OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, July 3, 2011

Usishangae posho, mawaziri hotelini ni kiama

MAWAZIRI na maofisa wengine wa serikali ni watendaji muhimu kwa serikali, tena wenye wajibu mkubwa wa kulinda maslahi ya Tanzania na watanzania kwa kufanya maamuzi magumu, hivyo wanastahili kutazamwa vyema.

Wanastahili kulipwa vyemA, kupata makazi bora pamoja na huduma zingine muhimu, hilo halina ubishi na sote tunakubaliana na nalo, lakini kwamba baadhi yao wanaishi katika hoteli ya hadhi ya nyote nne, na kulipiwa hadi milioni 50, kwa mwezi hili linatushtua na kutupa mashaka makubwa.

Habari za kuaminika kutoka bungeni Dodoma zinaeleza kuwa baadhi ya mawaziri wana miezi saba hotelini wakiishi kama watalii, wakilipiwa mamilioni ya fedha ambazo ni jasho la masikini wa Tanzania waliokatwa vati wakinunua viberiti na sabuni ya kufulia unguo zao chakavu.

Ni aibu isiyo na mfano kwa Waziri kuishi New Afrika Hotel, akilipiwa Dola za Marekani 300 kwa siku, kwa kila chumba huku akiwa na vyumba zaidi ya kimoja.

Naam, si New Afrika pekee, bali wapo wanaoishi Sea Cliff Hotel, ambao inadaiwa kuwa malipo ya Chumba ni hadi Dola 400, kwa siku huku kikifungwa tu nyakati anapokuwa nje ya nchi.

Tunajua kuwa haya sasa ni malipo ya dhambi kuu ya kuuza nyumba za serikali, iliyofanywa na uongozi wa awamu ya tatu, ambao unaitafuta si serikali pekee bali ni umma wa watanzania wote.

Tungeshauri serikali kufanya maamuzi makubwa katika hili, kwa kukodi hata nyumba maalumu zitakazolipiwa kodi kwa mwaka ili kuokoa mamilioni ya shilingi yanayoangamia mahotelini kwa kulipia mawaziri.

Tunajua kuwa si serikali hii inayostahili kulipa gharama ya dhambi ya kuuza nyumba za serikali, lakini tukumbuke wote (serikali ya awamu ya tatu na ya nne) walifanya maamuzi hayo baada ya kutafsiri sera za chama husika.

Itakuwa ni unafiki kukabiliana na ufisadi wa maafisa wa ardhi, waliogawa viwanja vya wazi wakati huu wa kuachia mamilioni yalipiwe kwa makazi ya waziri mmoja hoteli ya nyota nne ukipewa kisogo. Tukumbue katiba yetu inatamka wazi kuwa wanadamu wote ni sawa na wanastahili kutendewa haki.

Tunasisitiza kuwa ufisadi ni ufisadi tu, uwe wa kukwapua fedha tasilimu au kupindisha sera ili kujinufaisha kwa kujiuzia mali za umma, kisha mamilioni ya fedha yatumike kuwalipia mawaziri mamilioni ya fedha ili waishi kama watalii, haiingii akilini.

Tunasisitiza kuwa ni vyema maamuzi makubwa yanayogusa moja kwa moja maisha ya watanzania yakafanywa kwa umakini, huku uzalendo na hofu dhidi ya Mungu aliye baba wa wajane na masikini ikipewa kipaumbele kwa kuwa iko siku wahusika watalipwa sawa sawa na matendo yao.

No comments:

Post a Comment