza nyumba ili kuja Afrika kuhubiri injili.

Huku akiamini kwamba kuhubiri injili ya Kristo, inahitaji kujitoa kwa hali zote ikiwa ni pamoja na mali, mwanamke huyo aliamua kuuza kila kilicho chake na kwenda nchini Malawi kusambaza ujumbe wa Yesu Kristo katika siku hizi za mwisho.

Bi. Rosemary ambaye ni Mmissionari na Mwinjilisti mwenye elimu ya chuo kikuu, ambaye pia aliwahi kuwa mwalimu nchini mwake, alifikia uamuzi huo miaka kadhaa iliyopita, ambapo alianzia kwa kufanya kazi katika shule moja ya seminari

Rosemary alihitimu elimu yake ya chuo kikuu katika chuo cha Central Missouri University, baada ya hapo akapata nafasi ya kufanya kazi kama mwalimu kwenye baadhi ya shule nchini kwake ambapo aliacha na kujiunga na shirika la habari lijulikanalo kama Public Television, kisha kujiunga na Kauffman Foundation ya Kansas City.

Alifanikiwa kujiunga na shirika la Sheffield Family Life Center ambapo mwaka 1997 alipata nafasi ya kwenda Malawi alipoalikwa kufundisha course ya uongozi kwa muda wa wiki tano.

“Wakati huo ndipo Mungu aliposema na mimi kuwa natakiwa kuwa mahali pale,” alisema Rosemary muda mfupi baada ya kuwasili Amerika na baada ya hapo akapata jukumu la kuuza nyumba yake iliyopo Kansas City na mwaka 1999 akarudi Malawi alipokuwa akifundisha watu kuwa viongozi ambapo alikutana na Mhubiri Rev. Moffat Phiri ambaye alikuwa akihudhuria masomo ya Seminary.

Mwinjilisti huyu amekuwa akihubiri kwenye makanisa mbalimbali kwa msaada wa Australia ambao walikuwa wakimsaidia tangu akiwa shuleni, alikuwa akifundisha masomo mawili ambayo ni Theolojia pamoja na Stadi za maisha.

“Baada ya miaka michache Mungu akatupa maono ya kujenga kanisa ambalo tulilijenga maili 50 kutoka nje ya mji,” alibainisha Rosemary na mume wake Phili na kuongeza: “Tumeamua kuwasaidia watoto yatima ambapo hadi hivi sasa tuna yatima 12 ambao tunataka waendelee.”

Kabla ya kuanza kufundisha kijijini hapo, walianza kukusanyika kwenye nyumba moja ya Mzungu na kuanza kuabudu wakiwa watu 12. Hivi sasa watu zaidi ya 500 wanahudhuria ibada hiyo jambo ambalo imelifanya kuwa moja ya makanisa makubwa katika eneo la Malawi Kaskazini; na hata kuwa nguvu kubwa kwa matajiri na wasomi.

Alitanabaisha kwamba wamekuwa wakipokea vitu vya gharama kutoka kwa mfanyabiashara maarufu nchini kwao kama; Frank Moseley wa Kansas City Christian ikiwa ni pamoja na kadi ya SOS ambayo imeandaliwa kwa ajili kuwaelekeza watu kwa Yesu, na shirika la mpango wa kueneza injili wa Moseley inayoitwa “You’re Some One Special.”

Sambamba na hilo hadi sasa kadi hizo zimeweza kusambazwa katika nchi zaidi ya 20 ikiwemo India ambayo itasaidia watu kutoka katika dhambi pamoja na vifungo vyote vya ibilisi.

Watu wengi wakiwemo wanawake kwa wanaume wameweza kushiriki katika kusoma kadi hizo na mamia ya watu wameweza kufikiwa na ujumbe wa Kristo na hata kwenye makanisa pia.

Mwana mama huyo wa Kansas City, kutokana na imani yake aliacha kila kitu kwa ajili ya kuisaidia Malawi mbali na mambo injili, pia wamekuwa wakisaidia katika nyanja mbalimbali za kijamii likiwemo la kifedha na Elimu ya juu ambapo kwa kushirikiana na mumewe wamekuwa wakisaidia na watoto kwa ujumla.

Japo bado kuna mahitaji makubwa ambayo kwa namna moja au nyingine watu wanakabiliana nayo lakini, Mwinjilisti huyu amekuwa akisaidia yatima na wanaosumbuliwa na njaa sambamba na wale waliopoteza mzazi au wazazi kwa ugonjwa wa Ukimwi.

“Nchini Malawi shule za sekondari ni lazima mtoto ajilipie mwenyewe vitabu na sare za shule, wasiojiuweza ni gumu, sasa mimi husaidia kulipa ada ya shule, kusomesha wanawake,” alisema na kuongeza:

“Kwa siku tunawahudumia watoto 100, kuwalipia wanafunzi 25 ada ya shule lakini kwa sasa tunalipia wanafunzi saba tu kutokana na mtaji kutokuwa vizuri,”

Pia vurugu ambazo zimekuwa zikijitokeza kila mara nchini Malawi kutokana na suala la njaa bado wao hawaziogopi na badala yake wanaendelea kujipa moyo na kumwomba Mungu ili wasiache huduma yao hiyo ikiwa ni pamoja na kujipa moyo kuishi bila kuogopa japo wamejaribu kuvamiwa mara kwa mara.

“Nilipokuwa nikiishi Kansas City nilijitolea kufanya kazi na Rescue Mission, natumika kwa wale waliopoteza matumaini na ninajisikia kuumia ninapoona watu wengine wakionewa na kunyanyaswa.

Mtumishi huyu Bi. Rosemary Gibbons mara nyingi kutokana na huduma yake hiyo watu wamekuwa wakiguswa na mara zote anapopata muda wa kwenda nchini mwake Australia amekuwa akipewa na watu mbalimbali nchini humo vitu kama; Laptop ili kusaidia wasio na uwezo nchini Malawi

No comments:

Post a Comment