OTHER WEBSITE LISTS


Sunday, July 3, 2011

Mgao wa umeme wengi wapoteza kazi


UHABA wa nishati ya umeme unaolikabili taifa wakati huu ambao linaelekea katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wake, ni janga la kitaifa ambalo limesababisha idadi kubwa ya wafanyakazi wa viwandani kupoteza ajira, baadhi ya viwanda kufungwa, huku wafanyabishara walio kwenye mikoa ya pembezoni wakitamani kutumia umeme kutoka mataifa mengine.

Wakiongea na Jibu la Maisha kwa nyakati tofauti juu ya sakata la umeme ambalo limekuwa ni tishio kwa waajiriwa, wafanyabiashara na hasa wenye viwanda, wamekiri kuwa wako njia panda, hawajui mustakabali wa maisha yao wala kazi na biashara wanazofanya.

Miongoni mwa wale walioeleza hisia zao kuhusu mgao wa umeme ni mfanyabiashara mashuhuri katika Mkoa wa Arusha, Bw. Baraka Nyanda, ambaye alisema kuwa tatizo la umeme lililoikumba nchi kwa muda mrefu limekuwa tishio kubwa kwa wafanyabiashara, watanzania na hata kwa Waziri husika.

Akisisitiza, Bw. Baraka alisema kuwa inashangaza kuona kuwa hadi sasa Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, alipaswa awe amejiuzulu kwa kuwa ameshindwa kuiongoza Wizara yake katika kubuni sera za kuliwezesha taifa kukabiliana na uhaba wa umeme ingawa Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati hiyo, lakini sasa ni kama hakuna umeme kabisa.

“Hatuwezi kusema kwamba Tanzania kuna umeme, sisi tunajiandaa kuchukua umeme kutoka nchi jirani ya Kenya. Hivi kwani kipindi cha nyuma hakukuwahi kuwa na kiangazi? je kipindi hicho watu walikuwa wakikosa umeme? Sayansi yote hii na teknolojia, watu bado wanataja maji kwamba ndiyo chanzo pekee cha nishati ya umeme! Hii ni aibu,” alisema.

Naye Meneja uzalishaji wa kampuni ya madawa ya AA Pharmaceuticals Limited yenye makao yake Mbezi, jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Boi, akiongea na Jibu la Maisha katika mahojiano maalumu alisema kuwa tatizo la umeme limewafanya wapate hasara kubwa ambayo hawajui itadaiwa na kitu gani kutokana na kufanya kazi mara mbili kwa wiki badala ya siku sita kama ilivyokuwa kabla ya mgao wa umeme.

Alisema kwamba si hilo tu, lakini wamelazimika kupunguza vibarua kutokana na uzalishaji kuwa mdogo na hivyo kutohitaji watendakazi wengi, ingawa si jambo jema ambalo walifurahia kulifanya kutokana na kwamba imefanya watu kukosa chochote cha kupeleka majumbani.

“Imetulazimu kupunguza watu, lakini hata hivyo tumewaambia kwamba umeme utakapokaa vizuri, basi wao watapewa kipaumbele ili waendelee na kazi, unajua nini; sisi tunazalisha bidhaa, lakini tunapokweda kuchukua vifaa vya kufungia bidhaa ‘paking material’ tunashindwa kupata kwa wakati na hata tukipata vinakuwa ni vichache na ni kutokana na suala la umeme kwa ujumla,” alisema na kuongeza:

“Suala la kutumia jenereta Mwandishi ni gharama sana, na hata hivyo kuna mashine zingine tunazotumia hapa umeme wa jenereta hauwezi kuzisukuma.Sisi tunatumia phase 2 na 3, hii ya 3 uwezo wa jenereta ni mdogo hivyo, uzalishaji wetu umepungua kwa asilimia 20.”

Sambamba na hilo alisema kuwa lazima serikali katika mazingira kama haya ijaribu kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na ubunifu kutokana na kwamba, hata kipato kinachotokana na kodi kitashuka.

Jibu la Maisha lilivinjari Kariakoo jijini Dar es Salaam, ili kupata maoni ya wafanyabiashara ambapo pindi umeme unapokosekana, basi soko hilo hugeuka na kuwa kama kiwanda kutokana na kelele za jenereta, ambazo husababisha watu kutoelewana, sio hilo tu, bali pia kwa wale ambao hawana jenereta maduka yao hufungwa hadi hapo umeme unaporudi.

“Hapa hatuelewani hata kidogo, nyumba moja inakuwa na jenereta 20 na zote zinanguruma na kutoa moshi , tuko katika wakati mgumu, tunahofia afya zetu kutokana na moshi, sio hilo tu mwandishi hata mauzo yetu kwa kweli yameshuka, bidhaa za vinywaji kwa sasa haviuziki kabisa na kama ujuavyo jiji letu lilivyo na joto,” alisema mfanya biashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Emmanuel.

Sambamba na hilo Jibu la Maisha liliongea na wauza majenereta ambao na wao huku wakionekana wenye furaha kubwa kuhusiana na kukatika ovyo kwa umeme, walikuwa na haya ya kusema:

“Kwa kweli sio siri biashara kwetu ni nzuri sana, ni neema kubwa kwani kwa siku tangu umeme uanze kutokuwa na utaratibu tumekuwa tukiuza majenereta 15 hadi 20 kwa siku,” alisema Muhindi mmoja ambaye aliogopa kutaja jina lake.

Alisema kwamba nyakati za nyuma walikuwa wakiagiza majenereta machache kutokana na wateja kuwa wachache lakini kipindi hiki imewalazimu kuagiza idadi kubwa kutokana na uhitaji wa watu. Mmoja wa waathirika wa hali hiyo; ni Sungu Mbila, Mkurugenzi wa Kampuni ya SGL System Limited, iliyopo Mtaa wa Muhoro, Kariakoo inayoandaa na kuchapa vifaa vya stationeries, ambaye ameilalamikia Serikali kushindwa kurekebisha tatizo la umeme na kudai kuwa watashindwa kuzitumia vyema mashine walizonunua kutoka TRA kwa kuwa hawataweza kufikia malengo yaliyokadiriwa, pia kulipa wafanyakazi kwa kazi za usiku za masaa ya ziada ni ghali.

Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Shayo; ambaye ni mchapaji (Printer), mwenye Press yake mtaa wa Muhoro, Kariakoo alieleza kuwa amekuwa akilala kiwandani wakati mwingine kutokana na kukatika kwa umeme mchana, kwa lengo la kuuwinda umeme ili aweze kufanya kazi za wateja wake unapopatikana usiku, hali ambayo inawaweka wateja na wenye viwanda kwenye hali ngumu isiyojulikana itaisha lini.

Naye Betty Mwakyusa, mfanyakazi wa Graphics mtaa wa Kongo, Kariakoo jijini Dar es Salaam, anaeleza kuwa; wanatumia gharama kubwa kufanya kazi chache za wateja, kwa kuwa inawalazimu kutumia jenerata, muda mwingi, jambo ambalo linawagharimu zaidi.

Mwingine ni Bw. Urio ambaye anafanya kazi za stationaries katika mtaa wa Nyamwezi, Kariakoo ameeleza kuwa, kwa hivi sasa hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya nchi bila kuondoa tatizo la umeme, maana waathirika wa shida hii ni wengi; uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini ni wa kubahatisha.

Hata hivyo wadau mbalimbali wakiongelea sakata hili la umeme walieleza kwamba, maji si jambo ambalo Wizara inaweza kulitaja kwa sasa kuwa sababu ya kukosekana kwa umeme nchini, wakati kuna njia nyingi mbadala ambazo wanaweza kuzitumia na nchi ikapata umeme.

“Serikali iachane na kutumia chanzo kimoja cha kuleta umeme, kuna njia nyingi ambazo zinaweza kutumiwa na watu wakapata umeme kama; makaa ya mawe, gesi na hata upepo,” alisema Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mh. James Mbatia

Mwananchi mmoja ambaye alitumia shirika la utangazaji la BBC kutoa maoni yake katika kipindi cha Amka na BBC, alieleza kwamba hali ngumu aliyo nayo, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa umeme ni vigumu kusherehekea miaka 50 ya Uhuru vyema bila kutoa tathmini kuwa tunaenda mbele au tunarudi nyuma.

No comments:

Post a Comment